Na HANIFA RAMADHANI,
Pemba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali, imeamua kuwapa wakulima hatimiliki za mashamba ya mikarafuu, ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo kutoka tani 10,000 hadi 20,000 kwa mwaka.
Dk. Mwinyi, aliyasema hayo katika hafla ya kukabidhi hati za mashamba ya karafuu Kisiwani Pemba, katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Alisema uzalishaji wa zao la karafuu, bado mdogo ukilinganisha na nchi nyingine zinazozalisha zao hilo, ikiwemo Indonesia.
Alisema kwa mwaka, wanavuna zaidi ya tani 100,000, mavuno ya Zanzibar bado yapo chini.
Alisema wametafakari na kutafuta sababu ya jambo hilo, wakabaini ni kutokuwa na uhakika kwa wale ambao wanayatunza mashamba hayo.
“Unaweza kuwa na shamba lako, kipindi cha msimu kikifika, unapewa taarifa kwamba, wizara imemkodisha mtu kuchuma na kupelekea watu kutoyatunza, ndiyo maana tija ikapungua na uzalishaji kuwa mdogo,” alisema.
Hivyo, alisema ni matarajio yake kwamba, hatua hiyo ya ugawaj hatimiliki, wakulima watayatunza vizuri, kwani ni mali yao na vizazi vyao, vinaweza kurithi.
Alieleza kuwa, ni vyema kuhakikisha wanapanda zao hilo kwa wingi kuongeza tani kutoka 10,000 hadi 20,000 kwa mwaka.
Aliwataka wananchi kuitumia fursa hiyo vizuri kwa kuyashughulikia na kuyaendeleza mashamba watakayokabidhiwa ili kilimo cha zao hilo, kiwe na tija kwao na taifa kwa ujumla.
Alisema ana imani watafanya kazi kwa bidii, kilimo chao hicho kizidi kuimarika na kuinua uchumi wa nchi.
Alisema wakulima wanapoamua kuyashughulikia na kuyaendeleza mashamba hayo, mazao huwa mazuri na hutolewa maamuzi ya kukodishwa kwa watu wengine pia faida zaidi, hupatikana.
Pia, alisema jambo hilo, halileti tija na malengo yaliyokusudiwa na serikali katika ugawaji wa ekari tatu kwa kila mmoja, hivyo kuondoa changamoto zote zinazokabili wakulima wa mashamba hayo.
Alisema serikali imeamua kutoa hati rasmi za matumizi kwa wananchi waliokabidhiwa mashamba hayo kwa utaratibu maalumu utakaowekwa na serikali.
Alisema serikali imefanya tathmini ya kina, ikiwemo ya kutafuta ushauri wa kisheria kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuangalia namna bora ya kuwakabidhi mashamba hayo wananchi ili malengo ya Mzee Abeid Amani Karume ya mwaka 1964, yafikiwe kikamilifu.
Aidha, alisema serikali inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wakulima wa karafuu, wanaendeleza shughuli zao za kilimo katika mazingira mazuri, kuwa na kilimo chenye tija.
Alisema mbali na uamuzi wa ugawaji wa hati kwa wakulima, serikali kupitia Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC), limeimarisha mfumo mzima wa ununuzi wa zao hilo kutoka kwa wakulima.
Dk. Mwinyi, alisema serikali imehakikisha mkulima wa zao hilo, hakopwi, anapatiwa fedha zake papo hapo kwa njia ya fedha taslimu kwa ujazo mdogo na kwa benki au kupitia mitandao ya simu.
Hata hivyo, Dk. Mwinyi, alisema serikali kupitia shirika lake, linaendelea na utaratibu wa kuwapatia bima wachumaji wa karafuu kila mwaka kwa watakaopata athari wakati wa uchumaji.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Rahma Kassim Ali, alisema utoaji wa hati hizo ni jambo la historia kwa wananchi wa Zanzibar.
Alisema hayo yote, yanatokana na maelekezo na miongozo ya Dk. Mwinyi, kuitaka wizara kutenda haki kwa wananchi na sasa jambo hilo limezaa matunda.
Mbali na hayo, alisema wizara imehakikisha kuwa, suala hilo limefanikiwa kwa Unguja na Pemba, wananchi wengi wamefahamu matumizi mazuri ya ardhi.
Naye, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Ardhi, Mussa Kombo, alisema suala la mashamba ya serikali, yana historia ndefu na kuwa, mara baada ya Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964, serikali iligawa mashamba kwa wanyonge, ambao hawakuwa na uwezo wa kupata ardhi Zanzibar.
Alisema wanyonge hao, waliitumia ardhi hiyo, kuimarisha maisha yao kupitia mashamba hayo ya serikali.