Na NASRA KITANA
SIMBA ni shangwe tu zinaendelea, baada ya kuitandika mabao 6-1 timu ya 15 Agosto ya Guinea Ikweta huku ‘straika’ akitupia mabao mawili.
Pambano hilo la awali la Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), lilipigwa katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam ambapo Doumbia aliondoa gundu la kutofunga mabao tangu alipojiunga na Simba.
Doumbia aliyesajiliwa Simba, msimu huu, akitokea AS Korofina ya Mali, kwa mkataba wa miaka miwili, alionekana kulaumiwa na mashabiki wa soka nchini kutokana na kutoridhishwa na kiwango chake, lakini jana alidhihirisha ubora wake huku akiingia wavuni mara mbili.
Staa huyo, raia wa Mali, msimu uliopita alionesha kiwango bora na kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Mali, akipachika mabao 17.
Tangu Ligi Kuu Tanzania Bara ianze kutimua vumbi Agosti 14, mwaka huu, Doumbia jana ndiyo alifungua akaunti yake ya mabao na kushangiliwa sana na mashabiki wa soka waliofika uwanjani hapo.
Katika mchezo huo, mpira ulianza kwa kasi huku kila timu zikishambuliana kwa zamu na dakika ya 15, Neo Maema alipata nafasi na kupiga shuti lililotoka nje ya lango.
Katika dakika ya 32, Simba walifanya shambulizi la kushitukiza, ambapo Libasse Gueye alipiga shuti kali na mpira kutoka nje ya lango baada ya kupokea pasi kutoka kwa Clatous Chama.
Simba waliendelea kulisakama lango la 15 de Agosto kama nyuki, dakika ya 35 Chama alishindwa kutumia vyema nafasi aliyoipata na mpira kuokolewa na kipa.
Mchezaji wa Simba, Anicet Oura nusura aipatie bao timu yake katika dakika ya 42 kufuatia kufumua shuti kali akiwa nje ya eneo la hatari mpira ukatoka nje ya lango.
Katika dakika ya 43, staa wa Simba, Nathaniel Chilambo aliwainua mashabiki wa klabu hiyo, baada ya kupachika bao la kwanza kwa kichwa kufuatia mabeki wa 15 Agosto kujichanganya na mpira kujaa wavuni, hadi mapumziko ya kipindi cha kwanza Simba ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, Simba walifanya shambulizi la kushitukiza dakika ya 55 ambapo Elie Mpanzu alifunga bao la pili kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Libasse Gueye.
Wakitandaza kandanda safi huku wakigongena pasi fupi fupi, Simba walipata bao la tatu lililowekwa kimiani na Doumbia baada ya kuwazidi ujanja mabeki na kumtoka kipa na kuujaza mpira wavuni moja kwa moja.
Katika dakika ya 71, Simba ilipata bao la nne kupitia kwa Kaletso Makgalwa kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Morice Abraham.
Simba walifanya shambulizi jingine, dakika ya 81, Oura alifunga bao la tano kwa shuti kali baada ya kupokea pasi murua kutoka kwa Morice.
Doumbia ambaye alionesha kiwango bora katika mchezo huo wa jana, alifunga bao la sita katika dakika ya 87 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Morice.
15 de Agosto walipata bao la kufutia machozi katika dakika ya 90 lililowekwa kimiani na mchezaji wake, Alonze Uwandu kufuatia mabeki wa Simba kujichanganya.
Hadi mpira unamalizika, Simba iliibuka kidedea kwa ushindi mnono wa mabao 6-1.
Simba ilifanikiwa kutinga hatua ya pili raundi ya awali ya CAFCL kwa kuifunga Mighty Wanderers ya Malawi kwa jumla ya mabao 7-1, mechi ya kwanza ugenini ikishinda 1-0 kabla ya kuirarua 6-1 ikiwa nyumbani.
Kikosi cha Simba: Djibrilla Kassali, Nathaniel Chilambo, Antony Mligo, Ismael Toure, Rushine De Reuck, Yusuf Kagoma, Libasse Gueye/Bakari Msimu, Neo Maema/ Morice Abraham, Elie Mpanzu/ Kaletso Makgalwa, Clatous Chama/ Ibrahim Doumbia na Anicet Oura.




