Na SELINA MATHEW,
Kigoma
MGOMBEA Mwenza wa Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema kutumikia wananchi ni kipaumbele cha kwanza cha CCM, ndiyo maana kimeendelea kuaminiwa.
Hayo aliyasema wakati akiomba kura kwa wananchi na wanaCCM katika Wilaya ya Kigoma Vijijini, Jimbo la Kigoma Kaskazini mkoani Kigoma.
“Tunaomba kura kwa miaka mitano ijayo, baada ya kukamilika mitano iliyopita, ambayo Rais Samia na serikali ya CCM, imefanya mabadiliko na maendeleo katika historia ya nchi yetu,
“Chama Cha Mapinduzi, kimeweza kwa mara nyingine kujithibitisha kwa umma kwamba, kina uwezo wa kuhangaika na maendeleo ya watu,”alisema Nchimbi.
Alifafanua kuwa, kuna vyama duniani havina haja na watu, vinashughulika na maendeleo yao ya uongozi pekee.
“Tuna viongozi duniani ambao hawajali maslahi ya watu wengine, tuna chi zipo Bara la Afrika, ambazo kwa habari za afya, elimu, miundombinu ya watu, wao haviwahusu wala vyama vya siasa.
“Lakini, CCM imethibitisha kwa vitendo kwamba, mambo yanayohusu wananchi wake ndiyo yanayohusu viongozi na uongozi wa CCM,” alisema Balozi Nchimbi.
Alibainisha kuwa, ndiyo maana Dk. Samia kwa kufuata misingi ya CCM, ameweza kujisimamia vizuri na kuhakikisha chama kinaendelea kusimama imara.
Alisema katika miaka yake ya uongozi, amekiimarisha Chama kwa kiwango cha hali ya juu, hali iliyosababisha wanachama kuongezeka kwa zaidi ya milioni 13.5, mabalozi na kamati zao wapo 800,000.
“Hii ni aina ya uongozi ambao umetoka juu mpaka chini ambao haupo katika nchi yoyote Afrika Mashariki na Kati. Chama chetu kimeendelea kujitambulisha na wananchi wa kawaida.
“Fahari kwa Chama chetu ni watumishi wa wananchi, kutumikia watu wetu ni kipaumbele cha kwanza, ndiyo maana Serikali za CCM katika ngazi zote, zinahangaika na maisha ya watu, kero,”alisema Dk. Nchimbi.
Alisema ndiyo maana CCM, inaendelea kuaminiwa na wananchi wote na imepata sifa na kuombwa katika nchi nyingine kwenda kutoa mafunzo.
Alisema miaka mitano iliyopita, CCM imewezesha baadhi ya mambo ya msingi kutekelezeka, yakiwemo maeneo ya afya, elimu, maji, miundombinu na nishati kufanya vizuri kuliko miaka mingine.
Alibainisha ndani ya miaka minne, uwekezaji umeongezeka zaidi ya mara nne, mazingira ya biashara yameimarika, utalii umekua, anaamini mabadiliko yaliyotokea katika kukuza uchumi, yatafanya uimarike zaidi.
Alisema Dk. Samia aliigiza filamu na kuisambaza dunia nzima na kuleta heshima kwa wanawake nchini.
“Kila aliyekuwa na mashaka kuhusu uwezo wa wanawake wa Tanzania, hana mashaka tena, wanawake wa hapa nchini hakuna nafasi walizopewa wakashindwa kutumikia,”alisema Dk. Nchimbi.
YATAKAYOFANYIKA
Dk. Nchimbi, alifafanua kuwa, mambo yatakayotekelezwa kupitia ilani ya 2025/30 katika jimbo hilo, ni ujenzi wa soko la mafuta ya mawese eneo la Mwandiga.
Alisema kuimarisha diplomasia ya uchumi kupata masoko nje ya nchi na mahusiano kati ya mkoa huo na nchi jirani za Burundi, Zambia na nyingine ili kuwa na masoko ya uhakika ya mazao.
Vilevile, alisema sekta zisizo rasmi, zitarasimishwa ili wafanyabiashara wanaofanya biashara zisizo rasmi, wakopesheke.
Kuhusu uwezeshaji wananchi kiuchumi, alisema mikopo ya asilimia 10, itaimarishwa katika halmashauri na kufanya mabadiliko makubwa.
Pia, utafanyika ujenzi wa vituo vya afya vinne, zahanati saba, nyumba za watumishi 12 katika sekta ya afya na kujenga shule za msingi tano, sekondari tatu, madarasa mapya 73 na nyumba za walimu 21 na mabweni.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kigoma Vijijini, alisema wananchi wanalengo la kukipa ushindi CCM kupitia kura za kishindo ambapo watarundika kura katika sanduku.