Na MUSSA YUSUPH,
Mtwara
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Chama kinahitaji ushindi wa heshima ambao utawaziba midomo wapinzani.
Amesisitiza kuwa maendeleo yaliyopatikana nchini na maelfu ya wananchi wanaojitokeza kukiunga mkono, hakuna shaka kuhusu ushindi wa chama hicho bali kinachohitajika kwa sasa ni ushindi wa heshima.
Dk. Samia ametoa msisitizo huo katika mikutano yake ya kampeni iliyofanyika katika wilaya za Nanyumbu na Masasi mkoani Mtwara.
Katika mkutano wake uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi eneo la Nangaka wilayani Nanyumbu, Dk. Samia amesisitiza makubwa zaidi yamefanyika nchini katika sekta mbalimbali.
“Ushindi tutashinda Chama Cha Mapinduzi, yanayojitokeza na yaliyofanyika bila shaka tutashinda. Tunataka ushindi wa heshima wa kuwafunga midomo wale wengine.
Alisisitiza: “Tunataka ushindi wa heshima, kwa hiyo tarehe 29 mwezi wa 10 tunaomba kura kwa Chama Cha Mapinduzi kwa mafiga matatu na pamoja tunakuja kujenga taifa letu,” amesema na kushangiliwa.
Ameongeza:” “Hii ni imani yenu kwa Chama Cha Mapinduzi kwa viongozi wenu ambao kwa pamoja tumefanya kazi kulijenga taifa letu.”
SABABU YA KUOMBA KURA
Dk. Samia amesema amewasili mkoani humo kuomba kura baada ya kutimiza miaka mitano ya kwanza.
“Tunarudi kuomba kura kwa kujiamini Chama Cha Mapinduzi, serikali zake ndizo zinazoweza kufanya kazi ya kuinua hali na utu wa Mtanzania.
“Tumefanya miaka mitano iliyopita, tuna imani na tunajiamini tunaweza kufanya miaka mitano inayokuja. Na ndiyo maana tunaomba kura,” alisisitiza.
Amesema mengi yaliyofanyika miaka mitano iliyopita, baadhi yameelezwa vizuri na wagombea ubunge huku wananchi wakishuhudia utekelezaji wake.
Dk. Samia amesema kuanzia shule za msingi na sekondari, vituo vya afya, zahanati, hospitali za wilaya, maji na umeme vyote wananchi wameshuhudia kazi iliyofanyika.
Amewapongeza wananchi kwa kutumia vizuri mbolea na pembejeo za ruzuku zinazotolewa na serikali, hali ambayo imeongeza uzalishaji mazao nchini.
“Ruzuku zimewezesha kuongeza mazao kama korosho kutoka tani 15,000 hadi 24,000. Korosho mara ya mwisho imeingiza ndani ya Nanyumbu sh. bilioni 73 ambazo zipo mikononi mwa wakulima,” alibainisha.
Vilevile, amesema uzalishaji karanga umepanda kutoka tani 26,100 zenye thamani ya sh. bilioni 65 hadi tani 33,170 zenye thamani ya sh. bilioni 82.9.
Amesema katika ufuta uzalishaji umeongezeka kutoka tani 1,580 zenye thamani ya sh. bilioni 3.9 na kuvuka malengo ya kuzalisha tani 11,800 zenye thamani ya bilioni 38.8.
Pia, katika mbaazi amesema zao hilo zamani lilikuwa likitumika kama mboga, lakini sasa limekuwa la kibiashara.
“Tumeongeza uzalishaji mbaazi kwa tani 1,130 ambazo zilikuwa na thamani ya sh. bilioni moja hadi tani 5,950 zenye thamani ya sh. bilioni 10.8 ambazo zimeingia kwa wakulima.
Amesisitiza: “Tukisikia kazi na utu tunasonga mbele, kazi hii ya kuleta pembejeo na mbolea, kukuza kilimo wakulima wapate fedha iliyoingia mikononi mwao ni kuujenga utu wao.”
Dk. Samia amesema fedha hizo zitawawezesha wakulima kujenga makazi bora, kusomesha watoto, kupata matibabu na kuimarisha uchumi wao.
