Na REHEMA MOHAMED
RAIA wawili wa China, wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashitaka mawili ya kuongoza genge la uhalifu na kujipatia zaidi ya Dola la Marekani 707,075 (sawa na zaidi ya sh. bilioni 1.7) na sh. 281,710,000 kwa njia ya udanganyifu.
Weisi Wang na Yao Licong walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.
Wakili wa Serikali, Benjamin Muroto, akishirikiana na Wakili wa Serikali, Patrick Mwita, alidai kati ya Desemba Mosi, 2024 hadi Desemba 30, mwaka jana, washitakiwa waliongoza genge la uhalifu.
Muroto alidai washitakiwa walitenda kosa hilo katika Mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza na Kisiwani Unguja, Zanzibar na sehemu nyingine ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alidai Wang na Licong wakiwa maeneo hayo waliongoza genge la uhalifu kwa kutengeneza Kadi za Benki (ATM CARD) zenye taarifa za kughushi, kukwepa kodi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Pia, washitakiwa wanadaiwa katika tarehe na meneo hayo, kwa vitendo vyao walijipatia Dola za Marekani 707,075 na sh. 281,710,000, huku wakijua fedha hizo ni mazalia ya kosa la kuendesha genge la uhalifu.
Baada ya kusomewa mashitaka, Hakimu aliwaeleza washitakiwa kuwa hawapaswi kujibu lolote kwa ababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi, bali Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, upelelezi utakapokamilika.
Pia, aliwaeleza hawatapata dhamana kwa sababu shtaka la utakatishaji fedha halina dhamana, hivyo watapelekwa mahabusu.
Shauri hilo liliahirishwa hadi Januari 21, mwaka huu, kwa kutajwa.




