• ePaper
Wednesday, October 15, 2025
Subscribe
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
No Result
View All Result
Home Habari

DK. SAMIA AFICHUA FAIDA MAPINDUZI YA VIWANDA

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
September 28, 2025
in Habari, Kitaifa, Siasa, Uchaguzi
0
DK. SAMIA AFICHUA FAIDA MAPINDUZI YA VIWANDA

MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan

0
SHARES
1
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na MUSSA YUSUPH,

Kibaha

MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema mapinduzi ya viwanda yaliyofanyika katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, yameliwezesha taifa kujitegemea kwa mapato na bidhaa za viwandani.

Amesema endapo akipewa ridhaa ya kuongoza taifa katika kipindi kingine, serikali yake itajikita kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati itakayofungua zaidi fursa za kiuchumi.

Baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Bandari ya Bagamoyo hadi Bandari Kavu ya Kwala na eneo maalumu la kiuchumi ambalo vitajengwa viwanda vya kimkakati.

Dk. Samia ameyasema hayo alipohutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika uwanja wa Sabasaba mjini Kibaha mkoani Pwani.

Amesema mwaka huu alizindua bandari kavu ya Kwala na kuweka historia ya uzinduzi wa safari za treni ya mizigo kwa njia ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.

Amesema lengo ni kuona sehemu kubwa ya mizigo inayopita Bandari ya Dar es Salaam inapelekwa moja kwa moja Kwala, kisha magari ya mizigo yatashusha na kupakia eneo hilo.

BANDARI YA BAGAMOYO

“Mradi mwingine wa kihistoria ni Bandari ya Bagamoyo, ambayo inasubiriwa kwa muda mrefu lakini mkitupa ridhaa tutakwenda kuijenga Bandari ya Bagamoyo eneo la Mbegani.

“Bandari hiyo itajengwa gati za kisasa na ndefu ambazo zitakuwa na uwezo kupokea meli kubwa zaidi kuliko Bandari ya Dar es Salaam,” ameeleza.

Amesema bandari hiyo itaunganishwa kwa SGR kipande cha kilometa 100 kutoka Bandari kavu ya Kwala hadi Bandari ya Bagamoyo.

Ameeleza bandari hiyo itajengwa sanjari na eneo maalumu la kiuchumi lenye hekta 9,800 litakalochochea na kuvutia uwekezaji viwanda.

Dk. Samia amesema serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi huo na andiko la biashara.

“Tunakwenda kutekeleza mradi huu kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Reli Tanzania (TRC) na sekta binafsi hususan ujenzi wa kongani za viwanda.

Ameongeza:”Hii ni miradi ya kimapinduzi kuweza kufanyika ndani ya Mkoa wa Pwani kuwa kitovu cha usafirishaji nchini, kujenga fursa za ajira na biashara kwa wananchi wa Tanzania.”

UJENZI WA VIWANDA

Pia, alisema mkoa huo unastahili pongezi kwa kasi kubwa ya maendeleo ya viwanda ambavyo idadi imeongezeka kutoka 1,587 hadi viwanda 1,631 mwaka huu.

Alisema idadi hiyo sawa na ongezeko la viwanda 244 ndani ya miaka minne au viwanda 61 kila mwaka.

Dk. Samia alisema viwanda vya kati 81 vimejengwa, ambapo hivi sasa vimefikia 161 sawa na viwanda 26 kila mwaka.

“Viwanda hivi vimetoa ajira za moja kwa moja 21,146 na zisizokuwa za moja kwa moja 60,000.”

Alieleza Mkoa wa Pwani kuna uzalishaji mkubwa unaofanya nchi ijitegemee katika bidhaa muhimu zikiwemo za vioo, marumaru, saruji na mabati ya rangi ambavyo vinazalishwa nchini.

NISHATI YA UMEME

Dk. Samia alisema kutokana na kasi kubwa ya ukuaji viwanda, serikali imejenga vituo vya kupoza umeme eneo la Msufini Mkuranga kwa gharama ya sh. bilioni 388.3.

