Na NJUMAI NGOTA,
Ruvuma
MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, anatarajia kuanza mikutano ya kampeni mkoani Ruvuma, Septemba 20, 2025.
Mitaa mbalimbali ya mkoani humo, imepambwa na bendera za CCM, yakiwemo mabango ya Mgombea Urais wa Chama, Dk. Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani wanaotokana na CCM.
Baadhi ya wananchi, walionekana mitaani wakiwa wanashauku kubwa ya kusikiliza utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2020-2025 na Ilani mpya ya mwaka 2025-2030.
Dk. Nchimbi, amefanya mikutano ya hadhara ya kampeni za uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu, utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu katika mikoa 11 ambapo alifanya mikutano ya hadhara mikubwa, midogo na ya kusimama njiani kusalimia wananchi waliokuwa wakijitokeza kumlaki.

Mikoa ambayo Mgombea Mwenza wa Urais, tayari amefanya kampeni ni Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Kagera, Rukwa, Katavi, Arusha, Kilimanjaro, Mara na Tanga huku ikihudhuriwa na mamia ya wananchi waliokuwa na shauku kubwa ya kusikiliza sera za Chama, huku wakiahidi kumpigia kura za kishindo Mgombea Urais wa Chama, Dk. Samia, aendelee kuwaletea maendeleo katika maeneo yao.
Balozi Dk. Nchimbi katika mikutano hiyo, alielezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025, ilivyotekelezwa kwa vitendo katika mikoa hiyo na kuinadi Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025/2030.
Dk. Nchimbi, katika mikutano hiyo, aliwaomba wananchi waendelee kukiamini Chama na kuwapigia kura wagombea wanaotokana na CCM akiwemo Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Mgombea Urais wa Chama, aendelee kuwaletea maendeleo miaka mitano ijayo.
Mgombea Mwenza wa Urais akiwa mkoani Ruvuma, anatarajia kufanya mikutano ya hadhara ya kampeni katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Wilaya ya Madaba.

Kwa mujibu wa ratiba ya kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa wagombea Urais na Mwenza, iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Balozi Dk. Nchimbi, leo atasafiri kwenda Litui, Halmashauri ya Nyasa katika mkutano mkubwa wa kampeni.
Pia, Dk. Nchimbi, jioni atakwenda Songea Mjini kwa maandalizi ya kumpokea Dk. Samia, kesho watafanya mkutano wa pamoja Mbambay Bay, Nyasa.
Aidha, ratiba ya kesho kutwa, inaonesha wagombea hao wawili, watakuwa na mkutano mkubwa wa pamoja Songea Mjini.
Baada ya mkutano huo, Mgombea Mwenza wa Urais, Dk. Nchimbi, atakuwa na mkutano mdogo eneo la Madaba, baadaye atakwenda Ludewa Mjini kwa mkutano mkubwa.
Ratiba inaonesha, baada ya kumalizika kwa mkutano huo, atakwenda Njombe Mjini.