Na MUSSA YUSUPH
Zanzibar
ZANZIBAR ushindi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hayo ndiyo, yamethibitika baada ya maelfu ya wananchi kufurika katika uwanja wa Maisala mjini Unguja kushuhudia Mgombea Urais kupitia CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, akihitimisha kampeni zake za Urais visiwani hapa.
Katika mkutano huo wa kampeni, Dk. Samia ametoa wito kwa wananchi ifikapo Oktoba 29, mwaka huu, hakuna kubaki nyumbani kwa wenye sifa za kupiga kura, wajitokeze katika vituo kuwachagua viongozi wa CCM.
“Twendeni tukashiriki uchaguzi bila hofu yoyote, kwani vyombo vya ulinzi na usalama vipo timamu wakati wote kuhakikisha usalama wa wananchi wake kabla na baada ya uchaguzi.
“Tunakuja kwa wingi katika mikutano ya kampeni, wingi huu hautakuwa na maana kama hatutautafsiri katika masunduku. Katika viwanja tujae katika masunduku tujaze kura.
“Unapotoka mama au baba, vijana wako walioandikishwa toka nao. Unachopaswa kufanya sasa ni kutambua mapema kituo chako cha kura, nenda kahakiki jina lako, siku ikifika nenda kapigekura,” alieleza Dk. Samia huku shangwe likiibuka kutoka kwa wananchi.
Amesema serikali za CCM (Bara na Zanzibar), zinathamini ahadi zinazotolewa na Chama ambapo kazi kubwa imefanyika katika utekelezaji miradi ya maendeleo.
“Leo nilipokuja nimekwenda moja kwa moja nyumbani Mwanakerekwe. Sikuamini macho yangu nilipoona daraja kubwa, nikawa nampongeza Dk (Hussein Mwinyi) akaniambia hujaliona daraja lingine la amani,” ameeleza.
Dk. Samia amewahakikishia wananchi kwamba, serikali zote zitaendelea kushirikiana katika kufanikisha utekelezaji wa ilani ya uchaguzi.
Kuhusu muungano, amesema serikali zote zitaulinda kwa nguvu zote kwani una faida kwa pande zote mbili.
Vilevile, amesema serikali hizo zitaendelea kushirikiana kuongeza kasi ya maendeleo jumuishi na kutatua changamoto mbalimbali za wananchi.
Miongoni mwa changamoto amezoahidi zitapatiwa ufumbuzi wa kudumu ni kuhakikisha visiwa hivyo vinapata umeme wa kutosha saa 24.
ZANZIBAR ISHARA NJEMA YA USHINDI
Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Asharose Migiro, alisema katika mkutano huo, umeonyesha Zanzibar kuwa ishara njema kwa ushindi wa CCM.
Alieleza kuwa Dk. Samia ni taswira ya uongozi wa bidii, uadilifu na uzalendo kwa kuunganisha Watanzania kwa umoja, amani na mshikamano.
Pia, alieleza kuwa, Dk. Samia kwa kushirikiana na Dk. Mwinyi kwa pamoja wametambua kwamba, maendeleo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo maendeleo ya Zanzibar.
“Ulisisitiza maendeleo hayana mipaka, shida ya mama wa bara ndiyo shida ya mwanamke wa Zanzibar, hakuna ustawi wa Tanzania bila ustawi wa Zanzibar. Dk. Samia alishiriki katika filamu ya ‘Royal Tour.’
“Alishiriki kwa upande wa bara na Zanzibar alishirikiana vyema na mwenzake Dk. Mwinyi. Alipochukua uongozi wa taifa letu alishiriki katika kufanikisha maendeleo ya milenia,” alifafanua.
Alieleza kuwa, maendeleo yanayoshuhudiwa Zanzibar ni fahari kwa Tanzania huku akisisitiza utulivu uliopo ndiyo uliowafanya watalii kuiamini Zanzibar kama kitovu cha uwekezaji.
Alitoa wito kwa wananchi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, mwaka huu kupigakura.
“Tutakapopiga kura siku hiyo tutamtizama Dk. Samia, tutakapopiga kura ya Zanzibar tutamtizama Dk. Mwinyi,” alisisitiza.
WENJE AIPARUA CHADEMA
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Ezekia Wenje, alisema Dk. Samia ameonesha uongozi wa mfano kwa kuamua kuzungumza hata na watu wenye kumpinga.
Hata hivyo, alisema watu hao wametengeneza propaganda kwa kudai kwamba Tanzania haiendeshwi kwa misingi ya kidemokrasia.
Wenje alisema Dk. Samia alipoingia madarakani alifungua milango ya mikutano ya hadhara, maandamano na kufuta kesi 417 za wapinzani kati ya kesi 419.
Alitaja sababu kubwa ya chama hicho kugomea uchaguzi ni kwa sababu ya kushindwa kutunza fedha za uchaguzi huku mgombea wao wa Urais akiwa hana uwezo wa kukusanya fedha hata sh. milioni 100.
Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Mjini Magharibi, Hussein Ayoub, alisema Dk. Samia amekuwa akihubiri amani ndani ya nchi.
Alieleza kuwa, Ilani ya CCM yenye kurasa 303 imetekelezwa ipasavyo kwani zaidi ya kilometa 100.9 za barabara zimeimarishwa hatua ambayo imeongeza kasi katika shughuli za uchukuzi katika mkoa huo.
UJASIRI WA DK. SAMIA
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa, alisema amani na utulivu imechagizwa na Dk. Samia anayeongoza kwa ujasiri na maono kwa maendeleo ya taifa.
Alisema Dk. Samia ni kiongozi mwenye mapenzi na Tanzania ndiyo sababu amekuwa akisisitiza kazi ya kuendelea kujenga taifa.
“Kuna watu wanataka kuleta propaganda kutaka kuonyesha serikali haishughuliki na maisha ya watu. Serikali ya Dk. Samia imeendelea kushughulika na matatizo ya maji kwa sababu inawajali wananchi.
“Imeendelea kujenga hospitali na kuleta vifaa tiba na ndiyo maana halisi ya kazi na utu kwa sababu ni serikali yenye kujali watu wake,” alibainisha.
Alitoa wito kwa vijana kuendelea kuimarisha amani na mshikamano kwani viongozi waasisi wa taifa walijenga mazingira bora kwa kizazi cha sasa.
KERO 15 ZA MUUNGANO ZATATULIWA
Mgombea Ubunge Jimbo la Kikwajuni, Hamad Yusuph Masauni, alisema kazi ya kukiombea kura CCM katika kipindi hiki ni nyepesi kwa sababu ya rekodi nzuri ya utekelezaji ilani ya CCM.
Masauni ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, alisema Dk. Samia amehakikisha nchi imeendelea kuwa yenye amani na utulivu.
Alieleza kuwa amani na utulivu msingi wake ni muungano kwani katika kipindi ambacho muungano umekuwa imara zaidi ni kipindi cha sasa.
Alisema moja ya sababu za mataifa mengi muungano wao kutudumu ni kwa sababu changamoto pindi zinapojitokeza hatua hazichukuliwi.
Masauni alisema katika kipindi cha miaka minne Dk. Samia ametatua kero 15 za muungano.




