Na NASRA KITANA
UNAWEZA kusema Simba hii gusa unase baada ya jana, kuitandika Mighty Wanderers ya Malawi kwa mabao 6-1.
Matokeo ya mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), yameifanya Simba kutinga hatua inayofuata kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-1.
Timu hizo za Simba na Mighty Wanderers zilishuka dimbani katika mchezo huo wa marudiano wa raundi ya awali, uliopigwa kuanzia saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Wekundu wa Msimbazi katika mchezo wa kwanza, walishinda bao 1-0 wakiwa ugenini.
Katika pambano hilo la jana, Simba ilipata bao la kuongoza dakika ya saba ya mchezo kupitia kwa Clatous Chama kwa shuti kali, Chama alimalizia pasi safi kutoka kwa Anicet Oura.
Kasi ya Simba iliongezeka katika dakika ya 26 ya mchezo huo, baada ya Libasse Gueye kupiga shuti kali na mpira kutinga wavuni, Gueye alipokea pasi kutoka kwa Elie Mpanzu.
Bao la tatu la Simba, lilipachikwa wavuni na Chama katika dakika ya 33 baada ya kupokea mpira kutoka kwa Oura.
Dakika ya 69, Gueye alifunga bao la nne huku bao la tano lilipachikwa wavuni dakika ya 88 na Keletso Makgalwa.
Makgwala alimalizia pasi kutoka kwa Ismail Mgunda ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Gueye.
Bao la sita, lilipachikwa wavuni na Morice Abraham aliyeingia dakika ya 62 ya mchezo akichukua nafasi ya Chama ambapo alipiga shuti kali lililotinga wavuni.
Kufuatia ushindi huo, Simba itakutana na timu ya FC 15 de Agosto de Akonibe ya Guinea ya Ikweta.
Timu hiyo ya Guinea Ikweta ilifanikiwa kutinga hatua nyingine baada ya kuitoa Fomboni FC ya Comoros katika raundi ya pili ya mchujo.
Awali, pambano hilo, lilianza kwa kasi huku timu zote zikishambuliana kwa zamu ambapo dakika ya tatu ya mchezo, Mpanzu alikosa bao baada ya kupiga shuti kali na kipa wa Mighty Wanderers, Dalitso Phiri aliokoa.
Mighty Wanderers walijibu ambapo dakika ya nne, Lameck Mithi alipiga shuti kali na mpira ulitoka nje ya lango.
Mighty Wanderers walipata bao la kwanza katika mchezo huo kwa njia ya mkwaju wa penalti,dakika ya 44 iliyopigwa na Isaac Kaliati.
Wanderers walipata mkwaju huo wa penalti baada ya Ismael Toure wa Simba kumfanyia madhambi, nyota wa Wanderers, Clement Nyondo katika eneo la hatari.
Kipindi cha pili, ilianza kwa kutafuta matokeo ambapo dakika ya dakika ya 50,Chama alikosa bao baada ya kupiga shuti kali na kipa ,Phiri aliokoa mpira huo.
Mighty Wanderers katika dakika ya 57, walifanya shambulizi kupitia kwa Thierry Sama ambaye alifumua shuti lililookolewa,kipa Mahamadou Kassali.
Msimu uliopita, Simba iliishia hatua ya makundi ya michuano hiyo ikipangwa na timu za Petro de Luanda, Stade Malien na Esperance de Tunis.
Mara ya mwisho Simba kucheza hatua ya nusu fainali ya CAFCL (zamani Klabu Bingwa Afrika), ilikuwa mwaka 1974.
Wakati huo huo, timu ya Singida Black Stars imesonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kuifunga Al Ghazala kwa jumla ya mabao 10-I.
Simba iliwakilishwa na Mahamadou Kassali, Nathaniel Chilambo, Antony Mligo, Rushine De Reuck, Yusuph Kagoma, Libasse Gueye, Neo Maema, Elie Mpanzu, Clatous Chama na Anicet Oura.
Mighty Wanderers: Dalitso Phiri, Promise Kamwendo, Lameck Mithi, Felix Zulu, Blessings Singini, Gaddie Chirwa, Issac Kaliati, Timothy Silwimba, Rajab Nyirenda, Stanley Sanudi.



