Na NASRA KITANA
SIKU moja baada ya kutwaa Kombe la Mapinduzi 2026, Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, amefurahia kiwango cha timu yake na anaamini michuano hiyo itakuwa chachu ya kuendelea kutikisa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano mingine.
Yanga ilibeba taji la Mapinduzi juzi baada ya kushinda kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya dakika 120 kumalizika kwa suluhu katika fainali iliyopigwa Uwanja wa Gombani, Pemba.
Baada ya michuano hiyo, sasa Yanga itajipanga kwa mechi za Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) zinazotarajiwa kuchezwa hivi karibuni.
Akizungumza kutoka Pemba, Pedro raia wa Ureno, alisema michuano hiyo ilikuwa na ushindani mkubwa na itakuwa chachu ya kikosi chake kuwa imara zaidi msimu huu.
Alisema fainali ilikuwa bora kutokana na wapinzani wake kuonyesha ushindani wa hali ya juu, itawasaidia kufanya vizuri katika mechi zake za kimataifa.
Pedro alisema bado ana kazi ya kufanya hasa katika eneo ya ushambuliaji wachezaji wake watumie vyema nafasi wanazozipata.
“Tumechukua ubingwa wa Mapinduzi ni jambo zuri kwetu kwani ndiyo malengo tuliyojiwekea katika kombe hili, lakini pia (michuano hii) imetupa fursa ya maandalizi mazuri hasa katika mechi zetu zijazo,” alisema.
Kocha huyo alisema atakwenda kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo huo kufanya vizuri na kushinda kwa magoli mengi katika michezo ijayo.
Naye beki wa timu hiyo, Dikson Job alisema mechi hiyo ilikuwa ngumu lakini anafurahi kuona wakitimiza lengo la kubeba taji.
“Mwisho wa mashindano haya ndiyo mwanzo wa mashindano mengine, hivyo tunajipanga kupambana na kufikia malengo ya timu,” alisema.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ipo kundi B na timu za Al Ahly ya Misri, AS Far ya Morocco na JS Kabylie ya Algeria.
Yanga wiki ijayo itachuana na Al Ahly nchini Misri kabla ya Januari 30 kurudiana katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.




