Na AMINA KASHEBA
TIMU ya Taifa ‘Taifa Stars’ itashuka dimbani leo kupambana na Zambia katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Mchezo huo umepangwa kufanyika saa 4:00 usiku katika Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar.
Akizungumza na vyombo vya habari, Kocha Mkuu wa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ amesema maandalizi yote yamekamilika kuelekea pambano hilo.
“Tuko vizuri wachezaji wote wamejipanga vizuri na kila moja anahitaji kuonesha ushindani, tunatambua mechi ni ngumu dhidi ya Zambia tutapambana kushinda,” alisema.
Morocco alisema wachezaji wake wapo fiti kuikabili Zambia na kushinda mchezo huo.
“Wachezaji wana morali ya kutosha kila moja nashukuru wana fanya vizuri, wananipa moyo kutokana na kiwango chao kuwa kizuri,” alisema Morocco.
Kocha huyo aliwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani katika mchezo huo kwa lengo la kuwapa hamasa wachezaji hao.
Mwakilishi wa wachezaji, Bakari Mwamnyeto alisema wachezaji wapo tayari kupambana katika mchezo huo kupata ushindi.
“Tumejipanga na tutasikiliza maelekezo ya mwalimu kwa lengo la kupata ushindi katika mchezo huu, tunatambua mechi ni ngumu tutahakikisha tunapata ushindi,” alisema.
Kocha wa Zambia, Avram Grants alisema wachezaji wake hawana presha kuelekea katika mchezo huo japokuwa utakuwa mgumu.
“Wachezaji wako vizuri kuelekea mchezo wa leo, kila kitu kipo sawa tumejipanga kuhakiksha tunapata ushindi,” alisema.
Kocha huyo alisema mipango yake ni kushinda katika mchezo huo, ingawa amekiri mchezo utakuwa mgumu, lakini hana wasiwasi wowote wa kupata matokeo mazuri.
Mwakilishi wa wachezaji wa Zambia, Kennedy Musonda alisema wamejipanga kuhakisha wanafanya vizuri katika mchezo huo.
“Natambua uzuri wa wachezaji wa Tanzania sisi wachezaji tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri na kupata ushindi, hatuna presha yoyote zaidi ya kupambana na kupata matokeo mazuri,”alisema Musonda.
Katika msimamo wa kundi E, Stars ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 10, Morocco inaongoza kundi hilo, ikiwa imefuzu huku ina pointi 21.
Timu ya Niger ipo nafasi ya tatu katika msimamo huo ikiwa na pointi tisa, Zambia ina pointi sita.
Timu ya Congo inaburuza mkia katika kundi hilo, ikiwa na alama moja.