Na AMINA KASHEBA
PAMOJA na kupata ushindi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), uongozi wa Simba umetoboa siri kwamba mechi ilikuwa ngumu kutokana na uzuri wa wapinzani wao.
Juzi, Simba ilishinda bao 1-0 dhidi ya Gaborone United katika mchezo uliofanyika nchini Botswana.
Akizungumza kupitia ukurasa wa mtandao wa klabu hiyo, Meneja wa Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally alisema wapinzani wao wana timu nzuri na hawapaswi kubezwa.
“Tunayo furaha kubwa kupata ushindi tulitegemea tutapata upinzani na tulifahamu katika mechi za awali lazima tutakutana na timu zenye ushindani.
“Lakini Elie Mpanzu alipambana na kuhakikisha tunapata ushindi ugenini, tulipoteza nafasi nyingi za kufunga mabao katika mchezo wetu, laskini tunashukuru tumepata pointi tatu,” alisema Ally.
Meneja huyo alifafanua kuwa mechi ya marudiano wana kazi kubwa ya kuzuia na kupambana kupata matokeo mazuri.
“Mechi ya marudiano tuna kazi mkubwa,lakini tutahakikisha tunapambana kupata matokeo mazuri ambayo yatatusaidia kusonga mbele,” alisema meneja huyo Ally.
Hata hivyo, Meneja huyo alisema wamepokea taarifa kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) katika mchezo huo wa marudiano dhidi ya Gaborone United, Simba hairuhusiwi kuingiza mashabiki kutokana na adhabu walipewa.
“Tumefanya mazungumzo na CAF kwa kukata rufaa, hivyo tunasubiri majibu ya rufaa hiyo kama hiyo mechi inaruhusiwa kuwepo kwa mashabiki au hawaruhuwi hivi sasa hatupo katika nafasi nzuri ya kuzungumza, ” alisema Ally.
Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana alisema klabu ya Simba imeonesha hatua mkubwa na utulivu katika mchezo wao dhidi ya Gaborone United.
“Simba imeonesha hatua kubwa, imeonesha mchezo mzuri, nawapongeza Watanzania waliojitokeza kwenda kuiunga mkono timu hiyo hadi imepata ushindi wa bao 1-0,” alisema.
Simba inatarajiwa kushuka dimbani Septemba 28, mwaka huu katika mchezo wa marudiano dhidi ya Gaborone United utaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.