Na MWANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mwanasiasa nchini Kenya, Raila Odinga, kilichotokea asubuhi nchini India.
Odinga (80), amefariki dunia asubuhi ya Oktoba 15, 2025 katika Wilaya ya Kerala nchini India baada ya kupata mshtuko wa moyo.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Dk. Samia, aliandika kuwa, amepokea kwa masikitiko makubwa, taarifa ya kifo cha kiongozi mahiri, Odinga.
“Tumempoteza Mwanamajumui wa Afrika, mpenda amani na mtafuta suluhu, ambaye ushawishi na upendo wake, haukuwa tu ndani ya Kenya, bali Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
“Msiba huu si wa Kenya pekee, bali wetu sote,”alisema Dk. Samia katika taarifa yake.
“Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatuma salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Dk. William Ruto, Mama Ida Odinga, watoto, familia, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wote wa Kenya kwa msiba huu.
“Tunaungana kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu, awajalie subra, faraja na imani katika kipindi hiki na ailaze roho ya mpendwa wetu, Odinga, mahali pema peponi,”aliandika Dk. Samia.
RIGATHI GACHAGUA
Naye, kinara wa Chama cha DCP nchini Kenya, Rigathi Gachagua, alimuomboleza Odinga kama mtu aliye na heshima kubwa nchini, Kenya na Kimataifa.
Kupitia ukurasa wake wa X, Gachagua alimtaja Odinga kama baba wa demokrasia na shujaa shupavu wa ukombozi wa pili wa taifa.
Alimkumbuka Odinga alivyojitoa kupigania utawala wa kidemokrasia, licha ya kupitia mateso ya kifungo, utesaji na kuwekwa kizuizini mara kadhaa.
“Pumzika kwa amani Baba na nuru ya milele ikuangazie daima,” alisema Gachagua.
TUME YA UMOJA WA AFRIKA
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Mahmoud Ali Youssouf, alituma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mwanasiasa wa upinzani Kenya na Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Odinga
Youssouf alimtaja Odinga kama mtu mashuhuri katika maisha ya kisiasa na mpiganaji thabiti wa demokrasia, utawala bora na maendeleo yanayozingatia watu, ameacha alama isiyofutika siyo tu kwa Kenya, bali bara zima la Afrika.
“Afrika imepoteza mmoja wa wanawe wenye maono; kiongozi aliyejitolea maisha yake kutafuta haki, demokrasia na umoja.
“Urithi wake utaendelea kujenga Afrika yenye amani, ustawi na demokrasia,”alisema.
KENYATTA AMLILIA
Aliyekuwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, alituma salamu za rambirambi kwa familia ya Odinga.
Kupitia ujumbe wake wa mtandao wa Instagram, Kenyatta alimtaja Odinga kama mwenzake katika safari yake yote ya kisiasa.
“Nimepoteza rafiki na kaka. Kwangu mimi, Raila alikuwa zaidi ya mwenzangu wa kisiasa, alikuwa sehemu ya pekee ya safari yangu, katika utumishi wa umma na maishani,” alisema Kenyatta.
HICHILEMA AOMBOLEZA
Naye, Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, alituma salamu za pole kufuatia kifo cha Odinga.
Katika taarifa yake kupitia mtandao wa X, Hichilema alisema: “Nasikitika kusikia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga.
“Tunatuma rambirambi zetu kwa watu wa Kenya, familia ya Odinga, Rais wa Kenya, William Ruto na wote walioguswa na mtetezi huyu mkuu wa demokrasia.”
Alisema kuwa, urithi wa Odinga, utadumu, amemtakia apumzike kwa amani ya milele.
WAZIRI MKUU WA INDIA
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, alimtaja Odinga kama kiongozi mashuhuri na rafiki wa dhati nchini India.
Kupitia ukurasa wake wa X, Narendra, alisema mchango wa Odinga katika kukuza uhusiano kati ya India na Kenya, ulikuwa wa kipekee, na kwamba, kumbukumbu zake zitaendelea kuenziwa.
Alisema Odinga alikuwa sauti ya hekima, demokrasia na mshikamano barani Afrika na kwamba, dunia imepoteza kiongozi wa kweli.
Alituma salamu za rambirambi kwa familia ya Odinga, wananchi wa Kenya na wote walioguswa na msiba huu na kuwatakia faraja na nguvu katika kipindi hiki kigumu.
Modi alieleza kuwa, Odinga alipendelea tiba ya Ayurveda na tiba asili za India kutokana na ufanisi wake katika afya ya binti yake.
“Alikuwa na mapenzi kwa India kuanzia tiba zetu na utamaduni wetu,” alisema.




