Na AMINA KASHEBA
WAKATI timu ya taifa ‘Taifa Stars’ ikionyesha kiwango cha kushangaza katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2025, magwiji wa soka wamesema miamba hiyo inaweza kutikisa katika AFCON mwaka 2027 kama maandalizi yatafanyika mapema na kwa usahihi.
Taifa Stars chini ya Kocha Miguel Gamond iliwashangaza watu wengi Afrika baada ya kuonyesha kiwango bora katika AFCON mwaka huu ikitinga hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza katika historia.
Katika michuano hiyo mikubwa zaidi Afrika, Taifa Stars ilitoka sare dhidi ya Tunisia na Uganda huku ikionyesha ubora ilipochuana na miamba Nigeria na Morocco japokuwa ilipoteza.
Awali, miamba hiyo ilizoeleka ‘kusindikiza’ wenzao katika michuano hiyo ambapo kabla ya AFCON hii, Taifa Stars ilikuwa na rekodi ya kutocheza hatua ya mtoano ikipoteza mechi sita na kutoka sare tatu kati ya tisa ilizocheza hatua ya makundi.
Lakini kutinga mtoano kumeifanya Taifa Stars kuwa moja na timu 16 bora zilizopenya hatua hiyo katika AFCON hii ambayo imekuwa na ushindani mkubwa.
Kiwango hicho kimewafanya magwiji wa soka nchini waliokipiga timu hiyo kuamini kwamba kuna kila sababu ya Stars kutikisa katika AFCON ya mwakani itakayopigwa Tanzania, Kenya na Uganda.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mchezaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Idd Pazi alisema kikosi hicho kina nafasi ya kufanya vizuri katika AFCON 2027 kama kitafanya maandalizi mapema.
“Mwalimu Miguel Gamondi anafaa kupewa mikoba rasmi, pia tumeona wachezaji wakipambana kwa ari ya juu kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika kila mchezo, nafikiri hakuna cha kutusimamisha kufanya vyema kama tutakuwa na maandalizi bora,” alisema.
Kiungo wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella, alisema Taifa Stars ya sasa ni tofauti ya awali, ubora wake sasa umeongezeka na anaamini utazidi kufikia AFCON 2027.
Alisema ana imani Stars itafanya vizuri kwa sababu Gamondi atapata muda wa kuandaa mkakati wake ambao atautumia katika maandalizi ya AFCON msimu unaokuja ili kufika mbali zaidi.
“Maandalizi ya mapema ndiyo yanahitajika kwa Stars nina imani watafanya vizuri kutokana aina ya mfumo wa mwalimu wao, Gamondi kitu kingine wachezaji wakianza kujiandaa itawapa muda wa kujipanga,” alisema.




