Na NASRA KITANA
UONGOZI wa klabu ya Azam FC umeweka wazi kuwa macho yote yapo katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika michuano hiyo, Azam imepangwa kundi B sambana na Wydad AC ya Morocco, Nairobi United ya Kenya na AS Maniema ya DR Congo.
Akizungumzia na UHURU jijini Dar es Salaam, kuelekea katika michuano hiyo, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Nassor Idrisa ‘Father’ alisema Azam msimu huu imejipanga vizuri kufanya vyema katika michuano hiyo.
“Unaona kwa sasa Azam ina mabadiliko makubwa na hata inavyocheza tofauti na msimu uliopita, hiyo inaonesha ni jinsi gani tunahitaji ushindi na kufika mbali katika mashindano hayo na kuweka rekodi safi,” alisema.
‘Father’ alisema kundi ambalo wamepangwa ni gumu lakini hakuna kinachoshindikana.
“Hapa tunaendelea kujipanga vizuri kuhakikisha tunafanyia kazi upungufu uliotokea katika michezo iliyopita,”alisema.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo alisema kuwa wanajisikia furaha kubwa kufanya kazi na kocha wao, Florent Ibenge ambaye anazidi kukiweka vizuri kikosi chao.
Kabla ya Azam FC kuanza kucheza mechi hizo za kimataifa, itakuwa na mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Azam itacheza ugenini dhidi ya timu ya Namungo, mechi hiyo imepangwa kupigwa Jumapili katika Uwanja wa Majaliwa.




