Na MUSSA YUSUPH,
Rukwa
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema katika miaka mitano ijayo serikali itajenga gridi ya taifa ya maji ambayo itamaliza changamoto ya maji nchini.
Amesema gridi hiyo itajumuisha vyanzo vikuu vya maji kutoka Ziwa Victoria, Nyansa na Tanganyika kisha kuungwa katika mtandao wa maji unaojumuisha vyanzo vingine ambavyo ni mito, mabwawa na visima.
Dk. Samia amesema kupitia mtandao huo, Tanzania itakuwa na hifadhi ya maji ya kutosha hivyo eneo moja endapo likikosa huduma kwa sababu ya hitilafu, gridi itapeleka maji kuziba pengo husika.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Shule ya Sekondari Kizwite mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, Dk. Samia amesema lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa karibu na huduma ya maji.
“Huko ndipo tutakapotoa njia tatu hizo (Ziwa Victoria, Nyasa na Tanganyika) ambazo zitakwenda mahali zikutane tutengeneze gridi ya taifa ya maji. Tuwe na hifadhi ya maji mengi.
“Upande wowote ukikosa maji, basi gridi inafanya kazi kugawa maji upande ambao umekosa maji. Kwa hiyo tunapozungumza maji safi na salama hatutanii. Tumejipanga kutumia fedha nyingi kutengeneza gridi ya taifa kila Mtanzania awe karibu na maji safi na salama,” ameeleza.
UNUNUZI MAHINDI
Akizungumzia ombi la ununuzi mahindi ya wakulima, Dk. Samia alimwagiza Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, kuangalia namna ambavyo serikali itanunua mahindi hayo.
“Nipo hapa na Waziri wa Fedha na Waziri wa Kilimo (Hussein Bashe). Najua bajeti tuliyoitoa ya ununuzi wa mahindi tuliimaliza, lakini wanasema jungu kuu halikosi ukoko. Waziri wa Fedha kachungulie katika jungu kuu tuone tutapata kiasi gani tuendelee kununua mahindi.
Aliongeza: “Tatizo ni kwamba tumetoa mbolea nyingi. Watu wamezalisha, tumepima udongo, tumeleta mbegu watu wamezalisha kwa wingi. Sasa uzalishaji kwa wingi kutahitajika maghala yawe mengi tuweze kuhifadhi na kutahitajika fedha kununua mahindi.”
“Tukiweza kuuza nje tutayahifadhi ambayo tutayanunua sasa hivi,” aliagiza Dk. Samia.
UJIO WA WAWEKEZAJI
Kwa upande wa madini, Dk. Samia alisema mkoa huo umepata wawekezaji 10 walioonesha utayari kuwekeza katika sekta ya madini, ambapo majadiliano yanaendelea.
Alisema pamoja na kujitokeza kwa wawekezaji hao, serikali itatengeneza mpango kuwaandaa wachimbaji wadogo washiriki katika shughuli hiyo.
Pia, alisema serikali inaangalia uwezekano kuanzisha kiwanda kikubwa cha kuchakata shaba ndani ya Rukwa.
“Bado tupo katika mazungumzo, wanaotaka kununua shaba ya Rukwa wamekuja kuangalia, tupo katika mazungumzo ndipo waweke kiwanda cha uchakataji, vijana wetu wapate ajira.
“Ndiyo maana tunajenga vyuo vya VETA vijana wafundishwe wakafanye kazi katika viwanda vya aina hii badala ya wageni kubeba dongo letu la shaba wakachakate kwao, wafanye hapa vijana wapate ajira,” alisisitiza.
Alitaja mkakati mwingine mkoani humo ni ujenzi wa kongani za viwanda ambavyo vitatumika kuchakata mazao na kuyaongeza thamani.
RUKWA IMEPIGA HATUA
Katika hotuba yake, Dk. Samia alisema Mkoa wa Rukwa umepiga hatua kubwa ya maendeleo, kwani mara ya kwanza alifika katika mkoa huo 1997 kufanya kazi na shirika lisilo la kiserikali liitwalo Rango.
Alieleza alikaa katika mkoa huo miezi mitatu akifanya utafiti kuhusu mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yaliyokuwepo mkoani Rukwa, ambapo kipindi hicho mkoa huo ulionekana kuwa nyuma kimaendeleo kutokana na kupitia wakati mgumu kupata hoteli.
