Na NJUMAI NGOTA,
Lindi
MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema Chama kitaendelea kumuenzi Hayati Rashid Kawawa, aliyekuwa miongoni mwa wazee waliolipenda taifa kwa dhati na kulitumikia kwa nguvu zote, uaminifu na moyo wa kizalendo.
Dk. Nchimbi amesema hayo katika Uwanja wa Ujenzi, Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, mkoani Lindi, jana, alipohutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara wa kampeni za Chama, kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Amesema taifa halitamsahau mwasisi huyo wa Chama, kutokana na mchango wake katika kulijenga taifa la Tanzania, utaendelea kuenziwa.
“Nataka niwaambie bila kigugumizi katika viongozi waliopata kutokea katika taifa hili ambao taifa hili halitawasahau maisha yake yote ni pamoja na Rashid Kawawa,”amesema.
Pia, ametumia fursa hiyo, kumwelezea Hayati Kawawa kama mfano bora wa kuigwa kwa kizazi cha hivi sasa na kijacho, huku akibainisha kuwa binafsi alinufaika kwa kuwa karibu naye alipokuwa kiongozi wa vijana wa CCM.
“Nilipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Vijana wa Umoja wa CCM (UVCCM) mara ya kwanza kabisa, kikao cha kwanza na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliniambia kama unataka kujifunza uzalendo katika nchi hii, kaa karibu na mzee Kawawa.
“Wakati huo, Mzee Kawawa alikuwa Kamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM, mimi katika kipindi chote nilichokuwa Mwenyekiti wa UVCCM, hakuna mwezi uliopita bila kwenda kuongea naye, kujifunza utumishi na uzalendo kwa nchi yetu,”amesema.
Amesema mazungumzo yake ya mwisho na Hayati Kawawa, yalikuwa Desemba, mwaka 2009, siku chache kabla ya kifo chake na alikuwa mkazi wa Liwale.
Amesema alikwenda hospitalini kumsalimia, alipoondoka, aliitwa tena kurudi kwa kuwa, Mzee huyo alikuwa na ujumbe wa mwisho wa kumwambia.
“Nilimsalimia nikatoka, nikiwa nje nikaambiwa Mzee ana jambo, anataka kukwambia. Nilirudi ndani, akaita watoto wake wawili – Vita na Zainab Kawawa, mimi na mlinzi wake mmoja. Akaniambia mimi sitatoka hapa, sitarajii kupona safari hii.
“Hakikisheni Chama chetu kinaendelea kuwa Chama cha watu, cha kuwatetea Watanzania wenye shida, cha wanyonge na kimbilio la wanyonge,” amesema.
Dk. Nchimbi, amesema alimwahidi Mzee Kawawa kuwa, maelekezo yake yatahifadhiwa moyoni na kutekelezwa kwa vitendo. “Nikamwambia Mzee tumekusikia na wiki ile haikuisha akafariki dunia. Nasema naendelea kuyaenzi maneno yake, tunaendelea kumuenzi kama Chama kwa sababu wazee waliopata kulipenda taifa letu na kulitumia kwa nguvu zao Mzee Kawawa ni mmoja wao,”alisema.
Amesema wiki hiyo, Mzee Kawawa alifariki dunia na taifa likapoteza mmoja wa waasisi wake muhimu.
Dk. Nchimbi, amesema anaendelea kuenzi maneno yake na zaidi ya hapo, watamuenzi kama Chama kwa sababu, katika wazee waliolipenda taifa na kulitumikia kwa nguvu zao zote, Mzee Kawawa ni miongoni mwao.
Amewapongeza wananchi wa Liwale kwa moyo wao wa kuendelea kumkumbuka Hayati Kawawa, hata baada ya kupita zaidi ya miaka 15 tangu alipofariki dunia na ni ushahidi wa namna alivyogusa maisha ya watu.
Akizungumzia miaka minne iliyopita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa wananchi kupitia sekta ya kilimo, mifugo, afya, elimu, maji na miundombinu.
Amesema Wilaya ya Liwale ikitajwa kunufaika moja kwa moja na mikakati hiyo ya kimaendeleo.
Dk. Nchimbi, amesema Dk. Samia, ameonesha uwezo mkubwa wa kiuongozi na maono ya mbali, hasa katika kuinua sekta ya kilimo ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa na maisha ya wananchi wengi wa vijijini.
“Katika miaka hii minne, uzalishaji wa korosho umeongezeka kutoka tani 30,000 hadi kufikia tani 90,000.
.
MIFUGO
Alisema bei za chanjo na dawa, zilipunguzwa kwa lengo la kuwawezesha wafugaji kufuga kitaalamu.
Kwa mujibu wa Dk. Nchimbi, bajeti ya sekta hiyo, imeongezeka kutoka sh. bilioni 66 hadi kufikia sh. bilioni 104, ukiwa ni uthibitisho wa dhamira ya serikali ya kuwajali wafugaji wa Tanzania.
“Mama Samia hakupuuza wafugaji. Serikali imehakikisha kuwa, dawa na chanjo, zinapatikana kwa bei nafuu, hivyo kuwawezesha kufuga kwa tija zaidi,”alisema.
Akizungumzia mipango ya miaka mitano ijayo, Dk. Nchimbi alisema serikali ya CCM iwapo itapewa ridhaa ya kuongoza nchi, imepanga kuibadilisha taswira ya kilimo wilayani Liwale kwa kujenga skimu tano za umwagiliaji na kukarabati zilizopo wananchi wasitegemee kilimo cha mvua pekee.
“Tutahakikisha wakulima wanapata ruzuku ya mbolea, dawa na huduma nyingine muhimu. Serikali pia itajenga majosho mapya matatu, machinjio ya kisasa na malambo ya kunyweshea mifugo ili kuchochea uchumi wa vijijini,” alisema.
Katika sekta ya afya, alisema wamedhamiria kujenga vituo vya afya viwili, zahanati tatu na nyumba za watumishi wa idara ya afya, hatua ambayo inalenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Liwale.
ELIMU
Alisema serikali itajenga shule mbili za msingi, shule moja ya sekondari na kuongeza madarasa 250 katika shule zilizopo na kujenga nyumba 25 za walimu kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Kuhusu huduma ya maji, Dk. Nchimbi alisema miradi yote ya maji iliyopo itaboreshwa kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Liwale.
Pia, alisema serikali ijayo ya CCM, imekusudia kujenga barabara za mjini Liwale kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa tatu, Nangurukuru–Liwale kilometa 230 kwa kiwango cha changarawe, uwekaji wa taa za barabarani na ujenzi wa barabara nyingine za mitaani.
“Liwale lazima ipate hadhi ya kuwa kitovu cha maendeleo kwa Mkoa wa Lindi. Hizi barabara zitafungua fursa nyingi zaidi, zitavutia wawekezaji na kuongeza thamani ya maisha ya wananchi,” alisema.
Aliwaomba wananchi wa Liwale kuendelea kuiamini CCM kwa sababu ni Chama pekee kilichoonesha uwezo wa kupanga na kutekeleza kwa vitendo miradi ya maendeleo.
Katika mkutano huo, Dk. Nchimbi alimwaombea kura Dk. Samia ambaye ni Mgombea Urais wa CCM, wabunge na madiwani huku akiwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, mwaka huu kwa kukipatia ushindi wa kishindo Chama