Na FRED ALFRED
Dodoma
WAZIRI Mkuu, Mwigulu Nchemba, ameipongeza timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, Serengeti Boys, kwa kuiheshimisha Tanzania katika ulimwengu wa soka, huku akisema si muda mrefu taifa litashuhudia Kombe la Afrika likitua nchini.
Dk. Mwigulu alitoa pongezi hizo bungeni jijini Dodoma kabla ya kuanza kujibu maswali ya papo kwa papo.
Alisema mafanikio ya Serengeti Boys yanaonyesha mchezo wa soka umepiga hatua.
“Niwapongeze vijana wetu wa Serengeti Boys kwa hatua kubwa na yenye heshima waliyofikia katika mashindano ya vijana chini ya miaka 17, kwa kucheza hatua ya fainali yenye ushindani mkubwa na kukosa bahati ya kuleta kombe.
“Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kuwa si muda mrefu Kombe la Afrika litatua hapa nchini, kwa sababu mwelekeo tulionao ni sahihi na tupo vizuri. Mambo makubwa yanakuja,” alisema Waziri Mkuu.
Aidha, Waziri Mkuu alisema hatua zilizofikiwa na klabu za Simba na Yanga katika michuano mikubwa ya klabu barani Afrika ni ishara kuwa soka la Tanzania linaendelea kupiga hatua na lina uwezo wa kutwaa mojawapo ya mataji ya Afrika katika siku zijazo.
Serengeti Boys, Jumanne usiku ilishika nafasi ya pili katika fainali za AFCON U 17, baada ya kufungwa mikwaju ya penalti 4-2 dhidi ya Senegal katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Moulay El Hassan, Rabat, Morocco.
Serengeti Boys ilianza michuano hiyo kwa kuifunga Msumbiji mabao 3-0, iliichapa Angola 3-0, ilipoteza mbele ya Mali kwa mabao 2-1, ikaitandika Algeria penalti 4-3 kabla ya kuirarua Misri kwa penalti 4-3.
Kwa mara ya kwanza Serengeti Boys ilishiriki michuano hiyo mwaka 2017 nchini Gabon kabla ya kucheza tena 2019 katika fainali zilizofanyika Tanzania ambapo timu hiyo ilitolewa hatua ya makundi.