Alieleza kituo kingine kitajengwa Zegereni Kibaha kwa gharama ya sh. bilioni 54.7 na Zinga Bagamoyo kwa sh. bilioni 120.

Alisema umeme huo utakuwa wenye uhakika kuufanya Mkoa wa Pwani kutokumbwa na upungufu wa umeme, hivyo viwanda vitazalisha muda wote.

Dk. Samia alieleza serikali imeongeza vijiji vyenye miundombinu ya umeme kutoka vijiji 282 mwaka 2020 na hivi sasa vijiji vyote 415 vimepata umeme. Alieleza kazi inayoendelea ni kuunganisha katika vitongoji.

Mgombea Urais kupitia CCM, alisema serikali imekamilisha ujenzi wa kituo kipya cha umeme katika mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kisha kuunganisha katika gridi ya taifa.

“Tunajenga njia mpya ya umeme katika kituo cha Chalinze, lakini tunajenga njia mpya ya umeme ya Kv 400 kutoka Chalinze-Kinyerezi hadi Mkuranga. Hivyo niwahakikishie tunakwenda kuwa na umeme wa uhakika tukikamilisha miradi hii ya umeme.

USAMBAZAJI GESI

Dk. Samia alisema endapo CCM ikipewa ridhaa serikali yake imejipanga kujenga mtandao wa gesi kutoka Kinyerezi hadi Chalinze ambao utakuwa na matoleo kuelekea maeneo ya uwekezaji ya TAMCO, Zegereni, Kwala na Bagamoyo.

Alisema kwa sasa mkandarasi mshauri anaendelea kufanya tathmini ya njia ya kupitisha bomba hilo.

Mgombea urais aliongeza ujio wa gesi utazidi kuvutia uwekezaji mkoani Pwani, kwani viwanda vitaendeshwa kwa gharama nafuu zaidi na bidhaa zitakazozalishwa zitapungua bei.

Alisema miongoni mwa ahadi katika ilani ya CCM ni kuchukua hatua kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi nchini kuwezesha wananchi wa kipato cha chini kujenga nyumba bora za kisasa kwa gharama nafuu.

Alisisitiza malengo ya serikali ni kuendeleza ujenzi makazi bora kwa bei nafuu na kuhakikisha majengo yote yanarasimishwa kwa kupimwa, kupangwa na kumilikishwa.

MIRADI YA MAJI

“Katika kukabiliana na changamoto ya maji tulileta sh. bilioni 187.3 katika mkoa huu. Uwekezaji huu umeimarisha hali ya upatikanaji maji safi na salama kutoka asilimia 67 hadi asilimia 89. Tunapokwenda mbele tutakamilisha miradi mingine minne yenye thamani ya sh. bilioni 44,” alisema Dk. Samia.

Alibainisha miradi hiyo itakayohudumia kata 53 za wilaya ya Rufiji, Kibiti Mkuranga na Kisarawe imeanza kutekelezwa.

Pia, alisema mradi wa maji Kwala utakaonufaisha maeneo ya Kwala, Bandari Kavu na maeneo ya viwanda na kueleza mradi wa maji Pangani utatatua changamoto katika kata hiyo na maeneo ya Msufini, Lulanzi na TAMCO.

Mbali na miradi hiyo alisema miradi mingine midogo yenye kuhusisha upanuzi wa mtandao wa maji kutoka Mlandizi, Bokomlegela, Janga, Mtongani na Kawawa itatekelezwa.

Vilevile, alisema serikali itajenga mradi wa maji katika eneo la viwanda wenye gharama ya sh. bilioni 10.9 ambao utanufaisha maeneo ya mkoa huo.

HUDUMA ZA AFYA

Akizungumzia afya, alisema serikali imefanya maboresho makubwa katika Hospitali ya Tumbi ambayo yamehusisha kuanzisha kituo cha kusafisha damu.

“Tumeleta vifaatiba vikiwemo CT Scan, X Ray na Utra Sound vyote vimesogeza huduma muhimu karibu zaidi na wananchi. Vipimo vyote sasa vinapatikana Tumbi.

