>> Fursa za ajira 12,000 sekta ya afya, ualimu, Waziri Ridhiwani asema usaili kufanyika kila mkoa
>> Asema mchakato uko wazi kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma
Na ELIZABETH JOHN
SERIKALI imeanza kutekeleza ahadi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alizoahidi kuzitekeleza ndani ya siku 100 baada ya kuingia madarakani katika kipindi cha pili cha urais wa awamu ya sita.
Akizungumza Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, alisema tayari serikali imetoa ajira 41,500, zikiwemo 12,000 ambazo ni ahadi ya Rais Dk. Samia.
“Katika kufanikisha maelekezo hayo, serikali katika mwaka wa fedha wa 2025/2026, imefanikiwa kutoa vibali vya kazi 41,500, zikiwemo nafasi 12,000 za ajira ambazo ni ahadi ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, nafasi 5,000 ni upande wa afya na 7,000 ni kada ya ualimu wa masomo ya sayansi na hisabati.
“Nafasi hizo, mchakato wake unakuwa wazi kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, tayari ajira 12,000 zimetangazwa, waombaji wenye sifa wameitwa, leo wanatarajiwa kufanyiwa usaili Tanzania Bara, Unguja na Pemba,” alisema.
Kikwete, alisema Ilani ya Uchaguzi ya CCM, imeielekeza serikali kuongeza fursa za ajira kwa vijana, kuongeza kipato kwa wananchi na kupunguza umaskini.
Alisema katika utekelezaji, imeelekeza kuzalisha idadi ya ajira zisizopungua milioni 8.5 kwa vijana kwa sekta rasmi na isiyo rasmi hadi mwaka 2030.
Kwa mujibu wa Kikwete, serikali itaendelea kuhakikisha nafasi za ajira kwa watumishi wa umma, zinawekwa wazi na kushindanishwa kama sera inavyotaka.
Alieleza utekelezaji wa mchakato wa ajira kwa awamu mpya, utaanza leo na kwa mara ya kwanza, usaili utafanyika mikoa yote, lengo ni kupunguza gharama kwa waombaji.
Waziri huyo, alisema usaili wa awamu hiyo, utafanyika kwa kutumia mfumo wa mtandaoni wa ‘online aptitude test’, vituo vitapatikana katika vyuo vikuu, vyuo vya mafunzo na Ufundi Stadi (VETA) na shule zenye maabara za kompyuta.
Aliwataka waombaji kufuatilia taarifa zao katika mfumo wa ajira na kufika vituoni wakiwa na vyeti halisi vinavyohitajika, vikiwemo vya taaluma huku akisema mchakato huo, utakamilika kabla ya mwisho wa mwezi ujao ili kwenda sawa na ahadi ya Rais Dk. Samia.
Akizindua kampeni za uchaguzi mkuu za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Agosti 28 mwaka huu, Kawe Jijini Dar es Salaam, Rais Dk. Samia aliahidi ndani ya siku 100 za uongozi wake, ataboresha huduma za afya kwa kuajiri wahudumu wa afya 5,000 wakiwemo wauguzi na wakunga.
Pia aliahidi kuajiri walimu 7,000 wa masomo ya hisabati na sayansi, ikiwa ni mkakati madhubiti wa kisayansi wa kuhakikisha kila mtoto wa darasa la tatu anaweza kusoma, kuhesabu na kuandika bila shida.
UTENDAJI KWA WATUMISHI
Waziri Kikwete, alisema serikali imejipanga kuimarisha utendaji wa watumishi wa umma na kuendeleza mageuzi ya kidijitali katika utoaji huduma kwa wananchi.
Alisema dhamira ya serikali ni kuondoa matumizi ya karatasi na kufikisha zaidi ya asilimia 80 ya huduma zote katika mifumo ya kidijitali, ifikapo mwaka 2050.
Alisisitiza wizara hiyo, inatekeleza maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, ikiwemo kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kuboresha ufanisi katika utumishi wa umma.
Aidha, alisema serikali imeanza kufanya tathmini ya rasilimali watu, kubaini mahitaji halisi ya watumishi kwa taasisi zote za umma.
“Serikali imeanzisha Daftari la Huduma za Serikali (Government Services Directory – GSD), ambalo linaainisha huduma zote za umma, taratibu, gharama, maeneo ya upatikanaji, njia za mawasiliano na namna ya kuwasilisha maoni. Mfumo huu unarahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu bila kufika ofisini,” alisema.
Waziri huyo alisema mifumo hiyo ni sehemu ya mageuzi ya kidijitali yanayolenga kuongeza uwazi, kupunguza urasimu na kusogeza huduma karibu na wananchi.
Alisema ingawa baadhi ya maeneo ya vijijini bado hayajafikiwa kikamilifu na teknolojia, serikali inaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za mtandao ili wananchi wote wanufaike.
Kuhusu changamoto za uadilifu na maadili ya viongozi na watumishi wa umma, Waziri Kikwete alisema wizara yake itasimamia maelekezo ya Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, kuhusu marekebisho ya sheria za maadili kwa nia ya kuongeza uwajibikaji kwa ngazi zote. Alisema muswada wa marekebisho ya sheria utapelekwa bungeni kuzingatia makundi yote ya watumishi.




