Na AMINA KASHEBA
BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo, anatarajia kupanda ulingoni kuzichapa katika pambano la ‘Boxing on Boxing Day’, linalotarajiwa kufanyika Desemba 26, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kocha wa Mwakinyo, Kanda Kabongo amesema bondia wake yupo tayari kwa pambano kufuatia kufanya maandalizi ya kutosha.
Amesema anaamini Mwakinyo atafanya vyema katika pambano hilo, japokuwa bado mpinzani wake hajajulikana.
Amesema Mwakinyo alishaingia kambini kwa muda mrefu kuhakikisha anakuwa fiti kupata ushindi na kutoa burudani murua kwa mashabiki wake.
“Tulishaanza mazoezi kwa muda mrefu hivi sasa, Mwakinyo yupo tayari kwa pambano na ninaamini atafanya vyema.
“Japokuwa bado mpinzani wa Mwakinyo hajajulikana, nina imani atafanya vyema kutokana na mazoezi ninayoendelea kumpatia.
“Mwakinyo ana muda mrefu hanajapanda ulingoni, hivyo ni fursa pekee ya mashabiki kujitokeza kwa wingi kwenda kumpa sapoti bondia wao katika pambano hilo,” alisema.
Kocha huyo alisema wamefurahi kuona pambano hilo limehamishiwa Mkoa wa Dar es Salaam baada ya mwanzo kupelekwa Mwanza.
Naye bondia wa ngumi za kulipwa, Debora Mwenda alisema amepata nafasi ya kucheza katika pambano hilo atahakikisha anapambana ili kuibuka kidedea.
Alisema anahitaji kupata ushindi kuwapa furaha mashabiki zake baada ya kufanya vibaya pambano lilofanyika Julai 25, mwaka huu kufuatia kupigwa kwa pointi na mpinzani wake Asia Meshack.




