Na AMINA KASHEBA
WADAU wa soka nchini wamesema timu ya taifa ‘Taifa Stars’ ikiwa na mpango bora, nidhamu na kujituma katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, itakuwa na nafasi kubwa ya kufanya vyema katika michuano hiyo.
Taifa Stars ni moja ya timu 24 zitakazoshiriki AFCON 2024 inayotarajiwa kuanza Jumapili hii nchini Morocco.
Katika michuano hiyo, Taifa Stars ipo kundi imepangwa kundi C na Nigeria, Tunisia pamoja na Uganda.
Tanzania itaanza ratiba yake Desemba 23, mwaka huu dhidi ya Nigeria.
Hiyo ni mara ya nne kwa Tanzania kushiriki fainali za AFCON ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1980 nchini Nigeria kisha mwaka 2019 nchini Misri na 2023 nchini Ivory Coast ambapo fainali zake zilichezwa mwaka jana.
Katika kundi hilo, Taifa Stars ndiyo timu iliyofuzu fainali hizo mara chache (4), Tunisia mara 22, Nigeria mara 21 wakati Uganda ikitinga mara nane.
Katika kundi hilo, Taifa Stars ndiyo timu pekee ambayo haijawahi kupenya hatua ya mtoano wakati Nigeria ikiwa ni bingwa mara tatu mwaka 1980, 1994 na 2013, Tunisia mara moja mwaka 2004 huku Uganda ikiwahi kushika nafasi ya pili mwaka 1978.
Hata hivyo, wadau wa soka nchini wamesema timu hiyo inayonolewa na Miguel Gamondi, awamu hii ina nafasi kubwa ya kufanya vyema na kuvunja mwiko huo ikiwa itaingia na mpango bora, nidhamu na kujituma.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mchezaji wa zamani wa Simba na Tafa Stars, Zamoyoni Mogella alisema mipango bora, nidhamu na kujitoa kwa wachezaji ndiyo sababu kubwa ya wao kufanya vizuri katika michuano hiyo.
“Sina hofu na ubora wa Kaimu Kocha Mkuu, Miguel Gamondi kwa sababu anatambua wachezaji wa Stars, hivyo ni muda wao kusikiliza maelekezo na mbinu wanazofundisha.
“Maandalizi yakiwa mazuri na wachezaji wakifuata mipango ya mwalimu wakiongeza nidhamu na kujitoa basi watafanya vizuri, haijalishi wanakutana na timu gani,” alisema Mogella.
Mogella aliongeza kuwa, kila nchi inajipanga kuhakikisha inafanya vizuri hivyo Gamondi anatambua ni mipango gani anakwenda nayo katika michuano hiyo.
Kocha wa soka la vijana, Maalim Salehe, alisema mpira sasa umebadilika hivyo hana wasiwasi na Taifa Stars kwa kuwa imejiandaa vyema kufanya vizuri.
“Kuwa na jina kubwa siyo sababu ya kufanya vizuri katika soka kwa sababu baadhi ya mataifa ambayo ni vinara hawajashiriki AFCON, kujipanga, nidhamu ya wachezaji wa Stars italeta matunda kwao.
“Pia, uimara wa mwalimu, Gamondi utaleta picha nzuri kuanza na Nigeria sio sababu ya kusema itashindwa kutamba maana mpira wa hivi sasa umebadilika,” alisema.
Kocha huyo aliongeza kuwa, jambo muhimu kwa wachezaji wanapaswa kuzingatia ni kusikiliza maelekezo ya mwalimu na kuongeza juhudi.
Aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya Watu Wenye Ulemavu ‘Tembo Warriors’, Salvatory Edward alisema Gamondi anafahamu anakwenda katika michuano ya aina gani, hivyo hana shaka na ubora aliokuwa nao.
Alisema hivi sasa Watanzania wanapaswa kuiombea dua timu hiyo kuhakikisha inafanya vyema.
“Kila kitu kinawezekana katika soka kwa sababu kila kocha anajua anakwenda na mipango ya aina gani, kwangu namuamini Gamondi kwa sababu ana mifumo ambayo italeta ushindi kwa Stars,” alisema.