“Nimekuja mara ya pili Rukwa katika kampeni za mwaka 2015 nikiwa mgombea mwenza, nikakuta mambo yamebadilika kidogo lakini siyo hivi. Baada ya kampeni nikarudi tena nikamkuta Mkuu wa Mkoa, Stella Manyanya.
“Tukawa na ile kaulimbiu Rukwa, ruka kwa maendeleo. Angalau mkoa ukaanza kufunguka na wakati ule ndipo nilipokusanya kero zote za Rukwa nikazibeba kwenda kuzifanyia kazi,” alieleza.
Dk. Samia alisema alirejea tena mkoani humo kwa ziara ya kikazi Julai, mwaka jana, kufungua na kuweka mawe ya msingi.
“Sasa hivi unatoka Dar es Salaam asubuhi Rukwa unaingia kwa wakati wako. Kama gari binafsi unafika mapema zaidi. Mambo makubwa yamefanyika.
Aliongeza: “Nilipokuja mwaka jana, kazi nilizozifanya niliweka mawe ya msingi katika shule ya wasichana ya sayansi. Shule ile sasa ipo tayari kuchukua wanafunzi.”
Dk. Samia alisema serikali imejenga shule maalumu za wasichana zenye mchepuo wa sayansi kuongeza idadi yao katika fani hizo.
Pia, alibainisha serikali imejenga shule maalumu ya wavulana wenye vipaji elimu ambazo zinajengwa maeneo mbalimbali nchini.
Alieleza shughuli ya pili aliyoifanya ni kuzindua chuo cha ualimu Sumbawanga ambacho ni miongoni mwa vyuo vya walimu 35 vya serikali.
Dk. Samia alisema lengo ni kuongeza idadi ya walimu ambao watasambazwa nchini hususan katika mikoa ya pembezoni.
Vilevile, alisema aliweka jiwe la msingi ujenzi wa kampasi ya Rukwa ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia eneo la Kayengesa ambako ujenzi upo katika hatua za mwisho kukamilika.
Aliongeza chuo hicho kitatoa fursa kwa vijana kupata ujuzi hatimaye taifa kuzalisha wanasayansi wengi katika fani za teknolojia.
“Wakati ule niliweka jiwe la msingi chuo cha VETA Sumbawanga ambacho kitakuwa chuo cha nne ndani ya mkoa huu. Tayari kimeshachukua wanafunzi na kinatoa huduma.
“Nilizindua jengo la huduma za dharura katika Hospitali ya Wilaya Nkasi ikiwa ni sehemu ya uwekezaji katika sekta ya afya mkoani hapa. Nimeona kila mashine inayohitajika zipo na ni mashine za kisasa,” aliongeza.
Pia, alisema aliweka jiwe la msingi katika uwanja wa ndege ambao tayari njia ya kurukia imeshakamilika na hatua inayoendelea ni ujenzi wa miundombinu mingine kuukamilisha.
WENJE KUJA NA ORODHA
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Ziwa Victoria, Ezekia Wenje, alisema atakuja na orodha ya watu kutoka nje ya nchi wanaoifadhili CHADEMA.
“Hakuna chama kilichobebwa na Dk. Samia kama CHADEMA na ndiyo maana aliwahi kuacha shughuli ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) akaenda ya Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA) amewahi kufanya hivyo kwa chama gani kingine?
“Leo CHADEMA hata kikitaka kufanya kazi popote wanapewa fedha na wanaharakati wapo nje ya nchi, ndiyo wanachanga fedha wapo katika mitandao huko.
Alisisitiza: “Yani chama kimesajiliwa hapa nchini halafu kinadhibitiwa na watu wa mitandao na ndiyo wanawafadhili kuwapa fedha, wakileta ‘pang’ang’a’ tutakuja na orodha ya hao watu wanaowapa hizo fedha,” alisema Wenje.
BASHE AFUNGUKA
Kwa upande wake, mgombea ubunge Jimbo la Nzega Mjini na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema wakati Dk. Samia anaingia madarakani matumizi ya mbolea nchini yalikuwa tani 350,000 huku ziada ya chakula ikiwa asilimia nne.
