Na MUSSA YUSUPH,
Dodoma
TANGU kuanza kampeni za Uchaguzi Mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu, Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuvutia maelfu ya Watanzania ambapo zaidi ya wananchi milioni 14.62, wamejitokeza katika mikutano yake 77 iliyofanyika mikoa 21.
Pia, watu zaidi ya milioni 31.6, wamefuatilia mikutano hiyo ya kampeni iliyofanyika katika kanda za Kati, Magharibi, Pwani, Kusini, Nyanda za Juu Kusini, Pemba, Unguja na Kanda ya Kaskazini.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa kampeni hizo jijini Dodoma, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, amesema mahudhurio hayo makubwa, yameonesha namna Dk. Samia, anavyokubalika na wananchi.
“Imani ya wananchi kwa Dk. Samia Suluhu Hassan, siyo bahati wala mkumbo, bali imechagizwa na uongozi wenye mafanikio makubwa katika miaka minne aliyoshika usukani wa Urais,” amesisitiza.
Kihongosi, amesema Dk. Samia, aliupokea mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JINHPP) ukiwa asilimia 37 ambapo hadi sasa mradi huo umeanza kuzalisha umeme.
Vilevile, amesema Dk. Samia, amefanya vema katika miradi ya miundombinu, kuanzia Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam mpaka Makutupora (kilometa 722) yaliyoleta mapinduzi makubwa ya usafiri wa treni kati ya Dar es Salaam na Dodoma.
“Ndani ya miaka minne ya uongozi wake, Dk. Samia amejenga kilometa 15,366.36 za barabara. Chini ya uongozi wa Dk. Samia, ndege mpya sita za abiria na moja ya mizigo zimenunuliwa, hivyo kufanya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuwa na ndege 16.
Ameongeza: “Wananchi hasa wa vijijini, wamekuwa mashuhuda wa kazi kubwa ya Rais Samia, miradi 1,633 ya usambazaji wa maji imekamilika, miongoni mwa hiyo miradi 1,335 ni ya vijijini peke yake.”
Kwa upande wa sekta ya afya, alisema ndani ya miaka minne ya Dk. Samia, vituo vipya vya afya 1,368 vimejengwa.
Amesema hospitali zinazotoa huduma za dharura (EMD) zilikuwa saba nchi nzima wakati Dk Samia anashika madaraka, lakini sasa zipo 116 huku vituo 183 vyenye uwezo wa kutoa huduma za uzazi ikiwemo upasuaji, vimejengwa.
“Sekta ya elimu, shule za msingi zimeongezeka hadi kufikia 19,783, kutoka 16,656, wakati Dk. Samia anaingia madarakani. Shule za sekondari zimefikia 5,926 kutoka 5,001, bajeti ya mikopo ya elimu ya juu imeongezeka kutoka sh. bilioni 464 mpaka sh. bilioni 786.
“Uchumi wa nchi umekua kwa kasi, kutoka asilimia 3.9, Dk. Samia aliposhika madaraka hadi asilimia 5.5 mwaka 2024. Matarajlo ni kufikia asilimia sita mwaka huu. Ajira milioni nane zilitengenezwa ndani ya miaka minne ya Dk. Samia,” amesisitiza.
KUANZA KAMPENI MWANZA
Katika hatua nyingine, Kihongosi alisema Dk. Samia ataanza ziara yake ya kampeni kesho Kanda ya Ziwa yenye mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita, Mara na Kagera.
Alisema katika mikoa hiyo, maendeleo mengi yamefikiwa ikiwemo kukamilika Daraja la Kigongo – Busisi (Daraja la Magufuli), kukamilika ujenzi wa chanzo cha maji cha Butimba kinachowanufaisha wananchi 450,000 mkoani Mwanza.
Pia, alisema serikali imefanikiwa kutekeleza mradi wa maji ya Ziwa Victoria unaowahudumia wananchi 86,980 wa Tinde na Shelui.
“Ujenzi wa vivuko sita Ziwa Victoria vimekamilika na kuanza kazi. Boti ya kuhudumia majeruhi wa ajali Ziwa Victoria. Chanjo ya mifugo imezinduliwa ambapo sh. bilioni 62 imetolewa,” alisisitiza.