Na NASRA KITANA
WAKATI kikosi cha Simba kikitarajiwa kuondoka nchini leo, kocha wa timu hiyo Dimitar Pantev amesema ana furaha na nyota wake baada ya kupata ushindi katika mechi mbili za kirafiki.
Pantev ametoa kauli hiyo Dar es Salaam, baada ya timu yake kuibuka na ushindi dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan kwa kuifunga mchezo wa kwanza mabao 2-1 kabla ya juzi kupata ushindi wa mabao 4-1, michezo hiyo ilipigwa katika Uwanja wa Gymkhana.
“Ushindi ambao tumeupata katika mechi zetu mbili za kirafiki dhidi ya Al Hilal, umetuongezea morari ya kutosha kuhakikisha tunapata ushindi tukiwa ugenini katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kumalizia nyumbani,”alitamba kocha huyo.
Pantev alisema Simba imejipanga vizuri kushinda mchezo wake wa kwanza wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nsingizini Hotspurs utakaochezwa Jumapili, wiki hii nchini Eswatin.
Mechi hiyo ya raundi ya kwanza inatarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa Uwanja wa Somhlolo, uliopo Lobamba nchini humo saa 10:00 jioni.
“Nimepata taswira ya jinsi gani ya kukitengeneza kikosi hicho hasa kuelekea katika mchezo huu wa Kimataifa.
“Ukweli mechi hizo zimewapa morari ya kutosha wachezaji wangu kuhakikisha tunashinda mchezo dhidi ya Nsingizini, nina imani tutafanya vizuri,”alisema.
Hata hivyo, Pantev alisema hivi sasa hawezi kubadilisha kila kitu kwa wakati mmoja, lakini anahitaji timu inayocheza kwa mpangilio, kushambulia na kulinda kwa pamoja, kitu ambacho amesema amekiona wachezaji wake wanakifanya.
“Nilipokuwa najiunga na Simba, niliomba mechi za kirafiki za kimataifa, kuona namna gani timu inacheza, hivyo mechi hizo mbili ni kwa ajili ya kujenga maelewano ya kimbinu.
“Tunahitaji kuwa na timu inayocheza kwa mpangilio, inayoshambulia kwa hesabu na kujilinda kwa pamoja, hizi ndizo mechi zinazoniwezesha kuona nani yuko tayari kupigania nembo ya Simba, ” alisema kocha huyo.
Alisema pamoja na kwamba kikosi chake kinacheza bila baadhi ya wachezaji ambao wapo katika vikosi vya timu za taifa, lakini waliobaki wanakuwa tayari kiakili na kimwili ili wakirejea iwe rahisi kwake kuunganisha mfumo.




