Na DEUSDEDIT UNDOLE
OFISA Habari wa Klabu ya Azam, Hashim Ibwe amesema kikosi chao kimepanga kuanza mazoezi Desemba 23, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Ibwe alisema maandalizi hayo yamelenga kujiandaa kikamilifu kwa mechi zijazo za Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) na nyinginezo.
“Baada tu ya kusimama kwa msimu huu Ligi Kuu ili kupisha AFCON, Azam FC tulitoa mapumziko kwa wachezaji na benchi letu la ufundi, ila tumepanga kurejea mazoezini Desemba 23, mwaka huu,” alisema Ibwe.
Alisema kikosi hicho ambacho msimu huu kinanolewa na Florent Ibenge ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC), kimejipanga kufanya vyema.
Ofisa huyo alisema wamedhamiria kukiongezea nguvu kikosi hicho dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa mwezi ujao.
“Kimsingi Azam FC licha ya kuanza kwetu kwa kusuasua mechi zetu mbili za CAFCC za hatua ya makundi. Lakini tutahakikisha tunaimarisha kikosi chetu ili tuhimili ushindani kwenye michuano hiyo ya pili kwa ukubwa inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF),” alisema ofisa huyo.
Mechi za CAFCC ambazo Azam FC imepoteza ni ile ya ugenini dhidi ya AS Maniema ambayo ilipigwa DRC Novemba 23, mwaka huu ambapo kikosi hicho kilala kwa mabao 2-0 na Novemba 28, mwaka huu katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar wawakilishi hao wa Tanzania Bara walikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Wydad AC ya Morocco.




