Na NJUMAI NGOTA,
Singida
MGOMBEA Mwenza wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema katika miaka mitano ijayo, CCM imedhamiria kukamilisha ujenzi wa reli ya kisasa ya mwendokasi ya SGR kutoka Dodoma, Tabora, Mwanza na Kigoma ambayo itapita wilayani Itigi mkoani Singida.
Dk. Nchimbi, amesema hayo katika Uwanja wa Mpira wa Mitundu, wilayani Itigi, mkoani Singida, alipohutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara wa kampeni za Chama, kuelekea Uchaguzi Mkuu, utaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
“Katika miaka mitano ijayo, kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025 hadi 2030, tutahakikisha tunakamilisha ujenzi wa reli ya kisasa ya Mwendokasi (SGR) kutoka Dodoma kwenda Tabora, Mwanza na Kigoma, ambayo inapita hapa Itigi,” amesema.
Amesema ujenzi wa reli hiyo, siyo utarahisisha usafiri wa abiria na mizigo, bali utachochea ukuaji wa biashara, ajira kwa vijana na kuongeza thamani ya mazao ya wakulima katika mikoa yote inayopitiwa na reli hiyo.
Pia, amesema Serikali ya CCM ijayo, imepanga kujenga kituo kikubwa cha kupooza na kusambaza umeme wilayani Itigi.
Akielezea mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama ya mwaka 2020-2025, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia katika ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, ni miongoni mwa miradi mikubwa iliyogusa moja kwa moja maisha ya wananchi wa eneo hilo.
Amesema katika kipindi cha miaka minne na nusu, serikali imeendelea na ujenzi wa reli hiyo kwa kasi kubwa, hatua zilizofikiwa hivi sasa, zinatia moyo na kipande kinachopita wilayani Itigi, kimefikia hatua za mwisho za ukamilishaji.
Amesema Dk. Samia, alipoingia madarakani, aliahidi kuendeleza ujenzi wa reli hiyo, hivi sasa wanashuhudia kazi hiyo ikiendelea kwa kasi.
IKUNGI
Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema miaka mitano ijayo, iwapo watapewa ridhaa kuongoza nchi, watashirikiana na Bodi ya Mazao na kuhakikisha bei zinaendelea kuwa nzuri.
Akiwa Ikungi, Dk. Nchimbi, alisema Serikali ya CCM, imepanga kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya kilimo, kuwainua wakulima.
Alisema kuwa, katika sekta ya kilimo, wanakwenda kufanya mambo makubwa.
“Tunakusudia kujenga maghala ya mazao, tunakwenda kujenga skimu za umwagiliaji, wakulima walime kwa kutegemea umwagiliaji, badala ya mvua peke yake,”alisema.
Pia, alisema Serikali ya CCM, haitawaangusha wakulima na wafugaji, hivyo wataongeza ruzuku ya mbolea na mbegu na kuimarisha huduma za ugani kwa kilimo cha kitaalamu.
HUDUMA ZA AFYA
Vilevile, alisema Serikali ijayo ya CCM, itaweka mkazo mkubwa kuboresha huduma za afya wilayani humo kwa kujenga majengo katika Hospitali ya Wilaya ya Ikungi.
Pia, kuongeza vifaatiba na wataalamu, hospitali hiyo itoe huduma za kibingwa zinazopatikana maeneo mengine.
Katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa maeneo ya vijijini, Dk. Nchimbi, alisema Serikali ya CCM, inakusudia kujenga zahanati 16, vituo vya afya 10 wilayani humo na kukamilisha nyumba 19 za wahudumu wa afya.
ELIMU
Kuhusu sekta ya elimu, Dk. Nchimbi, alisema Serikali ya CCM, imepanga kujenga shule za msingi 11, sekondari saba na madarasa 140 katika shule za zamani na ujenzi wa nyumba za walimu 21, kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
KUHUSU UFUGAJI
Kwa upande wa ufugaji, Serikali ya CCM, imepanga kuimarisha bajeti ya Wizara ya Mifugo, kujenga majosho mengi zaidi, malambo ya kuhifadhi maji kwa mifugo na machinjio ya kisasa.
SEKTA YA MADINI
Akizungumzia sekta ya madini, Dk. Nchimbi alisema Serikali ya CCM, itaendelea kuwaunga mkono wachimbaji wadogo kwa kuongeza masoko ya madini.
Dk. Nchimbi, alisema mbali na soko la Shelui lililopo hivi sasa, masoko mengine yataanzishwa Puma na maeneo mengine.
Dk. Nchimbi, alisema sekta ya maji, wameahidi kuongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 73 hadi 85 kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maji ya visima virefu, mvua na kuunganisha wilaya hiyo na mtandao wa kitaifa wa maji kutoka Ziwa Victoria.
Alisema katika sekta ya barabara, serikali imepanga kujenga barabara mbalimbali kwa kiwango cha lami na changarawe, zinazopitika muda wote.
MGOMBEA UBUNGE
Naye, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ikungi Magharibi, Elibariki Kingu, alisema wananchi wa Singida, wapo tayari kuvunja rekodi ya kura za urais mwaka huu kwa kumpigia Dk. Samia na Nchimbi, kutokana na kazi kubwa iliyofanyika ndani ya miaka minne iliyopita.
Kingu alisema kila kata na kijiji ndani ya wilaya hiyo, imeguswa na Serikali ya Awamu ya Sita, kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aidha, Kingu alimpongeza Dk. Nchimbi kwa kuteuliwa kuwa, Mgombea Mwenza, akimwelezea kama kiongozi shujaa, mchapakazi, mzalendo, mtiifu na anakipenda Chama.




