Na NJUMAI NGOTA,
Pemba
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, wamefanya kazi kubwa kuwaletea Watanzania maendeleo makubwa katika nyanja zote.
Kimesema kina uhakika wa kupata ushindi wa kishindo katika visiwa vya Pemba na Zanzibar.
Hayo yalibainishwa Kinyasini, Wete Kaskazini Pemba, Zanzibar, na Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, alipohutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara wa kampeni za Chama kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.
Alisema kazi kubwa zilizotekelezwa na viongozi hao, zimesababisha wananchi wa Zanzibar na Bara, kuona fahari kuwa sehemu ya mafanikio hayo.
“Dalili ni kwamba, Chama chetu hapa Pemba kitapata ushindi wa kishindo.
“Mambo ambayo yamefanywa na Dk. Samia na Dk. Mwinyi ni makubwa katika nyanja zote,” alisema.
MARIDHIANO
Dk. Nchimbi, alisema katika miaka mitano ijayo, wakipewa ridhaa ya kuongoza nchi, wamedhamiria kuendeleza maridhiano na kwamba mafanikio ya Dk. Mwinyi katika kudumisha upendo na mshikamano, lazima yalindwe kitaifa.
“Chama chetu kimejizatiti kuendeleza maridhiano. Ndani ya siku 100 tukipewa ridhaa, Dk. Samia amesema tutaunda Tume ya Maridhiano kila mmoja asikilizwe,” alisisitiza.
AMZUNGUMZIA DK. MWINYI
Alisema anamfahamu vizuri, Dk. Mwinyi tangu walipofanya kazi katika Wizara ya Ulinzi, yeye akiwa Naibu Waziri wake kwa miaka mitatu.
“Sina shaka na dhamira yake ya kuwatumikia Wazanzibari, sina shaka na uwezo wake kwa nafasi aliyonayo na historia ya miaka mitano inajieleza.
“Changamoto pekee ambayo Dk. Mwinyi anayo, hana uwezo wa kujigambagamba, hana uwezo wa kujisifiasifia.
“Ana uwezo wa hali ya juu wa kuchapa kazi na kazi alizofanya Zanzibar, zinajieleza, naomba tumpe nafasi miaka mitano mingine atuletee mabadiliko makubwa,” alisema.
KAMPENI ZA CCM
Dk. Nchimbi, alisema kampeni za CCM zimekuwa rahisi kwa sababu, Dk. Samia amefanya kazi kubwa.
“Hivi sasa, nimwombee kura Dk. Samia, nataka nirudie kuwaambia kama kuna Mtanzania, mwanamke ametoa heshima ya nchi yetu ni Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kazi za maendeleo alizofanya katika miaka minne na nusu.
“Nataka niwaambie hakuna mfano wake katika nchi yoyote inayotuzunguka, ndiyo maana kampeni za CCM zimekuwa rahisi fuatilieni mikutano anayopita Dk. Samia, kila anakokwenda mamia kwa maelfu ya watu wanajitokeza kumwambia Dk. Samia, wao ndiyo anayewadai, sisi hatukudai, kila tunakokwenda wananchi wanasema mama unatudai tutakulipa kwa kura.
“Hapa wapemba fikisheni salamu, kama kuna kitu dunia itatushangaa basi ni kumpa kura chache,” alisema.
Aliwaomba wananchi wa Pemba kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, mwaka huu na kuwapa kura Dk. Samia, Dk. Mwinyi na wagombea wote wa CCM.
“Hata walio karibu na OMO (Othman Masoud Othman), nendeni mkamwombe kura kwa heshima. “Mwambieni mzee kazi aliyoifanya Dk. Samia mmeiona, kazi aliyoifanya Dk. Mwinyi mmeiona, basi tunaomba kura yake.
“Asitukanwe mtu, asidhalilishwe mtu, bali tuombe kura kwa heshima,” alisema.
Alisisitiza CCM itaendelea kuwa, nguzo ya amani, maendeleo na umoja wa Watanzania huku akiahidi kuwa, historia ya mapinduzi, muungano na mshikamano wa Watanzania, itaendelea kung’ara zaidi katika miaka mitano ijayo.
Akizungumzia kasi ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar, Dk. Nchimbi, alisema umefikia asilimia saba kutokana na ushirikiano wa wananchi na serikali, jambo linaloonesha mafanikio makubwa ya uongozi wa Dk. Mwinyi katika kuimarisha uchumi wa visiwa hivyo.
“Leo wanaCCM wanaona fahari kujinasibu na viongozi wetu hawa. Hawana makuu, hawana makeke, kwani kazi zao zinaonekana.
“Hatulazimiki kuongea hadi asubuhi kwa sababu, kazi zao zinaonekana,” alisema.
Alisema mafanikio makubwa yaliyofikiwa ni matokeo ya amani na umoja ulioendelezwa na viongozi hao, ambao wamehakikisha Muungano wa Tanzania, unabaki kuwa chachu ya mshikamano na maendeleo ya taifa.
