Na NJUMAI NGOTA, Lindi
MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ameahidi kukamilisha Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, iwapo Chama kitapewa ridhaa ya kuongoza tena nchi katika miaka mitano ijayo.
Dk. Nchimbi aliyasema hayo Kata ya Tingi, Jimbo la Kilwa Kaskazini, mkoani Lindi, katika mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Alibainisha kukamilika bandari hiyo ni sehemu ya vipaumbele vya CCM katika kuendeleza sekta ya uvuvi.
Kwa mujibu wa Dk. Nchimbi, katika miaka mitano ijayo wamedhamiria kujenga soko la kisasa la samaki, majokofu ya kuhifadhia na chanja za kisasa za kukausha samaki wawe na ubora.
“Pia, tunakwenda kutoa mafunzo kwa wavuvi wetu wavue kitaalamu na wafanye biashara yao kwa tija, ndani ya miaka mitano ijayo tunakwenda kuhakikisha zana za uvuvi zinapatikana kwa urahisi,” amesema.
Ameeleza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika miaka minne na nusu ya uongozi wake, katika eneo la uvuvi amefanya kazi kubwa kwa kupandisha bajeti zaidi ya mara sita lengo likiwa ni kuijenga sekta hiyo.
“Hapa Lindi imejengwa bandari ya kipekee ya uvuvi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 280, gati limekamilika, kituo cha barafu pamoja na sehemu ya kuhifadhi samaki.
“Inahitaji ujasiri wa mwenda wazimu kutompa kura Dk. Samia kwa hayo aliyoyafanya,” amesema.
Dk. Nchimbi amesema Dk. Samia ameipa heshima kubwa CCM na wanawake wa Tanzania kwa ujumla.
Akieleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, Dk. Nchimbi alitaja maeneo ya kilimo, uvuvi na miundombinu yamepewa msukumo mkubwa.
Amesema upatikanaji wa mbolea ya salfa bure umechochea kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa korosho, ambapo Mkoa wa Lindi umeongeza uzalishaji kutoka tani 30,000 miaka minne iliyopita hadi kufikia tani 92,000 msimu uliopita.
“Hivi sasa, kati ya kila kilo 100 za korosho zinazozalishwa nchini, kilo 15 hadi 20 zinatoka Lindi. Ukitaja wakulima wa korosho bila kuitaja Lindi, una matatizo ya akili,” alisema.
Amesema CCM imelenga kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuendelea na ruzuku ya mbolea, kusambaza miche bora ya korosho, kujenga maghala ya kuhifadhia nafaka, kuimarisha mashamba darasa na kuboresha miundombinu ya umwagiliaji.
Kwa upande wa biashara na uwekezaji, Dk. Nchimbi alisema serikali ya CCM imepanga kujenga masoko matatu ya wamachinga, stendi ya mabasi pamoja na maegesho ya malori kuchochea uchumi wa Kilwa.
KILWA
Dk. Nchimbi amesema Kilwa ni eneo linalofahamika dunia nzima tangu enzi za biashara ya utumwa katika karne ya tisa hadi ya 14 kwa kufanyika biashara za pembe na dhahabu.
“Amekuwepo Balozi Ali Mchumo. Pia, alikuwepo mzee wetu Kingunge Ngombale Mwiru ambao wote hao wamejenga historia kubwa ya Kilwa na kufanya ifahamike kitaifa na watu wote wajue Kilwa kuna watu wa maana,”amesema.
Amesema taarifa zilizopo zinaonesha Kilwa ni sehemu inayochangia uchumi wa nchi, ambapo zaidi ya asilimia 55 ya wakazi wake wanajihusisha na kilimo na asilimia 20 ni wavuvi na wengine wanafanya biashara ndogondogo.
Katika mkutano huo, Dk. Nchimbi amemwombea kura Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia, wagombea ubunge na madiwani. Naye, mgombea udiwani wa Kata ya Tingi kwa tiketi ya CCM, Rajab Katanga, alipongeza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wa Rais Dk. Samia na kuwaomba wananchi wa Kilwa kumpigia kura pamoja na wagombea wote wa CCM.