“Tunafikiria kuweka MRI vipimo vyote vipatikane pale na wananchi wapate huduma bora zaidi,” alisisitiza.

UJENZI WA BARABARA

Kuhusu ujenzi wa barabara, alisema anatambua mahitaji ya miundombinu hiyo kwa sababu ya msongamano wa magari katika barabara ya Morogoro kutokana na wembamba wa barabara hiyo.

Alisema tayari usanifu unaendelea kwa upanuzi wa barabara kutoka Mailimoja hadi Picha ya ndege ili iwe na njia sita za magari na njia mbili za mwendokasi.

Vilevile, alisema serikali itaboresha mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 71, pia uboreshaji barabara kilometa 17 katika mji huo.

Alisema kwa kushirikisha sekta binafsi kupitia ubia na serikali, utatekelezwa ujenzi wa barabara ya haraka kutoka Kibaha-Chalinze-Morogoro itakayojengwa kwa awamu.

Alieleza barabara hiyo inatija kubwa kiuchumi, hivyo kupitia njia ya PPP ili fedha za serikali ziende katika miradi mingine ya huduma za jamii.

“Tutaijenga barabara ya Bagamoyo – Mlandizi – Manelomango yenye urefu wa kilometa 100 kwa awamu ya kwanza tumeshaingia makubaliano na mkandarasi kujenga kilometa 23 kuanzia Mlandizi hadi stesheni ya SGR Ruvu.

“Tumeanza ujenzi pia wa barabara ya TAMCO Kibaha hadi Mapinga Bagamoyo ambayo kilometa zote 23 zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi na mwakani tutakamilisha ujenzi huu,” alisisitiza.

Dk. Samia alisema serikali imeanza ujenzi wa barabara ya Utete – Nyamwage ambayo itazidi kuufungua mkoa huo.

Aliahidi katika miaka mitano ijayo pia serikali itakamilisha barabara ya Dar es Salaam-Kibiti-Mingoyo yenye urefu wa kilometa 487.

Katika jitihada za kuboresha mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara na wawekezaji, alisema serikali itajenga soko la kisasa eneo la Lolindo kwa gharama ya sh. bilioni 18.

“Tutandeleza ujenzi wa stendi Kibaha vijijini lakini tutaangalia uwezekano wa stendi ya kusini,” alisema.

Dk. Samia alisema kazi kubwa imefanyika kuimarisha ushirika, ambapo sasa vyama hivyo vimeimarika vyema.

KATIBU MKUU CCM

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Asharose Migiro, alieleza kuwa chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia ustawi wa wananchi umeonekana.

Alisema Mkoa wa Pwani ni kituo cha biashara na utalii kupitia vivutio mbalimbali ambayo vilikuwa sehemu ya masimulizi kupitia filamu ya Tanzania Royal Tour.

Aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 mwaka huu kumpigia kura Dk. Samia, wabunge na madiwani wa CCM kwani kufanya hivyo ni kupigia kura maendeleo na utu wa Mtanzania.

Mratibu wa Kampeni Kanda ya Pwani ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu, Halima Mwamuya, alisema hadi sasa ushindi mkubwa utapatikana katika mikoa hiyo.

Alieleza wagombea ubunge na udiwani katika kanda hiyo yenye kujumuisha mikoa ya Pwani, Tanga na Morogoro wanakubalika.

Halima alisema alikutana na kundi la wazee ambao nao wamemhakikishia kwamba wanamuunga mkono Dk. Samia katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlawu, alisema wananchi wa mkoa huo wanamshukuru Dk. Samia kwani hakuna sekta yenye kumnufaisha mwanadamu ambayo haijaguswa.

Alisema upatikanaji pembejeo za mazao ya korosho na ufuta zimechangia kuongeza vipato vya wakulima.

Hata hivyo, aliomba barabara ya kwenda mikoa ya kusini eneo la Kokoto Mbagala kwani kipande hicho kimeendelea kuleta changamoto kwa wananchi.

Vilevile, aliomba ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoa ya kusini.

