Na MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesisitiza maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kuanza mara moja.
Makonda ametoa kauli hiyo ikiwa bado michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 inaendelea nchini Morocco, ambapo fainali inatarajiwa kupigwa Jumapili hii.
AFCON 2027 itafanyika katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Akizungumza jijini Dodoma, Makonda alisema ni muhimu kuanzishwa kwa mashindano ya michezo katika shule zote za msingi na sekondari nchini kama sehemu ya shamrashamra za mashindano ya AFCON 2027.
Alisema mashindano ya shamra shamra za AFCON, yataongeza hamasa na morali kwa Watanzania kuipenda na kuishangilia timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, huku yakichochea matokeo chanya na kuibua vipaji vipya vya michezo miongoni mwa vijana.
“Mashindano ya shule hizo yataongeza hamasa na morali kwa Watanzania kuipenda na kuishangilia ‘Taifa Stars’,” alisema.
Pia, Makonda aliitaka wizara hiyo kuandaa programu maalumu itakayowawezesha walimu wa shule za msingi na sekondari wenye mapenzi na michezo, kupata mafunzo ya kitaalamu, ili wahitimu vyuoni wakiwa na uwezo wa kugundua, kukuza na kuongoza vipaji vya watoto katika sekta ya michezo.
Wakati huo huo, Makonda alisema kuelekea katika mwezi mtukufu wa Ramadhani unaotarajiwa kuanza mwezi ujao, atahakikisha michuano ya Ramadhani Cup inafanyika katika mikoa mitano.
“Tunakwenda katika mwezi wa Ramadhani, kwa miaka mingi Dar es Salaam kunakuwa na Ramadhani Cup, hivyo nimeshaongea na viongozi wa mashindano hayo kuhakikisha michuano hiyo hivi sasa itapelekwa katika mikoa mitano,” alisema Makonda.
Waziri huyo alisema watahakikisha wanatumia fursa hiyo michezo iwaunganishe watu kwa pamoja na kuleta maendeleo nchini.
Katika AFCON 2025, Taifa Stars iliishia hatua ya 16 bora baada ya kufungwa bao 1-0 dhidi ya mwenyeji Morocco.




