Na AMINA KASHEBA
PROMOTA wa ngumi za kulipwa, Meja Selemani Semunyu, amesema anahitaji zaidi ya sh. bilioni moja kufanikisha pambano kati ya bondia Hassan Mwakinyo na Twaha Kassim ‘Kiduku’.
Mwakinyo anayeshikilia rekodi ya kuwa bondia namba moja Afrika katika uzito wa kati kupitia Boxrec amekuwa katika vita ya maneno ya muda mrefu na Twaha Kiduku anayepigana uzito wa kati wa juu kila mmoja akitamba kuwa bora zaidi ya mwenzake.
Wakati mashabiki na wadau mbalimbali wa masumbwi wakihitaji kushuhudia miamba hiyo miwili ikitupiana makonde ulingoni, promota Semunyu ambaye amewahi kwa nyakati tofauti kuandaa mapambano mbalimbali kwa mabondia hao, anaamini sh. bilioni moja itafanikisha ‘pambano hilo la historia’.
Meja Semunyu alisema anatamani kuona pambano hilo likifanyika, lakini changamoto anayopitia kwa sasa ni kupata sh. bilioni moja ambayo itafanikisha mtanange huo.
Katika mchanganuo wa fedha hizo, alisema pambano kuu kati ya wawili hao litatumia takriban sh. milioni 500 hadi 600 wakati mapambano ya utangulizi na maandalizi mengine yatagharimu zaidi ya sh. milioni 400.
Semunyu alisema anaendelea kufanya jitihada za kutafuta wadhamini, kuhakikisha pambano hilo linafanyika mwaka huu.
Alisema mabondia hao wako tayari kuzichapa ulingoni, lakini ofa yao ni zaidi ya sh. milioni 500 kwa pamoja.
“Sote tunafahamu hawa wawili walikuwa wanarushiana maneno kwa lengo la kutaka kupigana hivyo wako tayari na mimi ninatamani mwaka huu kuandaa pambano hili.
“Sasa ni muda wa wadhamini kufanikisha pambano hili, nina imani utakuwa mmoja wa mtanange mkubwa nchini kutokana na rekodi zao na uchezaji wa mabondia hawa ambao muda mrefu walikuwa wakitafuta,” alisema.
Promota huyo alisisitiza kuwa, hivi sasa milango ipo wazi kwa wadhamini kutoa sapoti kihakikisha mtanange huo wa kibabe unafanyika.
KIDUKU, KAMBI YA MWAKINYO
Akizungumzia uwezekano wa pambano hilo, Kiduku alikiri yupo tayari kupambana na Mwakinyo kama promota atafikia ofa yake (hakuiweka wazi).
“Niko tayari kupigana maana ngumi ni kazi yangu, pia siku hiyo nitawaonyesha burudani nzuri Watanzania na mashabiki zangu ambao wanatamani kuona pambano hili kwa muda mrefu, siku hiyo nitaonyesha kazi nzuri,” alisema.
Naye Kocha wa Mwakinyo, Amos Nkondo maarufu Amoma, alisema bondia wake yupo tayari kwa pambano isipokuwa wanahitaji kutimiziwa mahitaji yao muhimu ikiwemo ofa.
“Tupo tayari kwa pambano, na uzuri Twaha alisema katika pambano hili atashuka uzito hivyo sioni pingamizi isipokuwa ofa yetu lazima ifikiwe, maana ngumi ni kazi,” alisema.




