Na NASRA KITANA
WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imesimama kupisha mechi za kirafiki za kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), timu za Simba na Yanga zimeweka wazi kwamba zinaendelea na kazi ya maandalizi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga itakuwa ugenini dhidi ya Mashujaa FC, Juni 13, mwaka huu huku Simba wakibaki nyumbani kupambana na Pamba Jiji Juni 14, mwaka huu katika mchezo wa mzunguko wa 26 wa ligi hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema baada ya mapumziko mafupi kikosi chao kitaendelea na maandalizi kwa ajili ya mechi tano zilizobakia.
“Wale wachezaji wetu abao hawakuitwa katika timu za taifa, wataingia kambini Juni Mosi, mwaka huu kwa ajili ya maandalizi ya mechi zilizobakia, na baada ya hapo watakuja kuungana na wale walioitwa katika kikosi cha taifa ili kuendeleza programu ya mwalimu wetu,” alisema.
Kamwe alifafanua kuwa wanaendelea kujiandaa na mchezo dhidi ya Mashujaa wakijua ni mchezo mgumu na wenye changamoto kubwa.
Aliongeza kuwa mechi tano za mwisho, zinahitaji maandalizi ya kutosha kuhakikisha wanapata ushindi na kutetea ubingwa wao.
Naye Meneja wa Habari na Mawasilino Simba, Ahmed Ally alisema kocha wao, Steve Barker amewapa mapumziko wachezaji wao.
Ahmed alisema wanajua mechi za mwisho wa msimu zinakuwa ngumu na zenye changamoto kubwa lakini hawatakubali kupoteza mchezo wowote ule.
“Unajua mechi za mwisho wa msimu zinakuwa ngumu na zenye changamoto kubwa lakini anaimani wachezaji wetu watapambana mwanzo mwisho ili kupata pointi tatu katika kila mchezo,” alisema Ahmed.
Alisema kuanzia Juni mosi, timu itaanza kufanya maandalizi katika mchezo wake dhidi ya Pamba Jiji.
Katika msimamo wa ligi, Yanga inaongoza ikiwa na pointi 60 huku Simba ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi 58 baada ya wote kushuka dimbani mara 25.
Timu hizo zimebakiza mechi tano ili kumaliza ligi kuu msimu huu, Yanga ikibakiwa na mchezo dhidi ya Mashujaa FC, Fountain Gate FC, Azam FC, TRA United na JKT Tanzania.
Kwa upande wa Simba imebakiwa na michezo dhidi ya Pamba Jiji, Mbeya City, Mtibwa Sugar, Singida Black Stars na KMC.




