Na ABDUL DUNIA
LICHA ya kukiri mechi dhidi ya Silver Strikers ya Malawi itakuwa ngumu, Kocha wa Yanga, Romain Folz, amesema lengo lao ni kupata matokeo mazuri katika mtanange huo.
Yanga itachuana na Silver Strikers katika mechi ya hatua ya pili ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), utakaopigwa Oktoba 18, 2025, katika Uwanja wa Taifa wa Bingu uliopo Lilongwe, Malawi.
Yanga ilianza michuano hiyo kwa ushindi wa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Wiliete de Benguela ya Angola kabla ya kushinda 2-0 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Silver Strikers ilitinga hatua hiyo kwa kuitoa Elgeco Plus ya Madagascar kwa faida ya bao la ugenini.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Mauritius, Silver Strikers ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya mwenyeji kabla ya kutoka suluhu katika dimba la Bingu nchini Malawi.
Akizungumzia mchezo huo, Folz alisema anaiandaa vyema timu yake kuhakikisha inapata matokeo mazuri licha ya mechi hiyo kuwa ngumu.
“Tunafanya kila linalowezekana kujiandaa vyema kuwakabili wapinzani wetu, ni ligi ya mabingwa hivyo kila timu ina ubora na kama isingekuwa hivyo basi timu kama hizo zisingekuwepo.
(Silver Strikers) Ni timu nzuri lakini tumefanya uchambuzi kuhusu wao, tunawaheshimu lakini hatimaye matokeo mazuri ndiyo kitu tunachotaka kupata,” alisema.
Mshindi wa jumla wa mechi mbili za hatua hiyo ndiyo itatinga hatua ya makundi ya CAFCL msimu huu.
Timu zinazoshiriki hatua za awali katika Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) zitavuna dola za Marekani 100,000 ambazo ni zaidi ya sh. milioni 244 za Tanzania.
Katika CAFCL, timu zitakazotinga hatua ya makundi zitakuwa na uhakika wa kuvuna dola za Marekani 700,000 ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 1.7 za Tanzania.
Timu zitakazotinga robo fainali, kila moja itakuwa na uhakika wa kuvuna dola za Marekani 900,000 ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 2.2 wakati zitakazoishia nusu fainali zikivuna dola za Marekani milioni 1.2 ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 2.9 za Tanzania.
Bingwa wa CAFCL msimu huu, anatarajiwa kuondoka na dola za Marekani milioni 4 ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 9.7 za Tanzania wakati mshindi wa pili ikiondoka na dola za Marekani milioni 2 ambazo ni zaidi ya sh. bilioni 4.9 za Tanzania.




