Na MWANDISHI WETU
GWIJI wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua ametoboa siri ya Prince Dube kuwa atakuwa kama mwokozi wa timu hiyo kwa kufunga mabao katika mechi muhimu kama alivyokuwa Fiston Mayele.
Akizungumza na UHURU Dar es Salaam, Chambua amesema ana imani mchezaji huyo anao uwezo mkubwa wa kufunga mabao.
“Dube amekuwa akikosa baadhi ya nafasi za kufunga na tumekuwa tukimvumila na yeye anatuvumilia,” alisema.
Hata hivyo, Chambua aliongeza Dube ni mshambuliaji mzuri kuliko ‘mastraika’ wengine wanaocheza Ligi Kuu nchini.
“Dube ni mshambuliaji mwenye kipaji, mimi naomba asaidiwe na makocha kumjenga vizuri zaidi, kumbuka Dube alizifunga Yanga na Simba akiwa na Azam, uwezo huo unamfanya kuwavutia makocha wanaokuja Yanga kumpa nafasi ya kucheza,” alisema.
Chambua alizitaja sifa za Dube kuwa ana ‘mikimbio’ ya aina yake ya mshambuliaji ambayo amekuwa akitumia na kufunga mabao kwa kushuka, kukaba na kisha kujiweka katika nafasi ya kufunga mabao.
Gwiji huyo alisema Dube bado anazo sifa hizo lakini, baadhi ya washabiki wanamchukulia tofauti na kumpa wakati mgumu.
“Siku nikikutana na Dube nitampa somo zuri na kumjenga, nina imani atafanya mambo makubwa ndani ya Yanga kama ilivyokuwa kwa Mayele,”alisema Chambua.
KAULI YA KAMWE
Ofisa Habari wa klabu ya Yanga, Ally Kamwe alisema Dube hivi sasa amerudi vizuri na anafanya vizuri.
“Ukweli Dube baada ya kupata sapoti kubwa kutoka kwa uongozi, benchi la ufundi, mashabiki na wanachama kwa ujumla ameanza kurudi vizuri na tuna imani atafanya vizuri zaidi,”alisema ofisa huyo .
Alisema Dube amekuwa akipewa ushirikiano mkubwa na wachezaji wenzake, kitu ambacho kimeanza kumpa nguvu ya kufanya vizuri.
“Kwanza muangalie Dube amebadilika kifundi anashuka kukaba na kupanda, jambo zuri akipata mpira anajua sehemu ya kukaa afunge bao, kitu ambacho kinatupa nguvu wanayanga wote,” alisema.
Aidha, Kamwe alisema Dube ambaye alitoka Azam FC ambayo juzi iliichapa Simba 2-0, atafanya mambo makubwa akikishirikiana na wachezaji wengine wa timu hiyo.
VITU MUHIMU VYA DUBE
Dube ameendelea kuwa mwiba ambapo juzi alifunga bao la ushindi dhidi ya Coastal Union katika pambano lililopigwa Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.Yanga ilishinda 1-0.
Hivi karibuni, Dube alifanya vitu adimu kwa kuwainua mashabiki wa Yanga vitini katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate.
Mchezaji huyo alifunga bao hilo dakika ya 29 kwa njia ya penati.
Bao hilo, alilifunga kufuatia mchezaji moja wa Fountain Gate kuushika mpira akiwa eneo la hatari.
Goli hilo lilikuwa la kwanza kwa Dube kufunga katika Ligi Kuu, kwa msimu wa Mwaka 2025/26 tangu ilipoanza.
Pia, Dube alikuwa mwiba mkali hivi karibuni katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.
Dube alifunga bao la ushindi katika mchezo dhidi ya Far Rabat ya Morocco na kuifanya Yanga kuibuka kidedea.