Amebainisha manufaa hayo ni kutokana na ruzuku zinazotolewa, ambapo aliwahakikishia wakulima serikali inakwenda kukamilisha ujenzi wa skimu za umwagiliaji za Likokona, Lukula na Masuguru.
KUTAFUTA MASOKO
Kadhalika, alisema serikali itaendelea kutafuta masoko zaidi kwa kuwa bidhaa hizo ni biashara zenye misimu ya kupanda na kushuka bei.
“Serikali yenu tunaendelea kutafuta masoko zaidi kulinda bei za mazao ambayo kiuhalisia hutegemea soko la kimataifa.
“Tupo katika mazungumzo na hatupo katika hatua mbaya, kwani bei hazitoshuka kama vile ambavyo watu wanasema,” alieleza.
Katika kuhakikisha mazao ya wakulima yanauzwa kwa bei ya uhakika, serikali itaanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao.
Alisema kongani za viwanda zitawekwa katika maeneo mbalimbali badala ya kuuza malighafi, yauzwe mazao yaliyoongezewa thamani.
Kuhusu umeme, alisema serikali inatekeleza mradi wa gridi imara wenye thamani ya sh. bilioni 300.7, ambapo itajengwa njia ya kusafirishia umeme kutoka Songea hadi Tunduru kisha Masasi.
Alibainisha pia kutajengwa vituo viwili vya kupoza umeme kimoja Tunduru ambacho kimefikia asilimia 50 na kingine Masasi.
“Lengo la vituo hivyo ni kuhakikisha Mtwara inapata umeme wakati wote bila kukatika au kupungua nguvu,” alieleza.
Akizungumzia ujenzi wa barabara katika Mji wa Mangaka, aliwaahidi wananchi serikali itaimarisha barabara za lami katika mji huo na mitaa yake.
Vilevile, alisema serikali itaendelea kujenga barabara zinazounganisha wilaya na makao makuu ya mkoa kwa kiwango cha changarawe na lami zipitike kipindi chote.
Dk. Samia alisema anatambua changamoto ya wanyamapori wanaoharibu mashamba na wakati mwingine kujeruhi wananchi.
“Hasa kwa waliozungukwa na Pori la Akiba Lukwira na Lumesule ambako wanyama hao wamekuwa wakiharibu mazao.
“Tatizo tunalijua, tunakwenda kuhakikisha wanyama hao wanabaki katika maeneo yao na hawafiki katika makazi ya watu,” alisisitiza.
Kwa upande wa wafugaji, alisema serikali itaongeza maeneo yaliyotengwa, kupimwa na kumilikishwa kwa wafugaji kutoka ekari milioni 3.4 hadi kufikia milioni sita.
Alibainisha utekelezaji huo ni hadi kufikia mwaka 2030 lengo kuondoa changamoto ya migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
AHUTUBIA NAKAPANYA
Awali, katika mkutano wake uliofanyika Nakapanya, Dk. Samia alisema anatambua maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika eneo hilo, hata hivyo bado kuna baadhi ya changamoto zinazohitaji kupatiwa ufumbuzi.
“Hapa Nakapanya bado kuna mahitaji mengi, nikiangalia nauona umeme na najua umefika vijiji vyote, hivi sasa tunaunganisha katika vitongoji.
“Lakini kuna suala la afya. Najua tumejenga vituo vya afya, zahanati na ninakumbuka vyema Kijiji cha Namiungo ilikuwa tujenge kituo cha afya, lakini hatukufanikiwa,” alieleza.
Aliwaahidi wananchi kujenga kituo hicho cha afya wananchi wapate huduma kwa karibu.
Vilevile, alisema kuna maboma ya zahanati ambayo ujenzi wake haujakamilika, hivyo serikali itayamalizia.
Kuhusu suala la maji, Dk. Samia alieleza bado baadhi ya maeneo yanakabiliwa na uhaba wa maji pamoja na serikali kujitahidi kufikisha huduma hiyo.
Alisema lengo la serikali kama ilivyoahidi kupitia ilani ya uchaguzi ni kila mwananchi apate maji safi na salama, kazi inayoendelea kutekelezwa nchini.
Akizungumzia kilimo, mgombea urais huyo kupitia CCM alisema serikali inasambaza mbolea za ruzuku na pembejeo za kilimo.
