Na MUSSA YUSUPH,
Mwanza
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, ameanika mkakati wa kulifanya Jiji la Mwanza kuwa lenye hadhi ya kimataifa.
Mkakati huo, umejikita katika utekelezaji miundombinu ya barabara, uboreshaji mtandao wa maji, ujenzi uwanja wa ndege wenye hadhi kimataifa na utekelezaji mradi wa reli ya kisasa (SGR).
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Buhongwa wilayani Nyamagana mkoani Mwanza, Dk. Samia, alitoa wito kwa wananchi kukipa ridhaa CCM kuongoza tena katika miaka mitano ijayo ili wananchi washuhudie neema hiyo.
“Ahadi ya CCM ni kuendelea kuiboresha Mwanza kuifanya kuwa jiji kweli kweli. Huu ni mkoa muhimu kwa biashara na shughuli za uzalishaji, kilimo na uvuvi,” alisisitiza huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi.
Dk. Samia, alisema kazi ya CCM na serikali yake ni kuendeleza na kukuza nguzo kuu za kiuchumi katika mkoa huo, ambazo ni maendeleo ya jamii, maji, nishati na usalama wa wananchi.
SEKTA YA MAJI
Akizungumzia sekta ya maji, alieleza kuwa, serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo muhimu kwa wananchi.
“Nakumbuka ziara yangu ya kwanza nikiwa Rais pale Butimba, nilipokelewa na ndoo za kinamama wakaniambia sisi hatuna maji. Nikawaahidi nitajitahidi nilete maji.
“Nataka niseme kijana wenu ( Waziri wa Maji Jumaa Aweso) yupo hapa. Nilikuwa nikimkaba na kazi nzuri ameifanya. Tumetekeleza mradi mkubwa wa Butimba wa sh. bilioni 71.7,” alieleza.
Alisema mradi huo, umewezesha kuwafikishia maji safi na salama wakazi 450,000 wa Buhongwa, Nyegezi, Igoma na maeneo ya pembezoni mwa jiji hilo.
Kadhalika, alisema serikali imetekeleza mradi mwingine wa maji wenye thamani ya sh. milioni 864 uliyonufaisha wakazi wa jiji hilo.
Alibainisha kuwa, miradi mingine ya maji inayotekelezwa kwa sh. bilioni 46, ipo katika maeneo ya Buhongwa, Kishiri na maeneo mbalimbali ya mkoa huo yakiwa yamefikia asilimia 85.
Dk. Samia, alitoa ahadi ya kuikamilisha miradi hiyo, ukiwemo wa upanuzi chanzo cha maji Kapripoint ili kuimarisha zaidi upatikanaji maji.
Kuhusu changamoto ya kukatika maji, alisema serikali ilimtuma Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, kushughulikia changamoto hiyo, kazi ambayo imefanyika kwa ufanisi.
“Kuna tatizo la presha ya maji kuwa ndogo, baadhi ya maeneo hasa yale ya miinuko.
“Serikali tunajenga matanki makubwa maeneo ya Nyamazobe lita milioni tano, Buhongwa lita milioni 10 na Fumagila ya juu tanki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 10.
Alisisitiza: “Ujenzi wa matanki hayo umefikia asilimia 35 hivyo kazi hiyo tutaimaliza na baada ya kuimaliza mtiririko wa maji utakuwa mzuri, yatapatikana saa 24.”
UJENZI WA MIUNDOMBINU
Suala lingine aliloligusia ni ujenzi miundombinu ya barabara ya Buhongwa Igoma (kilometa 14) kwa thamani ya sh. bilioni 22.7.
Alisema ujenzi huo umekwenda sambamba na ujenzi wa madaraja ya Mbuyuni na Mabatini kwa sh. bilioni 11.2 ujenzi ambao unaendelea.
Ili kuhakikisha ubora wa barabara, alieleza kuwa serikali itaongeza bajeti ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) waendelee na ujenzi wa barabara za ndani.
Pia, alisema kuhusu Kiwanja cha Ndege Mwanza, serikali itakikamilisha kuwa chenye hadhi ya kimataifa.
Kwa upande wa Nyamagana, alisema serikali imejenga miundombinu ya kituo cha mabasi Nyegezi na soko kuu la mjini kati.
