Na NJUMAI NGOTA,
Ruvuma
MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amewahakikishia wananchi mkoani Ruvuma, hatawaangusha katika kumsaidia Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025-2030, iwapo Chama kitachaguliwa tena kuiongoza nchi.
Dk. Nchimbi alisema hayo Uwanja wa Shule ya Msingi Lituhi, wilayani Nyasa, mkoani Ruvuma, alipohutubia mamia ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Alisema dhamira yake kuu ni kuhakikisha anakuwa msaidizi madhubuti wa Dk. Samia kwa kutekeleza kiufanisi kila ahadi iliyowekwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
“Nitumie nafasi hii kuwahakikishia wazee wetu wa Nyasa na ndugu zangu wa Nyasa nitafanya kila jitihada kumsaidia Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutekeleza Ilani ya Chama chetu.
“Pia, nitafanya kila jitihada kuhakikisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, anaona kuchukua mtu kutoka Ruvuma anaweza kuwa msaada kwake.
“Nitafanya kila jitihada sitawaangusha, kwa vyovyote itakavyokuwa nikimpa Rais wetu msaada, nikishindwa kumsaidia kwa uaminifu, nitakuwa nimewaangusha watu wa Ruvuma. Nitakuwa nimewaangusha watu wa kusini,” alisema.
Dk. Nchimbi aliwahakikishia watu wa mkoa huo atajitahidi na hatawaangusha katika kumsaidia Rais Dk. Samia, ambaye ni Mgombea Urais wa CCM.
Akimzungumzia Dk. Samia, Balozi Nchimbi alisema ana rekodi ya kutekeleza ahadi zake na amefanya mageuzi makubwa katika sekta ya afya, elimu, miundombinu, kilimo, ufugaji na hakuna eneo ambalo hajaleta mapinduzi makubwa.
“Ndiyo maana mabadiliko na mafanikio ambayo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameleta kwa nchi yetu katika miaka minne na nusu, kila mtu anashangaa,” alisema.
Kuhusu vipaumbele vinatarajiwa kutekelezwa wilayani Nyasa katika miaka mitano ijayo iwapo Chama kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi, Dk. Nchimbi aliahidi kuiboresha Hospitali ya Wilaya ya Nyasa kwa kuongeza majengo, vifaa na madaktari.
Pia, ujenzi wa zahanati mpya 10, vituo vya afya sita likiwemo ombi la Kituo cha Afya cha Lituhi ambacho kiliwahi kuombwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Nyasa, marehemu John Komba ambacho kitakuwa miongoni mwa vituo hivyo.
ELIMU
Dk. Nchimbi aliahidi ujenzi wa shule mpya tisa za msingi, sekondari sita, madarasa 210 maabara mpya 18 katika shule za sekondari.
UMEME
Dk. Nchimbi alieleza dhamira ni kuhakikisha vitongoji vyote vya wilaya hiyo vinafikiwa na nishati ya umeme.
MAJI
Mgombea Mwenza wa Urais alitaja miradi inayolenga kuongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 68 hadi asilimia 90, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mradi wa Luhangarasi, Ruhindo, ukarabati wa mradi wa Lundo-Nkindo-Ng’ombo, Ng’ombo-Kilosa-Ndegele-Songambele na visima virefu katika vijiji visivyo na maji ya kutosha.
Pia, kufunga machujio ya maji kuhakikisha ubora wa maji safi na salama, kufunga machujio ya kusafisha maji katika maeneo yote.
Dk. Nchimbi alisema wataongeza mtandao wa maji maeneo ambayo hayajafika kwa kuhakikisha yanapata maji safi na salama
Aidha, katika barabara, Dk. Nchimbi aliahidi ujenzi wa madaraja, barabara za lami na za changarawe pamoja kujenga stendi ya kisasa pale Kilosa.
Dk. Nchimbi alitoa wito kwa wananchi wote wa Nyasa kuhifadhi vitambulisho vya kupiga kura, visipotee na asikosekana hata mtu mmoja kwenda kupiga kura.
“Watu watakapokuwa wakisikiliza matokeo. Moja ya maeneo ambayo taifa zima litafuatilia kujua kura zilizopigwa ni Nyasa. Watu wanataka kujua kama watu wa Nyasa wamejitokeza kupiga kura. Na kama Nyasa, Rais Samia ameongoza kuliko maeneo mengine yote, mtoke kwa wingi Ruvuma itikise nchi, akiuliza mkoa gani unaongoza waseme Ruvuma haijapata kutokea,”alisema.
Dk. Nchimbi alitumia fursa hiyo kuwashukuru wazee wa Nyasa na wa kimila kwa heshima waliyompa. Balozi huyo baada ya kuwasili Lituhi, alipewa baraka kutoka nyumbani kwao kwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa urais, ambapo kazi hiyo iliongozwa na Katibu wa Machifu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Wabu aliyemkabidhi zana za kijadi.




