Na MWANDISHI MAALUMU, Moscow
TANZANIA na Russia, zimepongeza ukuaji wa biashara kati ya nchi hizo ambao umefikia asilimia 72 katika kipindi cha mitano kuanzia mwaka 2020 hadi 2025.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, aliandika kwamba, pamoja na mambo mengine, katika siku ya kwanza ya ziara yake nchini Russia, amepata heshima ya kukutana na Rais Vladimir Putin, jijini Moscow.
Rais Samia, alisema kwa kuzingatia historia kubwa ya ushirikiano na uhusiano wa kirafiki kati ya Tanzania na Russia, wamekubaliana kuongeza juhudi za kukuza biashara na uwekezaji kwa lengo la kuleta manufaa makubwa zaidi ya kiuchumi na ustawi wa wananchi wa nchi hizo.
Pia, alisema ukuzaji biashara na uwekezaji huo, utafungua fursa zaidi kwa wananchi na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Tumejadiliana namna ya kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za kimkakati, zikiwemo sayansi na teknolojia, elimu, nishati, madini, kilimo, miundombinu na utalii,” aliandika Rais Samia.
Mapema, Rais Samia, aliishukuru Serikali ya Russia kuwa mshirika wa muda mrefu wa maendeleo na kwamba, bado inaendelea kutoa mchango mkubwa.
Alitoa kauli hiyo jana, alipozungumza na Rais Putin, Ikulu ya Kremlin, jijini Moscow.
Rais Samia, alisema ziara yake nchini humo ni ya kihistoria kwake binafsi na taifa, kwa sababu umepita muda mrefu tangu ziara ya mwisho ya kiserikali nchini humo, ilipofanywa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1969.
“Kwangu ni ziara ya kihistoria ya kupata hii nafasi ya kujadili ushirikiano wa pande mbili na maendeleo endelevu ya wananchi wa Tanzania, kwa niaba yangu binafsi na wananchi wa Tanzania, natoa shukrani zetu za dhati kwa mwaliko huu.
“Kama ulivyosema kwa usahihi, hii ni fursa ambapo tunaweza kupata muda wa kujadili maendeleo yajayo ya nchi zetu, lakini kabla ya hilo, ni lazima kuishukuru Russia kwa mchango wake mkubwa iliotoa wakati wa harakati za ukombozi wa Afrika katika miaka ya 1960,”alisema
Pia, alimpongeza Rais Putin kwa kusherekea kumbukizi za miaka 81 ya ushindi wa kijeshi wa Shirikisho la Jumuiya ya Kisovieti katika vita kuu ya pili ya dunia, ambayo ilifanyika Mei 9, mwaka huu na kwamba, sherehe hiyo ni kumbukumbu ya uzalendo, kujitolea na mshikamano wa wananchi wa Urusi.
“Leo asubuhi (jana), nilikuwa na heshima ya kuweka shada la maua katika kaburi la mashujaa wa vita, ni fahari kubwa kwangu na kwa taifa langu. Tunashukuru kwa heshima hii,”alisema.
KAULI YA PUTIN
Kwa upande wake, Rais Putin, alisema kwamba, ni jambo la kufurahisha baada ya kuteuliwa kwa muhula wake wa kwanza, Rais Dk. Samia, aliamua kufanya ziara ya kwanza ya kiserikali nchini Russia.
“Hii ni ishara nzuri kwamba, kwa miaka yote, ukiwa Waziri na kisha Makamu wa Rais, umekuwa ukizingatia kuendeleza uhusiano wetu, mwaka jana, biashara kati ya nchi zetu ilikua kwa asilimia 20 hadi 25, jambo linaloashiria ukuaji mzuri wa ushirikiano wetu,” alisema.
Alisema kuna fursa nyingi za kushirikiana, ikiwemo katika maeneo ya nishati, uchunguzi wa kijiolojia, usafirishaji, afya na elimu.
“Kesho (leo) utapewa shahada ya heshima ya udaktari na Chuo Kikuu cha Urafiki wa watu wa Russia nakutakia hongera kwa heshima hiyo.
“Kesho pia nimeambiwa utahudhuria Jukwaa la 29 la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF 2026), tunatarajia nchi yako itashiriki kwa kiwango kikubwa,”alisema.
Rais Dk. Samia atatunukiwa shahada hiyo na chuo hicho kwa kutambua uongozi wake, mageuzi katika sekta ya elimu na juhudi zake za kuimarisha diplomasia ya Tanzania.
Pia, kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha hadhi ya Tanzania kimataifa ikiwemo ya kupitia sekta ya utalii.
Rais Dk. Samia yupo nchini Russia kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kwa mwaliko wa Rais Putin.



