NA HANIFA RAMADHANI,
Zanzibar
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk.Hussein Ali Mwinyi ameahidi kujenga barabara za ndani kwa kiwango cha lami katika Jimbo la Pangawe ikiwa atapata ridhaa ya kuwaongoza tena Wazanzibar kwa awamu ijayo.
Dk.mwinyi aliyasema hayo akizungumza na wananchi wa Jimbo la Pangawe ikiwa ni mwendelezo wa kampeni zake za Urais kisiwani Unguja.
Amesema, huyo alisema anatambua changamoto zilizopo katika jimbo hilo la majimbo jirani ikiwemo mahitaji ya ujenzi wa barabara za ndani ikiwemo kinuni skuli hadi Kwarara na Fuoni Mambosasa hadi Taveta magari ya mchanga na kuwaahidi nazo zitajengwa kwa kiwango cha lami.
“Hapa najua kunahitajika barabara ya kinuni skuli hadi kwarara, natambua kunahitajika barabara ya kutoa Fuoni mambosasa hadi Taveta magari ya mchanga, ndugu zangu ahadi yetu ni kwamba barabara hizo tutazijenga kwa kiwango cha lami,” amesema.
Kwa upande wa sekta ya elimu Dk. Mwinyi alisema anatambua kuna mahitaji ya skuli ya msingi Tomondo Uzi, Kinuni na mahitaji ya skuli ya maandalizi Kijitoupele mashine ya maji na kuahidi kuwa skuli hizo zitajengwa tena za kisasa.
Amesema, serikali imeingia mkataba wa ujenzi wa skuli mpya za kisasa za ghorofa 29 hivyo ataangalia maombi hayo ili kufanya mgao ili nao waweze kupatiwa skuli za kisasa.
Sambamba na hayo Dk. Mwinyi, aliwataka wananchi wa Zanzibar kuwa makini na kutokubali kudanganywa na wanasiasa wa vyama vya upinzani, akisisitiza kuwa hawana uwezo wala sera madhubuti za kuwatumikia wananchi.
Amesema tangu kuanza kwa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu, vyama vya upinzani vimeshindwa kuwasilisha sera zinazogusa maisha ya kila
siku ya wananchi, hususan katika sekta muhimu kama afya, elimu, maji, umeme, barabara, na huduma nyingine za kijamii.
“Wananchi msikubali kuhadaiwa, wanasiasa wa upinzani wanazunguka lakini hawana sera za maana kwani hawajaeleza watakavyowasaidia wananchi katika sekta muhimu, hakuna hata sera moja ambayo inawagusa wananchi hawa sio watu wa kuchaguliwa hawana uwezo wa kuongoza hawa kuweni makini,” alisema Dk. Mwinyi.
“Mikutano mingi ya CCM kuna mafuriko ya watu hawa tukiwashinda watasema tumewaonea kweli wakubali ukweli hawana watu, wote wapo CCM, wakati mwengine bora mkubali yaishe maana mtasingizia mmeonewa umati huu uliopo hapa hamuoni dalili ya kushindwa,” amebainisha.
Amesema wananchi wa Zanzibar ni mashahidi na wanaona jinsi ya serikali ya awamu ya nane inayotokana na CCM ilivyofanya mambo makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa skuli za kisasa, ujenzi wa hospitali za wilaya na mikoa, ujenzi wa barabara kuu na za ndani na viwanja vya michezo, masoko ya kisasa na miradi mengine mikubwa ya kimaendeleo ikiwemo ya umeme.
“Chama cha Mapinduzi kimefanya maendeleo makubwa na miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo inaonekana hivyo naomba mridhie kuwa kipimo chetu cha kutuchagua tena kwa miaka mitano ijayo mpaka 2030 ili tuendelee kuwatumikieni,” amewaomba.
Sambamba na hayo katika kuwawezesha wananchi kiuchumi alisema sera mama katika awamu ijayo ni kutengeneza ajira ikiwemo kuajiri serikalini, sekta binafsi na kuwawezesha vijana kujiajiri wenyewe kwa kuwapa mikopo isiyokuwa na riba ili waweze kujikwamua na umasikini.
Dk. Mwinyi ameawaahidi vijana kuwa serikali Itaangalia uwezekano wa kujenga viwanja vya kisasa hivyo kwenye majimbo ili kuwawezesha vijana kupata maeneo mazuri ya kufanya michezo.
Amesema iwapo atapewa ridhaa ya kuongoza tena, ataendeleza jitihada hizo kwa kasi zaidi, akijikita katika kuimarisha huduma za kijamii na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Aidha, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kuhakikisha wanachagua viongozi wa CCM ili kulinda mafanikio yaliyopatikana na kuendeleza maendeleo endelevu ya taifa.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Mohammed Said Mohammed, alisema wakimpa ridhaa kwa miaka mitano ijayo Dk. Mwinyi na viongozi wengine wanaotokana na chama cha Mapinduzi basi wananchi wa Zanzizibar na Tanzania wataendelea kufaidi maendeleo makubwa zaidi kupitia kauli ya mgombea kwamba yajayo ni neema zaidi.
“Mkichagua CCM ndio mmechagua amani ya nchi hii na mkimchagua Dk. Mwinyi, Dk. Samia, wabunge, wawakilishi na madiwani basi mmechagua maendeleo ya kweli,” alisema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Hassan Khamis Hafidh, aliwaomba wananchi kuendelea kuiunga mkono CCM kwani ndio chama pekee kinachoendeleza amani, umoja na maridhiano ya wanzanzibari na kuleta maendeleo ya kweli.
Alisema Dk.Mwinyi amefanya maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya afya ambapo wananchi wanapata huduma bora bila ya malipo katika hospitali zake zote Unguja na Pemba na kujenga vituo vya afya vyenye vifaa tiba, dawa na kupewa milo mitatu inayoendana na wakati.
Alibainisha kuwa maendekeo ni mbadiliko mema ambayo Dk. Mwinyi ameibadilisha Zanzibar kwa miradi mbalimbali ya kimaendeleo
ikiwemo miundombinu ya barabara, maji, elimu, afya na huduma nyengine za kijamii.
Mohammed Chomo ni kada wa CCM, alisema Dk. Mwinyi amesimamia mapinduzi ya kweli ya mwaka 1964 kwa wananchi wa Zanzibar ambayo aliyaleta Mzee Abeid Amani Karume kwani ana dhamira na maono ya dhati ya kuitoa nchi hapa ilipo.
Hivyo, aliwaomba wananchi kutofanya makosa Oktoba 29 na badala yake kumninia nyingi za ndio na viongozi wengine wa CCM ili kwa pamoja waendelee kuleta mwendeleo.