Na MUSSA YUSUPH,
Tanga
MTUPE kazi, tukafanye kazi. Huo ndiyo msisitizo wa Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Samia Suluhu Hassan akiwaomba kura maelfu ya wananchi waliofurika katika mkutano wa kampeni Jijini Tanga.
Katika mkutano huo uliofanyika katika Uwanja vya Usagara jana, Dk. Samia, alisema endapo akipewa ridhaa ya kuliongoza Taifa, amedhamiria kurejesha hadhi ya mkoa huo kuwa wa viwanda.
Alisema katika kuthibitisha hilo, Dk. Samia alitangaza mikakati kujenga reli ya kisasa yenye urefu wa kilometa 1,108 kutoka Tanga – Arusha hadi Musoma ambayo itaunganishwa na Bandari ya Tanga.
“Tutaanza utekelezaji mradi wa reli kuunganisha Bandari ya Tanga kuelekea Arusha hadi Musoma takriban kilometa 1,108. Reli hii, itafungua maeneo ya viwanda na madini hivyo kuongeza fursa za ajira ndani ya Mkoa wa Tanga,”alisema.
Alisema reli hiyo ni sehemu ya mpango wa uboreshaji wa Bandari ya Tanga kuwa eneo maalumu la bohari ya mafuta na gesi.
“Bandari ya Tanga, inakwenda na maamuzi tuliyoyafanya kuwa Tanga ni bohari ya mafuta na gesi, hilo litachangia kuzalisha ajira nyingine 2,100. Hili linakwenda kunyanyua uchumi wa wana Tanga.
“Mbali na mradi huu, tunao mwingine wa kimkakati, unaofungamana na bandari hii. Mojawapo ni bomba la mafuta kutoka Hoima hadi Chongoleani.
“Mradi ambao umekamilika kwa asilimia 84 na umeleta manufaa mengi sana kwa mfano tayari eneo la Chongoleani pekee watu 1,300 wameajiriwa na ndani ya Wilaya ya Tanga watu 2,000 wameajiriwa,”alisema.
Mbali na ujenzi huo, alisema serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) zitashirikiana kujenga barabara ya Handeni – Singida.
Pia, alisema serikali itafanya upanuzi na ukarabati mkubwa wa barabara ya Dar es Salaam – Chalinze – Segera – Arusha.
Alieleza katika kuongeza kasi ya ujenzi wa viwanda, serikali imevutia wawekezaji watakaojenga kiwanda cha kuunganisha magari ya wagonjwa.
“Mtupe kazi, tukafanye kazi tujenge utu wa Mtanzania. Tujenge utu wa mwana Tanga kwa sababu ukiimarisha huduma ya maji, afya, elimu, umeme unaimarisha utu wa Mtanzania.
“Tunawaomba mchague Chama Cha Mapinduzi ili mfanyekazi, tuimarishe na tujenge utu wa Mtanzania,” alisisitiza.
AUNGURUMA PANGANI
Akiwa wilayani Pangani, Dk. Samia, alisema Februari, mwaka huu, alifika Pangani kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Mto Pangani na barabara ya Bagamoyo – Saadani – Pangani – Tanga.
Alieleza kuwa, kwa muda mrefu, wananchi wamesubiri barabara hiyo ambayo itawaondolea adha ya kulazimika kusafiri masafa marefu kwa kukosa muunganiko kati ya Wilaya za Bagamoyo na Pangani.
“Barabara hii, inaendelea vizuri na itakwenda kufungua ukanda wa Pwani kiuchumi na kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji.
“Kwa wale ambao hawajapata fursa ya kusoma Ilani naomba nigusie kwamba tunapoanza na barabara hii kwa kipande cha Tanga – Pangani kilometa 50 ujenzi umefikia asilimia 75,” alieleza.
Alisema kwa kipande cha Pangani – Saadani – Makurunge chenye kilometa 95, ujenzi umefikia asilimia 50 huku daraja la Mto Pangani lenye mita 525 na barabara unganishi imefikia asilimia 60.
Dk. Samia alisema ahadi ya CCM kwa wananchi wa Pangani ni kuikamilisha barabara hiyo ambapo siyo muda mrefu wananchi wataanza kufaidi matunda.
Kwa upande wa uvuvi, alisema serikali imewezesha upatikanaji wa boti 15 zinazosafiri umbali mrefu baharini kwa shughuli za uvuvi wa dagaa na samaki.
“Ninakumbuka nilizindua mradi huu wenye thamani ya sh. bilioni 1.6 ambao utaongeza fursa za ajira kwa vijana wetu. Pia, tumeanza ujenzi wa soko la samaki la kimataifa Kata ya Kipumbwi.
“Mradi huo wa sh. bilioni 1.3 utakuwa na vifaa vya kukaushia dagaa ni muhimu katika kuwaongezea kipato wavuvi na kuchochea maendeleo ya wilaya yetu,”alisema.
Alisema katika awamu ijayo, serikali itaendelea kuwashika mkono wavuvi ili kuongeza vipato vyao.
