Na NJUMAI NGOTA,
Tabora
MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameandika historia mpya ya uongozi kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo na huduma kwa wananchi kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.
Dk. Nchimbi, aliyasema hayo katika Uwanja wa Mpira wa Kigwa, wilayani Igalula, mkoani Tabora, alipohutubia mamia ya wananchi, waliojitokeza katika mkutano wa hadhara wa kampeni za CCM, kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
“Katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wake, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amefanya kazi nyingi katika miradi ya maendeleo na huduma kwa kiwango ambacho hakijapata kutokea katika nchi yetu,” alisema.
Alisema mafanikio hayo makubwa, yameleta faraja na fahari kwa kila Mtanzania, hasa wanachama wa CCM ambao, hivi sasa wanatembea kifua mbele kwa sababu ya kazi nzuri ya Rais Dk. Samia.
“Ndiyo maana leo, tunakwenda kifua mbele tukijivunia kazi alizofanya Rais wetu.
“Kila kiongozi aliyesimama hapa, ameieleza kwa fahari kazi iliyofanyika.
“Kila kiongozi wa CCM na kila mwanachama wetu, anakwenda popote kwa kujiamini,”alisema.
Dk. Nchimbi, alibainisha kuwa, hivi sasa CCM ina wanachama milioni 13.5, wote wakiwa na imani kubwa na uongozi wa Dk. Samia, ambaye amejenga heshima ya serikali na Chama.
Aliwahimiza wananchi wa Igalula, kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura Oktoba 29, mwaka huu na kuhakikisha wanamchagua Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, wagombea wa ubunge na udiwani.
Mgombea Mwenza wa Urais, Dk. Nchimbi juzi alihitimisha mikutano yake ya hadhara ya kampeni mkoani Tabora.
KUTIKISA ZANZIBAR
Dk. Nchimbi, leo anatarajiwa kufanya mikutano ya hadhara ya kampeni za Chama eneo la Kinyasini- Wete, Kaskazini Pemba kisha kwenda kuzuru kaburi la Hayati Mohamed Seif Khatib.
Pia, mkutano mwingine, unatarajiwa kufanyika katika Jimbo la Chwaka lililopo Kusini Unguja.