Na SULEIMAN JONGO,
Geita
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, ametoa maelekezo kwa viongozi wa Chama kuanzia ngazi ya shina, kuhakikisha wananchi wanatoka nyumba kwenda kupiga kura Oktoba 29, mwaka huu, siku ya kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani.
Amesisitiza kuwa, msukumo zaidi uwekwe katika maeneo ambayo wagombea waliosimamishwa na Chama, wamekosa wapinzani wa kuchuana nao kwa kuwa, huko wanaCCM wajisahau kwa kudhani wamepita bila kupigiwa kura.
Wasira alitoa maelekezo hayo, alipozungumza na viongozi wa CCM Wilaya ya Geita, jana, akiwa katika mwendelezo wa kumnadi na kumwombea kura Mgombea Urais kupitia CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan na wagombea ubunge na udiwani, wanaopeperusha bendera ya Chama.
“Mamlaka ya nchi yapo mikononi mwa watu, tungependa watu wengi sana wapige kura na kwa sababu ya mazingira ya uchaguzi wa mwaka huu, kwa mfano, ukija hapa mjini (Geita), yupo ndugu yangu Waja (Mgombea Ubunge Jimbo la Geita Mjini), hana mpinzani, sasa katika mazingira hayo, watu wanaweza kudhani Waja ameshapita kumbe bado.
“Kwa hiyo, twende kwa wanachama, twende kwa wananchi, mabalozi ndiyo nguvu ya chama chetu na chama chetu ni chama cha wanachama na wanachama, wanaongozwa kuanzia nyumba kumi kumi.
“Tunawaomba wakuu wa mashina siku ya kupiga kura, muwatambue wapigakura wote, siyo wanachama tu, wapigakura wote washaurini tu hata wanaotukataa waende (kupiga kura) ili na zao zihesabiwe.
“Wanaosema hapana, waende wakapige kura na wanaosema ndiyo nao waende, halafu tuhesabu (kura) watashika kichwa, waseme hatukujua kama mambo yangekuwa hivi,” alisema.
Wasira alisisitiza kuwa, kila kiongozi anapaswa kuhakikisha wananchi wanapiga kura kuanzia ngazi ya nyumba kumi.
Alieleza kuwa, wananchi wakipiga kura, dunia itafahamu kwamba, uchaguzi umefanyika Tanzania na Watanzania wamepiga kura.
Pia, aliwasisitiza viongozi kuhakikisha Watanzania hawanunui woga wanaouziwa na mitandao ya kijamii.
“Kataa kununua woga, nenda upige kura nchi iko salama na dola ya CCM iko pale, hakuna mtu yeyote atakayechezea chochote,” alisisitiza.