Kuhusu wafugaji, alieleza kuwa serikali itaendelea kuleta mageuzi sekta ya ufugaji kuwa ya kisasa.
Alisema kwa Pangani serikali imetoa ng’ombe wa maziwa 51 huku kitaifa ikitoa ruzuku ya chanjo bure kwa kuku na nusu bei kwa mifugo mingine.
Pia, alisema kwa upande wa kilimo ahadi yake ni kuendeleza programu ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT) ya vijana ambapo kwa Pangani vimewekwa vituo vya zana za kilimo.
Alisema serikali itaendeleza programu hiyo, awamu kwa awamu katika maeneo mbalimbali nchini huku Pangani itaanza na maeneo ya Mseko, Kipumbwi na Kigurusimba.
Katika afya alisema serikali kutokana na uboreshaji huduma hizo, juzi akiwa Bagamoyo alipata taarifa kwamba, kwa mwaka mzima hakujatokea kifo cha mjamzito wilayani humo.
Alisema serikali itaendelea kuongeza upatikanaji huduma za afya, vitendeakazi, vifaa tiba, upatikanaji madawa na ongezeko la watumishi.
Kwa upande wa maji, alieleza kuwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ambaye ni mgombea ubunge katika jimbo hilo, amefanyakazi kubwa.
Alisema kiongozi huyo alipopewa dhamana ya kuongoza Wizara ya Maji amefanyakazi kubwa na ndiyo sababu kitaifa upatikanaji maji umefikia zaidi ya asilimia 80.
“Miaka mitano ijayo tunakwenda kuondoa kadhia ya upatikanaji maji safi na salama kote Tanzania kwa hiyo kijana (Aweso) amefanyakazi kubwa,” alibainisha.
Akizungumzia elimu, alisema ahadi yake ni kuongeza miundombinu ya elimu, kutoa vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na kutoa elimu bila malipo.
Dk. Samia alitumia wasaa huo, kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kukipigia kura CCM katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
“Nawaomba mkipigie kura Chama Cha Mapinduzi kiendelee kuongoza nchi kwa miaka mitano ijayo ili kiinue utu wa Mtanzania. Ombi langu kwenu tarehe 29 Oktoba tutoke twende pamoja katika vituo vya kura tukapige kura.
“Ombi langu kwa mabalozi usitoke peke yako, toka na nyumba zako twende pamoja tukapige kura. Ombi langu kwa vijana wa maeneo mbalimbali muhakikishe watu wote wametoka kwenda kupiga kura,” alibainisha.
DK. ASHA – ROSE MIGIRO
Naye, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Asha- Rose Migiro, alisema Dk. Samia ni kiongozi mwenye rekodi ya mafanikio.
“Namleta kwenu mgombea ambaye amekamilika, ametosha na ana rekodi ya mafanikio. Mnapokwenda kupiga kura mnapigia maendeleo, ustawi na utu, tunatiki na Dk. Samia,” alisisitiza.
NAPE AFUNGUKA
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye, alisema CCM ilipompitisha Dk. Samia kuwa mgombea wa Urais haikuwa kwa bahati mbaya.
“Hatukukurupuka, siyo kwa bahati mbaya, tulifanya tathmini ya kina tukajiridhisha kwamba, anatosha kwani ni mzalendo mwenye uwezo ni muumini thabiti wa utu wa binaadamu ndiyo maana tumemleta kwenu.
“Sisi CCM tathmini yetu ikatuonyesha siyo tu kwa sababu ya utamaduni ni kwa sababu ameweza na ndiyo maana tukasema tunaendelea naye,” alieleza.
Nape ambaye pia ni mgombea Ubunge Jimbo la Mtama, alisema Dk. Samia aliikuta nchi inakusanya kwa mwaka mapato ya sh. trilioni 18 kwa usimamizi mzuri na uzalendo amesimamia ukusanyaji mapato hadi kufikisha sh. trilioni 32 kwa mwezi.
AWESO ATAJA MATATU
Mgombea Ubunge Jimbo la Pangani, Jumaa Aweso, alimwomba Dk. Samia masuala mbalimbali pindi akipewa ridhaa kuliongoza taifa katika kipindi cha miaka mitano.
Aweso aliomba uwekezaji sekta ya maji, ajira kwa vijana, bandari ya mifugo na boti za kuvusha wananchi katika Mbuga ya Saadan.
Aliomba Mto Pangani utumike zaidi katika miradi ya maji kuboresha maisha ya wananchi na kuendeleza ajira kwa vijana.
Vilevile, aliomba msaada wa boti ili kufungua utalii zaidi katika mbuga ya Saadan pamoja na ujenzi wa bandari maalum ya mifugo.
Naye, Mgombea Ubunge Viti Maalum, Mhandisi Mwanaisha Ulenge, alisema miaka minne ya uongozi wa Dk. Samia imedhihirisha uwezo wake katika kutatua changamoto za Watanzania.