WAGOMBEA UBUNGE

Mgombea ubunge Jimbo la Kibaha Mjini, Sylvester Koka, alisema Dk. Samia ameinua hadhi ya Halmashauri ya Mji Kibaha hadi kuwa manispaa.

Alisema jimbo hilo limepatiwa sh. bilioni 17 ambazo zimetumika kujenga shule za msingi, sekondari, ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu.

Kwa upande wa afya, alisema sh. bilioni 13.9 zimepelekwa katika jimbo hilo zilizotumika katika ujenzi wa vituo vya afya na zahanati.

“Tunakushukuru unakwenda kuajiri watumishi wa afya ambao watakwenda katika zahanati na vituo vya afya, hivyo wananchi watapata huduma bora zaidi,” alieleza.

Pia, alisema jimbo hilo limenufaika kupitia mradi wa TACTIC wenye thamani ya sh. bilioni 18 ambazo zitatumika kujenga soko la kisasa na barabara za lami za mitaa mbalimbali.

Kwa upande wake, mgombea ubunge Kibaha Vijijini, Hamud Jumaa, alieleza CCM kitaibuka na ushindi mkubwa kwa sababu kazi nzuri aliyoifanya Dk. Samia katika miradi ya maendeleo.

Alibainisha katika kipindi cha miaka minne Bandari ya Dar es Salaam inapokea mizigo ya tani zaidi ya milioni 30 kutoka tani milioni 18 kabla ya Dk. Samia kuingia madarakani.

Alieleza katika jimbo hilo wameanza kunufaika kupitia sekta ya elimu ambapo sh. bilioni 1.6 zimetumika kujenga shule tatu na madarasa 61 kwa elimu ya msingi.

Alisema wamepata fedha kupitia mapato ya ndani kutoka sh. milioni 200 hadi kufikia zaidi ya sh. bilioni moja.

Mgombea ubunge viti maalumu Mkoa wa Pwani, Hawa Chakoma, alisema Rais Dk. Samia amehakikisha wanawake wanapatiwa majiko ya gesi kwa lengo la kuondokana na maradhi yanayosababishwa na matumizi ya nishati chafu.

Alisema Dk. Samia ambaye ni mgombea urais kupitia CCM, alipandisha hadhi ya mtoto wa kike katika sekta elimu kwa kuanzisha shule za sayansi kwa wasichana kwenye mikoa yote ya Tanzania Bara.

Naye, mgombea ubunge viti maalumu, Mariam Ibrahimu, alisema wananchi wa mkoa huo hususan wajasiriamali wamenufaika kupitia mikopo ya asilimia 10 bila riba.

Aliongeza mikopo hiyo imewawezesha wanawake, vijana na wenye ulemavu kujiimarisha kiuchumi kupitia miradi ya ujasiriamali.

Previous Post

YANGA, SINGIDA, MLANDEGE MZIGONI TENA KIMATAIFA

Next Post

MGOMBEA URAIS AAHIDI UTEKELEZAJI BARABARA KIBAHA – CHALINZE – MORO

Next Post
MGOMBEA URAIS AAHIDI UTEKELEZAJI BARABARA KIBAHA – CHALINZE – MORO

MGOMBEA URAIS AAHIDI UTEKELEZAJI BARABARA KIBAHA – CHALINZE - MORO

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

MOROGORO YA DK. SAMIA

MOROGORO YA DK. SAMIA

2 months ago
NCHIMBI : NIDHAMU NGUZO KUIMARISHA DEMOKRASIA

NCHIMBI : NIDHAMU NGUZO KUIMARISHA DEMOKRASIA

4 weeks ago

Popular News

  • SIMBA NI MWENDO WA MABAO LIGI KUU

    SIMBA NI MWENDO WA MABAO LIGI KUU

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • JESCA: DK. SAMIA NI KIONGOZI JASIRI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • MAFANIKIO YA WATANZANIA YAKO KATIKA MATENDO – DK. MIGIRO

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • DK. SAMIA AAHIDI UCHUMI JUMUISHI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • DK. MWINYI AAHIDI KUJENGA HOSPITALI MAALUMU YA SARATANI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
error: Content is protected !!
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2025 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.