Na MWANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa msamaha kwa wafungwa 1,036, miongoni mwao 22 wameachiwa huru na 1,014 wamepunguziwa adhabu zao, watabaki gerezani na kuendelea kutumikia sehemu ya vifungo vilivyobaki.
Dk. Samia amefanya hivyo katika maadhimisho ya miaka 64 ya Uhuru wa Tanzania Bara na ametumia mamlaka aliyopewa chini ya Ibara ya 45 (1)(a) – (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, kutoa msamaha kwa wafungwa kwa masharti.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, msamaha huo wa Rais aliuotoa kwa wafungwa wote wenye sifa stahiki wapunguziwe moja ya sita (1/6) ya adhabu zao wanazozitumikia hivi sasa baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu (1/3), linalotolewa chini ya Kifungu cha 49(1) cha Shería ya Magereza Sura ya 58.
Taarifa hiyo ilisema wafungwa hao sharti wawe wamehukumiwa kifungo cha kuanzia miaka miwili na kuendelea, ambao wametumikia robo ya adhabu zao gerezani na wawe wameingia gerezani kabla ya Oktoba 15, 2025, isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika sharti la 2(i — xvi).
Sehemu ya taarifa hiyo ilisema wafungwa wenye magonjwa ya kudumu au sugu ambão wapo katika hatua ya mwisho, lazima wathibitishwe na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya isipokuwa wafungwa hao wasiwe wametenda makosa yaliyoorodheshwa katika kipengele cha 2(i – xvi).
“Wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini au zaidi, umri huo uthibitishwe na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya isipokuwa wafungwa hawa wasiwe wametenda makosa yaliyoorodheshwa katika kipengele cha 2(i – xvi).
“Wafungwa wa kike walioingia na ujauzito gerezani au wenye watoto wanaonyonya au wasionyonya waliohukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na kuendelea, isipokuwa wafungwa hao wasiwe wametenda makosa yaliyoorodheshwa katika kipengele cha 2(i – xvi),”ilifafanua taarifa hiyo.
Taarifa iliongeza, pia, wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili wasio na uwezo wa kufanya kazi, ulemavu huo uthibitishwe na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya isipokuwa wafungwa hao wasiwe wametenda makosa yaliyoorodheshwa katika kipengele cha 2(i – xvi).
Ililiongeza pia, wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kuwekwa kizuizini (Under President’s Pleasure) ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka kumi zaidi.
WASIOHUSIKA
Aidha, msamaha huo hauwahusishi wafungwa wanaotumikia vifungo vya nje na wale waliowahi kukiuka masharti chini ya Sheria ya Bodi za Parole Sura ya 400 (R.E 2023) na kurudishwa gerezani kutumikia adhabu zao, Sheria ya Huduma kwa Jamii Sura ya 291 (R.E 2023) na Kanuni za Kifungo cha Nje.
Pia, msamaha huo hauwahusu wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo gerezani kwa makosa ya uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka, utakatishaji wa fedha, rushwa na usafirishaji au kujihusisha kwa namna yoyote ile na dawa za kulevya ikiwemo bangi.
“Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo gerezani kwa makosa ya kujamiana, utekaji au wizi wa watoto, kupoka, kuwapa mimba wanafunzi au makosa yoyote yale yanayohusiana na ukatili dhidi ya watoto na kujihusisha kwa namna yoyote ile na biashara haramu ya binadamu.
“Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo gerezani kwa makosa ya unyang’anyi, unyang’anyi wa kutumia nguvu, unyang’anyi wa kutumia silaha, kumiliki silaha, risasi, milipuko au kujaribu kutenda makosa hayo,”.
Pia, msamaha wa Rais hauwahusu wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo gerezani kwa makosa ya kukutwa na viungo vya binadamu, wafungwa wanaotumikia kifungo gerezani kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali au ujangili na wafungwa wanaotumikia kifungo gerezani kwa makosa ya wizi au ubadhilifu wa fedha za Serikali.
Msahamaha huo wa Rais pia hauwahusu wafungwa wanaotumikia vifungo gerezani kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali au kusaidia kutendeka kwa makosa hayo, wafungwa wenye makosa ya kujaribu kuua, kujiua na kuua watoto wachanga.
Pia, msamaha huo hauwahusu wafungwa wenye makosa ya ugaidi, uharamia na makosa ya kimtandao, wafungwa wanaotumikia kifungo cha pili au warudiaji, wafungwa waliowahi kupata msamaha wa Rais na wafungwa waliotenda makosa ya kinidhamu gerezani ambao makosa hayo hayajatimiza miaka mitatu mpaka kufikia Desemba 9, 2025.
Makosa mengine ambayo hayana msamaha wa Rais ni wafungwa wa madeni, wafungwa waliopatikana na hatia ya mauaji au kuhukumiwa adhabu ya kifo na wafungwa wanaotumikia kifungo cha maisha gerezani.
Taarifa hiyo Ilisisitiza kuwa, ni matarajio ya Serikali kuwa wafungwa walioachiliwa huru Desemba 9, mwaka huu, watarejea katika jamii kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.




