Na ABDUL DUNIA
WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara ikisimama kupisha mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026, Simba ndiyo timu iliyofunga mabao mengi katika michuano hiyo hadi sasa msimu huu.
Katika michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi za klabu nchini, jumla ya mabao 36 yamefungwa msimu huu, huku Simba ikipachika mabao sita.
Kwa mujibu wa msimamo wa ligi hiyo, jumla ya michezo 20 imechezwa ambapo baadhi ya timu zimeingia dimbani mara mbili na nyingine mara tatu.
Katika mchanganuo wa mabao, Simba inafuatiwa na JKT Tanzania na Dodoma Jiji zilizofunga mabao manne kila moja.
Yanga na Azam FC zimepachika mabao matatu kila moja zikifuatiwa na Singida Black Stars, Mashujaa, Namungo, Mtibwa Sugar, Coastal Union na Tabora United zilizopachika mabao mawili.
Timu zilizofunga bao moja ni Mbeya City, Tanzania Prisons, KMC na Pamba Jiji.
Hata hivyo ni Fountain Gate pekee ambayo hadi sasa haijapachika bao lolote katika mitanange mitatu iliyocheza msimu huu.
Akizungumza kwa njia ya simu, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema kikosi chao kimedhamiria kufanya vyema zaidi msimu huu.
“Sisi ni timu kubwa na tunahitaji mambo makubwa, huu ni mwanzo tu na Wanasimba wanapaswa kujua kwamba tuna timu ya kutoka kifua mbele kufanya makubwa katika kila mechi,” alisema.