Pia, alisema kazi ya ujenzi wa skimu za umwagiliaji inaendelea ambazo wakulima watazalisha mazao yao mara mbili kwa mwaka.
“Natambua Nakapanya ni wazalishaji wazuri wa mazao ya kilimo. Tupo na nyinyi kwa ruzuku ya pembejeo na mbolea.
“Najua tumeanza kujenga mabwawa ambayo bado hayajakamilika nayo tutakuja kuyakamilisha kwani yapo katika hatua mbalimbali,” alibainisha.
Kwa upande wa wanyama waharibifu, alisema anatambua changamoto hiyo ya wanyamapori wanaovamia mashamba.
“Natambua hapa kuna kituo kimoja tumejenga na kituo cha pili tunakijenga Lukumbile, lakini najua kuna askari katika maeneo matano mengine zote hizo ni jitihada za kuwafukuza wanyama hao wasiharibu mashamba na wasiumize watu
“Jana (juzi) nikiwa Tunduru serikali tumenunua ndege tano zisizokuwa na rubani za kufukuza wanyama. Zinafanyakazi maeneo mbalimbali kama tatizo likizidi zitaletwa ndege nyingine,” aliongeza.
BEI YA MAZAO
Akizungumzia kilimo alisema kuna miaka bei za mazao zinapanda na kipindi kingine zinashuka.
Alisema sasa hivi mbaazi na ufuta zinazalishwa katika kipindi ambacho nchi nyingi duniani zimezalisha zao hilo.
“Kwa maana hiyo bei iliyopo duniani hasa kwa wenzetu India ambao tunawauzia, wamezalisha kwa wingi kipindi hiki kwa hiyo wametushushia bei.
“Hata hivyo tunazungumza nao bei isishuke zaidi ya asilimia 60 ya bei ya mwaka jana, niwatie moyo serikali yenu bado inahangaikia bei ya mazao,” alieleza.
AVUNJA NGOME YA ACT
Katika mkutano huo, Dk. Samia alisambaratisha ngombe ya ACT-Wazalendo baada ya mgombea ubunge jimbo la Nanyumbu kupitia chama hicho, Hamad Hashim, kutangaza rasmi kuhamia CCM.
Hashimu ambaye pia alikuwa Katibu wa ACT Wilaya ya Nanyumbu, alisema uamuzi wake umetokana na kuvutiwa uongozi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya Rais Dk. Samia.
Alisema uamuzi huo ni wa hiari na hakuna mtu yeyote aliyemshawishi kukihama chama hicho.
“Ndugu zangu, mimi sijalazimishwa na mtu yeyote. Nimevutiwa na mwenendo na mwonekano wa CCM. Nimeangalia mikutano yake, nimeona viongozi wengi wanapita, lakini Mama Samia amenipa faraja kubwa.
“Nilidhani miradi aliyoikuta ingemshinda, lakini ameendeleza. Huyu ni mama wa pekee,” alisema.
Hashim ambaye pia aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF wilayani Nanyumbu, alisema amekuwa akifuatilia kwa karibu namna Serikali ya Awamu ya Sita inavyotekeleza miradi ya maendeleo.
Alibainisha alipoona namna Rais Dk. Samia alivyoendeleza miradi mikubwa ya kitaifa ikiwemo barabara, afya, elimu na nishati vijijini, alimfanya kutafakari upya kisha kuamua kubadili uamuzi wake.
“Nilifikiri miradi mikubwa ya kitaifa ingeishia alipoachia mtangulizi wake, lakini Mama Samia ameibeba na kuendelea nayo kwa kasi ya ajabu, ndiyo maana nimeamua kwa moyo wa dhati kujiunga CCM na kuunga mkono jitihada hizi,” alibainisha.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara, Said Nyengedi alimhakikishia mgombea Urais kupitia CCM ushindi wa kishindo Oktoba 29, mwaka huu.
“Kwa mapenzi uliyowafanyia wana Mtwara ndiyo maana wamejitokeza kwa wingi na Oktoba 29 wanaenda kutiki katika karatasi ya kura kumchagua mgombea Urais Dk. Samia, wagombea ubunge na madiwani,” alisema.