Na SELINA MATHEW,
Kakonko
MGOMBEA Mwenza wa Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi amewashukuru na kuwasihi viongozi wa dini nchini kuendelea kuiombea nchi amani.
Balozi Dk. Nchimbi aliyasema hayo katika Wilaya ya Kakonko, mkoani Kigoma alipomuombea kura mgombea Urais kupitia CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani.
“Nawashukuru viongozi wa dini mmesisitiza amani, utulivu, mshikamano, upendo hayo ndiyo mambo ambayo yameombewa kwa nchi yetu, wamesisitiza nchi yetu iendelee kuwa na umoja. Kupitia kwao, nawashukuru viongozi wote wa dini nchini ambao hawajawahi kaucha kuiombea nchi,” alisema.
Aliwasihi viongozi hao kuendelea kuiombea nchi na kuhimiza nafasi waliyonayo ni kuhakikisha wanasimamia walichokiahidi nchi iendelee kuwa na mshikamano, umoja, haki na inayojali wananchi wote.
“Baba wa taifa alituachia nchi ikiwa na amani hivyo ni wajibu wetu tunapopewa ridhaa kuhakikisha tunaikabidhi nchi kwa vizazi vijavyo ikiwa na umoja, amani na mshikamano,” alieleza.
Katika hatua nyingine, Dk. Nchimbi aliwashukuru wananchi wa Kigoma kupitia ziara iliyofanywa na mgombea Urais Dk. Samia, ambayo ilitoa salamu mkoa huo ni ngome ya CCM.
“Ninawashukuru kwa mapokezi mazuri na mazito, pokeeni salamu za umoja na mshikamano kutoka kwa Rais wetu amenituma niwape salamu nyingi za upendo na mshikamano anashukuru kwa ziara ya Kigoma iliyotoa salamu kwa nchi nzima kwamba ni ngombe ya CCM,”alisema Dk. Nchimbi.
YATAKAYOFANYIKA KAKONKO
Balozi Nchimbi alisema miaka mitano ijayo katika wilaya hiyo zitajengwa skimu mpya za umwagilaji, visima na kuimarisha kilimo kupitia maofisa ugani wasaidie ulimaji wa kistaarabu na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia chakula.
Kuhusu kilimo alisema suala la ruzuku ya mbolea, mbegu na pembejeo litaendelea kutekelezwa kwa nguvu zote kuhakikisha wanachi wananufaika na sekta hiyo.
Eneo la ufugaji, alisema kila mfugaji atajua umuhimu wa chanjo na kutoa ruzuku katika suala hilo ikiwemo ujenzi wa majosho.
Kuhusu wafanyabiashara alisema mazingira mazuri yataweka kwao wafanye sehemu yoyote bila kubughudhiwa na wasaidiwe badala ya kunyanyaswa.
Pia, diplomasia ya uchumi itaimarishwa kwa kuwa wilaya hiyo iko mpakani mwa nchi, hivyo miaka mitano ijayo nchi hizo zitanufaika kupitia biashara.
Katika sekta ya elimu alisema miaka mitano ijayo eneo hilo zitajengwa shule mpya za msingi nne, sekondari mpya tatu na madarasa mapya 107.
“Kwa kuwa watoto wanapenda masomo ya sayansi tutajenga maabara 16, mabweni mapya 10,”alisema Dk. Nchimbi.
Alisema eneo la afya, miaka mitano ijayo itaimarishwa hospitali ya wilaya na kuongeza madaktari bingwa wanachi watibiwe kwa urahisi, vituo vipya vya afya vitano vitajengwa zikiwemo zahanati mpya tisa.
Kuhusu nishati ya umeme, alisema miaka mitano ijayo wamedhamiria vijiji vyote na vitongoji viwe vimefikiwa na umeme ikiwemo kuendelea kuwawawezesha wananchi mikopo ya asilimia 10 kutoka halmashauri.
Vilevile, alisema CCM ikipewa ridhaa nyingine ya kuongoza watatengeneza ajira milioni nane kwa vijana na kuahidi watakamilisha miradi ya maji katika vijiji vilivyopo wilaya hiyo, upanuzi wa skimu za maji na uchimbaji visima virefu.
MAMBO YA KITAIFA
Dk. Nchimbi alifafanua Dk. Samia amefanya mabadiliko makubwa ikiwemo kuwaheshimisha wakulima nchini, ambapo asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo na asilimia 26 ya pato la taifa inatokana na sekta hiyo.
“Rais amewapata heshima na nafasi ya pekee kupitia kilimo, wakati anaingia madarakani bajeti ilikuwa kidgo lakini sasa imefikia zaidi bilioni moja. Uwezo wa serikali kutoa ruzuku katika mboleo hivi sasa umeongezeka na uzalishaji chakula umepanda,” alisema.
Alifafanua mageuzi hayo makubwa yameiwezesha nchi ya kujitegemea na kujitosheleza kwa chakula.
Balozi Nchimbi alisema Dk. Samia ameleta mabadiliko makubwa ndani ya miaka minne iliyopita ikiwemo kuongeza bajeti iliyowezesha ujenzi wa majosho, malambo na kiwango cha uzalishaji nyama kimeongezeka.
“Katika miaka minne Dk. Samia amejenga hospitali za halmashauri, vituo vya afya na kuongeza idadi ya mifumo ya kisasa ya kutolea huduma katika hospitali na kuboresha elimu kwa kujenga shule mpya za msingi na sekondari bila kusahau miundombinu,” aliongeza Dk. Nchimbi.