Na MWANDISHI WETU
DODOMA
BUNGE limewatangazia wabunge wote wateule kuwasili Dodoma kuanzia Novemba nane hadi 10 mwaka huu, kwa ajili ya usajili na shughuli mbalimbali za kiutawala kabla ya kuanza kwa mkutano wa kwanza wa Bunge la 13.
Kwa mujibu wa Tangazo la Rais katika Gazeti la serikali Toleo Maalumu Na. 11 la Novemba nne mwaka huu, mkutano wa kwanza wa Bunge jipya utafanyika Novemba 11 mwaka huu.
Aidha, taarifa iliyotolewa jijini Dodoma na Katibu wa Bunge, Baraka Leonard imeeleza kuwa, miongoni mwa shughuli zitakazofanyika katika mkutano huo ni kusomwa kwa Tangazo la Rais la kuitisha Bunge, uchaguzi wa Spika, kiapo cha uaminifu kwa wabunge wote na uthibitisho wa uteuzi wa Waziri Mkuu.
Taarifa hiyo imeeleza shughuli nyingine zitakazofanyika ni uchaguzi wa Naibu Spika pamoja na ufunguzi rasmi wa Bunge Jipya utakaoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Vilevile, wabunge wateule wametakiwa kuvaa mavazi rasmi, huku wakiwa na nyaraka muhimu ikiwemo Hati ya Kuchaguliwa, Kitambulisho cha Taifa, Kadi ya Benki, vyeti vya elimu na wasifu binafsi (CV).
Kwa wabunge walio katika ndoa, wanatakiwa kuwasilisha cheti halisi cha ndoa, huku wazazi wakitakiwa kuja na vyeti vya kuzaliwa vya watoto walio chini ya miaka 21.
Pia, utaratibu wa uchaguzi wa Spika na Naibu Spika umetangazwa rasmi kupitia matangazo Na. 14824A na 14824B katika Gazeti la Serikali, ukielekeza namna wagombea watakavyopendekezwa na kupigiwa kura ndani ya Bunge.