“Ni miundombinu ya kisasa inayotoa ajira na kuongeza mapato kwa halmashauri. Lakini SGR inaendelea. Hiyo ndiyo CCM.
Aliongeza: “Kuna ujenzi wa masoko yaliyopangwa kujengwa na kuboreshwa likiwemo soko la mchafukuoga, soko la samaki Mkuyuni, Nyegezi na soko la mazao Igoma.”
Alisema masoko mengine ni Mabatini, Buhongwa, Bukarika, Tambukareli na Butimba, ambayo yatajengwa kwa kushirikiana na halmashauri.
UPATIKANAJI HUDUMA ZA AFYA
Alisema katika miaka mitano iliyopita, serikali wilayani Nyamagana imeboresha hospitali ya wilaya, vituo vinne vya afya, shule sita za sekondari na nane za msingi.
Pia, alieleza kuwa, serikali imejenga mabweni mawili na uzio kwa ajili ya watoto wenye uhitaji maalum katika Shule ya Msingi Buhongwa.
MSISITIZO WA AMANI
Kwa upande wake, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, alitoa wito kwa vijana kuendelea kutunza amani na utulivu nchini.
“Vijana tulinde amani, asije akasimama yeyote kwenda kufanya fujo, watu wenye kupenda kwao hawaanzishi vurugu nyumbani. Kazi hii ya kutunza amani ni yenu vijana,” alisisitiza.
Kihongosi alisema miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa barabara na kukamilika daraja la Kigongo Busisi ni kazi kubwa iliyofanywa na CCM kuwaletea wananchi maendeleo.
Alieleza kuwa, katika sekta ya maji, serikali imetekeleza miradi ya maji kutoka Ziwa Victoria, mbali ya kunufaisha mkoa huo, pia Simiyu, Shinyanga na Tabora imeendelea kupata huduma ya maji.
USHINDI WA KISHINDO
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Lushinge, alieleza kuwa, tangu kampeni za uchaguzi mkuu zilipozinduliwa, mkoa huo uko tayari kuthibitisha mapenzi yao kwa Dk. Samia.
“Wananchi wa Mwanza shauku yao kubwa ni kukuona kwa sababu miradi mingi wameiona, kwani zaidi ya sh. trilioni tano, zimeletwa kutekeleza,” alieleleza.
MGOMBEA JIMBO LA NYAMAGANA
Mgombea Ubunge Jimbo la Nyamagana, John Nzelanyingi, alisema Dk. Samia katika kipindi cha miaka mitano amefanya mambo mengi makubwa katika jimbo hilo.
Alieleza kuwa, katika Kata ya Buhongwa Dk. Samia ametimiza ahadi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Buhongwa hadi Igoma kwa kiwango cha lami.
“Dk. Samia ujenzi wa barabara hiyo imefikia asilimia 95 na inapitika, umejenga barabara yenye urefu wa kilometa moja kutoka Buhongwa kuunganisha Misungwi,” alieleza.
WENYE NIA OVU
Dk. Samia, aliwataka Watanzania kuwaepuka watu wenye nia ovu ya kuichafua taswira Tanzania kimataifa.
Alisema wapo baaadhi ya watu, pindi wanaposhuhudia Tanzania ikiheshimika kimataifa, kazi yao ni kutaka kushusha heshima hiyo.
Dk. Samia alitoa wito huo, alipohutubia maelfu ya wananchi katika uwanja wa Tabasamu, wilayani Sengerema mkoani Mwanza jana.
“Wapo Watanzania ambao kila wakiona jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaheshimika duniani, kazi yao ni kushusha heshima ya nchi yao. Nawaomba tuachane nao, waacheni waende kivyaovyao. Hao siyo wenzetu.
“Tutaheshimisha nchi yetu kwa kuweka amani, kufanya uchaguzi bila matatizo, bila vurugu lakini tutaheshimisha nchi yetu kama tunafuata sheria zetu na tunafuata haki ndani ya nchi.
Alisisitiza: “Lakini nje ya nchi ni kuimarisha uhusiano kidiplomasia ambao mpaka hatua tuliyofikia jina letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni zuri sana, linaheshimika.”