Alisema Dk. Samia alipochukua uongozi hatua aliyoianza ni kutatua changamoto ya gharama za pembejeo, ambapo kwa miaka minne zaidi ya sh. bilioni 700 zimetolewa kugharimia ruzuku kwa mazao ya chakula.
Bashe alisema mwaka jana hadi hivi sasa NFRA imenunua mazao ya wakulima kwa zaidi ya sh. bilioni 400 na kuutaka wakala huo kununua mahindi sh. 700 kwa kilo moja badala ya sh. 400 kwa bei ya soko.
“Kwa miaka miwili tuna ziada ya chakula zaidi ya tani milioni 5.7. Taifa hili likifunga mipaka yake lina uwezo wa kujilisha mwaka mmoja na miezi sita bila tatizo,” aliongeza.
ONGEZEKO LA MAKUSANYO
Mgombea Ubunge Jimbo la Iramba, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema Dk. Samia ametatua kero za wananchi.
Alisema kiongozi huyo alipoingia madarakani alikuta malalamiko kuhusu uhusiano mbaya katika ukadiriaji kodi na baadhi ya watu wakibambikiwa kodi.
Mwigulu alisema baada ya Dk. Samia ‘kushika usukani, amefuta kodi na tozo zaidi ya 250 kwa makundi ya wakulima, wafugaji na bodaboda.
Alieleza Dk. Samia amelipa madeni ya watoa huduma wakiwemo wakandarasi, kwani alielekeza madeni hayo yalipwe.
“Siyo hilo tu ukaelekeza kukomesha makadirio ya kodi yasiyostahiki, ulielekeza uhusiano bora wa kodi na hiyo ndiyo siri ya kuongezeka makusanyo kutoka sh. trilioni 1.3 wakati unaingia madarakani hadi sh. trilioni tatu kwa mwezi,” alisema.
WAGOMBEA UBUNGE
Mgombea ubunge Jimbo la Sumbawanga Mjini, Aeshi Hillary alisema Dk. Samia ametimiza ahadi ya ujenzi wa uwanja wa ndege kwa kutoa zaidi ya sh. bilioni 60.
Pia, alisema mwaka jana wakazi wa jimbo hilo waliomba upanuzi wa mradi wa maji uliohitaji sh. bilioni 2.5, hivyo Dk. Samia alitoa fedha hizo na mkandarasi ameanza kujenga bwawa la maji.
Kwa upande wa kilimo, Aeshy alisema kuanzia mwaka jana wakulima wameuza mahindi sh. 700 kwa kilo moja kupitia NFRA.
Vilevile, alieleza Dk. Samia ametoa fedha kujenga soko kubwa la kimataifa la mazao ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 80.
Alisema kukamilika soko hilo wanunuzi kutoka Zambia, Malawi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), watalitumia kununua mazao ya wakulima.
Kwa upande wake, mgombea ubunge Jimbo la Kwera, Deus Sangu, alieleza katika kipindi cha miaka minne, zaidi ya bilioni 300 zimetolewa katika Halmashauri ya Kwera ambazo zimetumika kujenga jengo la utawala, nyumba za watumishi, ujenzi wa shule mpya za sekondari 14 na tawi la Chuo Kikuu cha Sayansi Mbeya.
Sangu alisema jimbo hilo limepata shule ya wasichana ya vipaji maalumu ambayo itaongeza mwitikio wa elimu katika mkoa huo.
“Umetujengea shule shikizi saba, umetujengea hospitali ya wilaya Mto Wisa, magari manne ya wagonjwa na zahanati 23,” alieleza.
Akizungumzia maji, mgombea huyo alisema jimbo hilo limepokea zaidi ya sh. bilioni 10 kutekeleza miradi 11 ya maji.
Mgombea ubunge viti maalumu, Slyvia Sigula, alisema Dk. Samia ametoa fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo iliyofungua mkoa huo.
Alieleza dhamira, ahadi na msimamo wa wananchi wa Rukwa ni kuhakikisha Oktoba 29 wanakwenda kumpigia kura za kishindo.
Alieleza katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji katika mkoa huo, CCM ilishinda asilimia 99.
“Picha kamili inakuja Oktoba 29. Tunakwenda kukuheshimisha wananchi wa Rukwa kwani umetuongezea sababu za kukuchagua. Umetuongezea bei ya kuuza mahindi kutoka sh. 400 kwa kilo hadi sh. 700,” alisema.




