Na MUSSA YUSUPH,
Bukombe
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa vijana kutokubali kurubuniwa na watu wenye dhamira ya kuharibu amani na utulivu uliopo nchini.
Amesisitiza vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda amani kwani hakuna mahali pakukimbilia, endapo utulivu ukitoweka nchini.
Akizungumza na maelfu ya wananchi katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika Lunzewe wilayani Bukombe mkoani Geita, amesema Tanzania ni taifa lenye kuheshimika duniani.
“Ninalotaka kuwaambia vijana, nchi inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo moja peke yake. Tangu nchi hii imeundwa tumepigana vita moja na tu Iddi Amin (aliyekuwa Rais wa Uganda) kwa sababu alituchokoza.
Amesisitiza: “Lakini miaka yote nchi hii ipo salama, tuna amani. Sisi tulikuwa wadogo tulizaliwa, tukakuzwa katika amani. Tumekuwa wakubwa tunaendesha nchi hii bado tunalinda amani.”
“Vijana twendeni tukalinde amani yetu, tusikubali kwa hali yoyote kushawishiwa kuharibu amani yetu. Hamtakwenda kuchimba (madini) hamtakwenda kwenye muziki, hamtafanya chochote amani ikiharibika,” ameeleza.
Dk. Samia amesema endapo amani ikiharibika nchini hakuna mahali pengine kwa wananchi kukimbilia, kwani hata raia kutoka mataifa ya kigeni wapo nchini kwa sababu ya utulivu uliopo.
“Wakati nakuja huku (Geita) nilisimama Kahama ambako kuna mchanganyiko wa watu kutoka nchi jirani. Wote wapo pale wamefuata biashara, wamefuata maisha, wamefuata amani.
“Kama wale wanakuja huku nyie mtakwenda wapi?, Hamtapata pakukimbilia. Pakukimbilia ni hapa kwetu. Niwaombe kwa njia yoyote ile asije mtu akasema fanyeni hiki mkavuruga amani ya nchi yetu mkaharibu sifa nzuri ya Tanzania,” amebainisha.
Awali, katika mkutano wake uliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Bukombe, Dk. Samia amewahakikishia wananchi atawatumikia kuleta maendeleo na kujenga taifa jumuishi.
Amesema wachimbaji wa wilaya hiyo walikuwa wakivamia Pori la Akiba Kigosi Moyowosi kuchimba madini ya dhahabu kwa njia isiyokuwa rasmi.
Ameeleza rasilimali hiyo ambayo Mwenyezi Mungu ameishusha nchini iwanufaishe vijana, serikali imeamua kuwamilikisha baadhi ya maeneo kuliko vijana kuendelea kuiba.
“Kuliko wapigwe na askari wa uhifadhi, wapelekwe mahakamani, nikasema hapana. Nikamtaka Dk. Doto Biteko na wenzake serikalini, waangalie namna watakavyofanya rasilimali hiyo iwafae vijana wa Bukombe.
Ameongeza:”Leo wanachimba, wanauza, tumewajengea masoko na maisha yanakwenda vizuri sana. Huku ndiko kujenga utu wa Mtanzania, ndiko kujenga utu wa vijana wetu. Ndiko kuwawezesha waendelee na maisha yao yawe mazuri wapate heshima ya kutosha.”
Kwa upande wa kilimo, Dk. Samia alisema wapo wakulima ambao muda mrefu walikuwa wakitaka kuvuna kwa kiasi kikubwa wapate fedha za kutosha kuendesha maisha yao.
Amebainisha hatua zilizochukuliwa na serikali ni kuwapa ruzuku ya mbolea, dawa za kilimo kisha kuwajengea skimu za umwagiliaji walime na kuzalisha mazao kwa wingi.
Vilevile, amesema wilaya hiyo ina wafugaji wa ng’ombe wa nyama na maziwa, ambapo serikali inajipanga kuongeza nguvu katika ng’ombe wa maziwa.
Amesema mpango huo wenye lengo la kuinyanyua sekta ya maziwa, serikali itaweka viwanda vitakavyochakata maziwa wafugaji wauze bidhaa hiyo kuongeza kipato chao.
Ameeleza serikali imeweka jitihada kubwa kufikisha huduma hizo katika maeneo ya wananchi.
“Tulitambua katika elimu tulikwenda hadi kidato cha sita, hivyo vijana wa Bukombe wanahitaji chuo ambacho tayari ujenzi unaendelea.”
BALOZI DK. MIGIRO
Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Asha-Rose Migiro alisema mafanikio ya Watanzania hayapo katika maneno, bali ni matendo.
Alieleza kwa kipindi kirefu wananchi wa Bukombe wameshuhudia utekelezaji miradi ya maendeleo katika afya, elimu na miundombinu hatua inayothibitisha CCM ikiahidi inatekeleza.
Alisema Dk. Samia amefungua fursa kwa vijana na kuleta mageuzi ya kiuchumi kupitia uwekezaji na ujenzi wa miradi ya kimkakati.
“Amefanya kazi kuhakikisha maendeleo hayapo mijini pekee bali hata vijijini. Kwa kutambua nguvu kubwa zaidi inapaswa kuelekezwa vijijini ndipo nguvu kazi kubwa ya wananchi wanaishi.