“Kubwa kuliko yote yaliyofanyika ni umoja wa Watanzania na Wazanzibar.
“Tunu yetu imelindwa. Viongozi wetu wameendeleza kudumisha amani na usalama wa nchi yetu.
“Tumeahidi katika Ilani yetu kuendeleza usalama, amani, undugu na kusaidiana,” alisema.
Alisema CCM itahakikisha inaulinda muungano huo kwa gharama yoyote kwa sababu, ndiyo nguzo ya umoja wa Watanzania, ndani ya miaka mitano ijayo, Chama kimepanga kuimarisha taasisi zote za umma, ziwatumikie wananchi kwa ufanisi zaidi.
“Tutaendelea kuulinda muungano kwa sababu, tunasema umoja ni nguvu na Muungano wetu ni wa undugu.
“Tutaziimarisha taasisi zote za umma, ziwe na matokeo chanya kwa wananchi,” alisema.
DK. NCHIMBI AELEZEA
UHUSIANO WAKE, PEMBA
Pia, aligusia historia ya uhusiano wake na watu wa Pemba, akibainisha kuwa, tangu akiwa mdogo, alianza kujifunza siasa kutoka kwa Mkazi wa Pemba,Ramadhani Shaibu, aliyekuwa mwanafunzi wa siasa katika Chuo cha Polisi, Moshi.
“Nilivyokuwa darasa la pili kule Kilimanjaro, Mzee Shaibu alikuwa akija kunifundisha siasa, Mapinduzi ya Zanzibar na uongozi wa Abeid Aman Karume (Hayati). “Huyu mzee wangu yupo hapa leo, amekaa jukwaa kuu. Kwa hiyo, Dk. Samia, amefundishwa siasa na mzee Mberwa, nimefundishwa siasa na mzee Shaibu,” alisema.
RAIS DK. SAMIA AIISHI PEMBA
Alisema Dk. Samia, aliwahi kuishi na kusoma mikoa yote ya Pemba, jambo linaloonesha uhusiano wake wa karibu na watu wa visiwa hivyo.
“Dk. Samia alizaliwa Unguja, aliishi na kusoma Pemba, kama alivyoeleza mzee Mberwa. Hii inaonesha uhusiano wa damu na moyo aliokuwa nao na watu wa Pemba,” alisema.
Dk. Nchimbi, alisema Chama kimejipanga kuhakikisha miradi ya maendeleo, inaendelea kwa kasi zaidi ukiwemo ujenzi wa makumbusho ya Zanzibar itakayohifadhi historia ya Mapinduzi, usawa na umoja wa Wazanzibari.
“Tunakwenda kujenga makumbusho ya Mapinduzi ya Zanzibar, historia ibaki kizazi na kizazi. “Historia ya wapambanaji wetu wa Mapinduzi, lazima ihifadhiwe,” alisema.
Kuhusu uchumi, alisema serikali ya CCM itaendeleza sera za uchumi wa bluu ulioanzishwa na Dk. Mwinyi kwa kuboresha Bandari ya Wete, kuimarisha ufungaji wa samaki, kukuza kilimo cha mwani na uvuvi wa kisasa.
“Hivi sasa Zanzibar inazalisha tani 80,000 za samaki kwa mwaka. Ndani ya miaka mitano ijayo tunataka ifikie tani 160,000. Tutaboresha zana za uvuvi na sekta hii itatoa ajira nyingi,” alisema.
Kuhusu sekta ya kilimo cha umwagiliaji, Dk. Nchimbi alisema itapewa kipaumbele kwa kutoa mbegu bora, mbolea, mikopo na masoko ya uhakika kwa wakulima wa karafuu, matunda na mboga.
Kwa upande wa miundombinu, alisema CCM imejipanga kuboresha Uwanja wa Ndege wa Pemba uwe wa kimataifa, jambo litakaloongeza idadi ya mizigo, watalii na ndege zinazotua visiwani humo.
“Tunakwenda kuboresha Uwanja wa Ndege wa Pemba uwe wa kimataifa. Ndege kubwa zitakuja kutua, watalii wataongezeka na mizigo itaongezeka,” alisema.
Alitaja barabara kuu na za ndani zinazotarajiwa kujengwa ikiwemo Chake–Mkoani, Mtambile, Chakechake na Stendi–Chakechake, ambazo zitasaidia kuunganisha maeneo muhimu ya Pemba na kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa.
Katika huduma za maji safi, Dk Nchimbi alisema mpango wa CCM ni kuhakikisha miaka mitano ijayo, asilimia 90 ya wananchi wa Zanzibar wanapata maji safi na salama kwa kuchimba visima, kujenga matenki ya kisasa na kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa maji ya mvua.
“Hivi sasa robo tatu ya maji ya mvua yanapotea. Tunataka kuyaokoa kwa ujenzi wa miundombinu bora ya ukusanyaji,” alisema.
Alisema katika sekta ya elimu, wamekusudia kuimarisha Zanzibar kwa kujenga shule za msingi na sekondari na kuongeza vyuo vya amali, vijana wapate ujuzi na ajira.