Na NJUMAI NGOTA,
Mtwara
MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, iwapo watapata ridhaa ya kuongoza nchi, wamedhamiria kujenga meli mpya ya mizigo itakayorahisisha usafirishaji bidhaa kutoka Mtwara kwenda Comoro.
Dk. Nchimbi, amesema hayo kwa nyakati tofauti, alipohutubia wananchi katika mikutano ya hadhara ya kampeni za Chama kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu, majimbo ya Mtwara Vijijini na Nanyamba, mkoani Mtwara.
Amesema lengo la kujenga meli hiyo ni kuinua uchumi wa wakulima na wafanyabiashara, kuhakikisha bidhaa zao zinapata masoko ya kimataifa kwa gharama nafuu na faida kubwa.
“Hakuna sababu ya wakulima wa Mtwara kukosa soko la bidhaa wakati tupo karibu na Comoro.
“Meli hii ya mizigo, itavusha bidhaa kwa urahisi na tutakuwa na uhakika wa bei nzuri kwa wakulima wetu. Huu ndiyo uchumi wa bahari tunaotaka kuuimarisha,” alisema.
Amesema katika miaka mitano ijayo, CCM imedhamiria kuanzisha mradi mkubwa wa kuchukua maji kutoka Mto Ruvuma na kuyasambaza maeneo ya Mtwara Vijijini, Nanyamba na Tandahimba.
“Mto Ruvuma ni mkubwa, bado wananchi wetu wanapata tabu ya maji. Hatutakubali hali hii iendelee. Tunatekeleza miradi mikubwa ya maji, kila mtu apate huduma hii muhimu bila shida,” amesema.
Akizungumzia sekta ya nishati, Dk. Nchimbi amesema serikali ijayo ya CCM, ina mpango wa kusimamia ujenzi wa bomba la gesi la kilometa 34 kutoka Ntorya hadi Madimba, kuhakikisha wananchi wanapata gesi ya uhakika kwa matumizi ya nyumbani na kibiashara.
MTWARA VIJIJINI
Akiwa Nanguruwe, Dk. Nchimbi, alisema katika kuhakikisha maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga, Serikali ya CCM, imedhamiria kupanua Kiwanja cha Ndege cha Mtwara kwa kuongeza majengo ya abiria, mnara wa kuongozea taa na eneo la Zimamoto.
“Ilimradi hadhi ya uwanja wa ndege ionekane na kuongeza usafirishaji wa watu na bidhaa zetu,”alisema.
AFYA
Alisema CCM katika Jimbo la Mtwara Vijijini, wamekusudia kujenga vituo vya afya vitano na zahanati 12, kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya karibu na makazi yao.
ELIMU
Pia, alisema CCM imedhamiria kuinua kiwango cha elimu kwa kujenga sekondari nne na shule za msingi tano ndani ya jimbo hilo.
Alisema hatua hiyo, inalenga kuhakikisha watoto wanapata elimu bora katika mazingira rafiki, yanayowezesha kujifunza kwa ufanisi.
BARABARA
Akielezea mpango wa CCM katika miundombinu, Dk. Nchimbi alisema barabara kadhaa muhimu zitatengenezwa kwa kiwango cha lami na kukarabatiwa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu.
Alizitaja baadhi ya barabara hizo na kilometa zikiwa katika mabano ni Nanguruwe – Masasi (160), Mtwara – Mingoyo (201), Madimba – Msimbati (35) na Mbuyuni – Newala (42).
NANYAMBA
Akiwa Nanyamba, Dk. Nchimbi, alisema wamekusudia kujenga shule mbili za msingi, sekondari tatu na kuongeza madarasa katika shule zilizopo, kwa lengo la kuhakikisha watoto wote wanapata fursa ya kusoma katika mazingira bora na ya kisasa.
Pia, alisema CCM imedhamiria kujenga barabara mbalimbali kwa kiwango cha lami na changarawe, zikiwemo za Nanyamba – Mkodolo na Mahakama Road – Nanguruwe – Mkulwa yenye urefu wa kilometa 1.8.
TANDAHIMBA
Akiwa katika mkutano wa hadhara wa kampeni Viwanja vya Kassim Majaliwa, alisema wamekusudia kujenga vituo vya afya viwili na zahanati 12, huku Hospitali ya Wilaya ya Tandahimba, ikiendelea kuboreshwa kwa kuongeza vifaatiba na miundombinu ya kisasa.
Kuhusu elimu, alisema CCM itajenga shule za msingi nne na sekondari mbili huku shule za zamani zikijengwa madarasa mapya 185.
Alisema katika miaka mitano ijayo, wanakusudia kujenga maabara 10 kwa masomo ya sayansi.
Aidha, wanakusudia kujenga baadhi ya barabara kwa kiwango cha lami na changarawe ikiwemo ya Mtama – Newala (74), hatua itakayorahisisha usafiri wa mazao, watu na bidhaa katika maeneo ya Tandahimba na maeneo jirani.
Kuhusu sekta ya biashara, Dk. Nchimbi alisema imepewa kipaumbele kwa kujengwa stendi ya kisasa, soko la kisasa huku wakiendelea kushirikiana na Bodi ya Korosho kwa kuhakikisha bei ya zao hilo inaendelea kuwa nzuri.
Dk. Nchimbi akiwa katika mikutano hiyo, alimwombea kura Mgombea Urais wa Chama, Dk. Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani wote wa CCM.