“Hapo ndipo lengo kuu la Dk. Samia kuelekeza nguvu kubwa mahali ambako Watanzania wengi wanapatikana na huo ndiyo utu. Tuna kila sababu kusema Oktoba 29 hakuna mbadala ni Samia,” alieleza.
DK. BITEKO AELEZA
Kwa upande wake, mgombea ubunge Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko, alisema katika kipindi chote Dk. Samia alipoanza kampeni hajawahi kuzungumzia watu binafsi.
Alisema Dk. Samia ametoa somo kwa wagombea kuzungumzia changamoto zinazowakabili wananchi na hatua za kuzitatua.
Biteko alisema Dk. Samia amethibitisha utu kwa kujenga daraja la maridhiano ikiwemo kuweka katika ilani ya uchaguzi mchakato wa katiba mpya.
Alieleza mgombea huyo urais kupitia CCM ametoa somo la kutenda zaidi badala ya kuzungumza, kwani katika kipindi cha uongozi wake ametoa msisitizo kazi zinapimwa kwa maendeleo yanayoonekana na siyo maneno.
Alibainisha Mwenyezi Mungu amelipatia taifa kiongozi mwenye maono makubwa kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa.
Vilevile, alisema amekutana na makundi ya kijamii wakati wa kampeni ambayo wamemtuma kumshukuru kwa maendeleo yaliyopatikana.
“Mengine umeyafanya nje ya ilani ambayo hata usingeyafanya hakuna mtu angekudai. Wilaya yetu kulikuwa kuna kata hazina shule za sekondari lakini hivi sasa zipo kata zenye shule tano.
“Umetujengea chuo cha VETA chenye hadhi ya kitaifa, kwa habari ya maji wakati unaingia upatikanaji ilikuwa chini ya asilimia 20, lakini sasa ni zaidi ya asilimia 60 huku miradi mingine ikiendelea kutekelezwa,” alisema.
Dk. Biteko alisema tangu wilaya hiyo ilipoanzishwa haikuwa na jengo la utawala la mkuu wa wilaya, lakini tayari ujenzi wa jengo hilo umeanza, pia mtandao wa barabara umefikia kilometa 1,400 kutoka kilometa 200 za awali.
Mratibu wa uchaguzi katika kanda hiyo, Aggrey Mwanri, alisema waratibu wa uchaguzi wanamthibitishia Dk. Samia ataibuka na ushindi wa kishindo.
NEEMA WACHIMBAJI WADOGO
Kwa upande wake, mgombea ubunge Jimbo la Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alisema Dk. Samia ametoa mitambo maalumu ya uchorongaji madini.
Pia, alisema Dk. Samia alitoa maelekezo kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapewa mafunzo, ambapo katika eneo la Bukombe kimeanzishwa kituo cha mafunzo ya uchenjuaji dhahabu.
Alieleza Dk. Samia ameagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Wizara ya Fedha kupitia Mfuko wa Dhamana, kuwawezesha wachimbaji wadogo waanze kumiliki migodi mikubwa na kuanza kununua madini.
“Umetuelekeza katika mashine 15 za kuchoronga, mbili ziende kwa kina mama na vijana kurahisisha shughuli za uwezeshaji wananchi,” alibainisha.
ONGEZEKO LA WATALII
Mgombea ubunge Jimbo la Arusha Mjini, Paul Makonda, alisema Dk. Samia amefanya makubwa katika sekta ya utalii.
Alisema mwaka 2021 utalii ulikumbwa na changamoto iliyosababishwa na maradhi ya Uviko-19, hata hivyo Dk. Samia alipoingia madarakani ameleta mageuzi makubwa.
Alisema watalii waliokuwa wanaingia nchini walikuwa 700,000 lakini hivi sasa watalii wa kigeni wamefikia zaidi ya milioni mbili huku watalii wa ndani wakifikia zaidi ya milioni tatu.
Makonda alisema hatua hiyo imewezesha kufikia ongezeko la watalii zaidi ya milioni tano ikiwa wa wastani wa asilimia 9.2, jambo lililowezesha kuvuka lengo la ilani ya uchaguzi iliyopita.
Aliongeza waongoza watalii idadi imeongezeka kutoka 1,000 wa awali hadi kufikia 6,000.
JESCA MAGUFULI AFUNGUKA
Mgombea ubunge viti maalumu, Jesca Magufuli, alisema Dk. Samia ni kiongozi shupavu ambaye katika kipindi cha miaka minne ametekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.
Alisema pamoja na kutekeleza miradi hiyo aliyorithi kutoka kwa mtangulizi wake Hayati Dk. John Magufuli, ameanzisha miradi mingine ya kimkakati.
“Wengi tunafahamu adha tuliyokuwa tukikumbana nayo Daraja la Kigongo-Busisi. Ametufanyia makubwa sisi wakazi wa Kanda ya Ziwa.
“Tuna kila sababu ya kumwamini kiongozi wetu, tukajitokeze kwa wingi kumpigia kura Dk. Samia ifikapo Oktoba 29 mwaka huu,” alisisitiza.
Jesca alisema katika ilani ya uchaguzi (2025-2030) CCM imeahidi kutengeneza ajira zaidi ya milioni nane, kutoa mafunzo kwa vijana na kukuza teknolojia kuongeza wigo wa ajira kwa vijana.