Na MWANDISHI WETU
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema kabla ya kuanza mchakato wa maridhiano ya kisiasa, ni vyema kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria kupitia vyombo vya haki, watu waliohusika na vurugu zilizosababisha madhara vikiwemo vifo wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
Amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuunda Tume ya Kuchunguza Vurugu zilizotokea kwa lengo la kufahamu kiini cha tatizo hilo.
Wasira alieleza hayo mwishoni mwa wiki, alipohutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Kigoma mjini akiwa katika ziara ya Kichama mkoani humo.
“Sijasema jina la mtu, wenye kujua hayo mambo wanajijua, waache jinai ichunguzwe kama walihusika, waende katika vyombo vya haki na siyo wengi, wanaobaki watu wema tukae tufanye nao maridhiano,” alisema.
Wasira alimpongeza Rais Dk.Samia kwa kuunda tume ya kusaidia kujua chanzo cha vurugu hizo, huku akitumia nafasi hiyo kuipongeza kazi nzuri iliyofanywa na tume hiyo.
“Rais (Dk. Samia) tunamshukuru na kumpongeza kwa kuunda tume ya kutusaidia kujua chanzo.
Tunampongeza na tunaipongeza tume ambayo imesema katika uchunguzi wake, imegundua kuna watu siyo wengi, lakini ndiyo walioanza mpango ule walifadhili.
“Hivi sasa wanasema (tume) wao hawakuwa polisi wa kuwakamata, wanasema tuchunguze wale walioonekana, tusiwe tunafuga nyoka ndani ya nyumba,” alisema na kuongeza kuwa, hakuna anayeshabikia matukio yenye kuumiza yaliyosababisha vifo na kwamba, anayefanya hivyo hayuko sawa kiakili.
“Wanasema watu wamekufa, ni nani anafurahia kufa watu labda uwe na wewe akili yako imeharibika kama unasherehekea kufa watu.
Wote tunapinga mauaji, nani amesababisha, halafu wale walioko wengine kama tunawahisihisi ndiyo tena wanataka kutufundisha namna ya kufanya…vurugu muanzishe nyie na namna ya kumaliza mgogoro mtupe nyie, hapana.”alisema.
Kwa mujibu wa Wasira, pamoja na kutofautiana kimawazo, huenda wapo watu wema ambao watakaa meza moja na kujadiliana mustakbali mwema.
“Mnaweza kuwa mnatofautiana mawazo, lakini ni watu wema tu, kutofautiana mawazo siyo mbaya, ni jambo la kawaid tu, hamuwezi kusema wote mtakuwa mnakubaliana, hata kondoo hawakubaliani mwingine anatangulia mbele mwingine nyuma.
“Hivyo wengi wanakubaliana maridhiano yafanyike baada ya waovu kupatikana,” alieleza.
VYAMA VINGI SIYO UHASAMA
Makamu Mwenyekiti Wasira, alisema Watanzania walikubaliana kuingia katika mfumo wa vyama na usiwe chanzo cha vurugu.
“Viko vyama vingi na tulikubaliana viwepo, hatukukubaliana mfumo wa vyama vingi uwe chanzo cha mgogoro katika nchi yetu, kama wewe una chama na unadhani amani siyo kitu cha maana umekosea, sisi tunataka amani,” alisisitiza.
Alifafanua kuwa, Mkoa wa Kigoma ni shuhuda wa madhara ya kutoweka amani kwa kuwa, umewahi kupokea wakimbizi waliozikimbia nchi zao kutokana na machafuko.
“Sisi wa Kigoma siyo watu wa kufundishwa gharama ya amani, ninyi mmeishi mahali ambapo amani hakuna, ninyi mmekuwa wenyeji wa watu waliokimbia fujo wameishi hapa na kuwatoa hapa ikawa shughuli, maana wanaona sasa amani hii tuiache, tumwachie nani mpaka ikabidi kushauriana nao.
“Nchi zote zinazozunguka hapa zimewahi kuleta wakimbizi Kigoma, sasa ninyi mnataka fujo mtakimbilia wapi, mnaijua safari ya sisimizi huwa wanaenda na huku wanarudi sasa haijulikani wanakokwenda.
“Sisi hapa tumepokea wakimbizi kwa maelfu sasa watu wanavuruga amani eti wanasema kuvuruga amani ndilo jibu la haki…”alikumbusha Wasira.
Aprili 23, mwaka huu, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alipokea ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Ghasia na Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman.
Akipokea ripoti hiyo, Ikulu, Dar e Salaam, Rais Dk. Samia, alisema tukio hilo linaashiria mwanzo wa hatua ya utekelezaji wa mapendekezo ya kuponya taifa, kuimarisha uwajibikaji na kujenga mustakabali imara zaidi.
Rais Samia, alisema anatambua kwa uzito mkubwa madhara yaliyolikumba taifa, akipokea maelezo kuwa, matukio hayo yalisababisha vifo vya takribani watu 518, majeruhi zaidi ya 2,390 na uharibifu wa mali unaokadiriwa kufikia zaidi ya sh. bilioni 125.
Alisisitiza kuwa, hasara hizo zimeacha majeraha makubwa ya kijamii, kiuchumi na kisaikolojia kwa wananchi.
“Hili ni janga na doa kubwa kwa Taifa letu,” alisema.




