Na MWANDISHI WETU
SERIKALI inaendelea kuweka mkazo maalumu kuboresha mfumo wa uratibu na upatikanaji wa mafunzo tarajali kwa kuwapa wahitimu wa kada mbalimbali, uzoefu na ujuzi unaohitajika kwa lengo la kuwafanya kuwa shindani katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.
Akiongoza kikao cha makatibu wakuu kilichofanyika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dk. Jim Yonazi, amesema uboreshaji unaoendelea kufanyika ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais Deogratius Ndejembi.
Makamu wa Rais akimwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma Septemba 28, 2026 jijini Arusha, alielekeza kuandaliwa mpango wa mafunzo kwa vitendo kuwawezesha angalau vijana 10,000 kupata uzoefu katika mashirika ya umma na wengine 20,000 katika sekta binafsi.
Ndejembi amesema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususani nguzo ya pili inayosisitiza maendeleo ya watu na rasilimali watu nchini.
Katika kikao hicho cha makatibu wakuu, Dk. Yonazi amesema serikali inaendelea kuweka kipaumbele kikubwa kwenye masuala ya mafunzo tarajali kuziba pengo la kutokuwa na uzoefu, na kuwapa wahitimu hao uwezo wa kuunganisha elimu ya darasani na uhalisia wa mazingira ya kazi pamoja na kuongeza ushindani karika soko la ajira.
“Mafunzo ya ujuzi na uzoefu wa kazi yanapatikana kupitia taasisi za serikali, vyuo vya ufundi, na programu za kitaifa zinazolenga kuwaandaa vijana kuwa shindani katika soko la ajira,” amesema Dk. Yonazi.
Kikao hicho kimewashirikisha makatibu wakuu wa kisekta kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Wizara ya Fedha, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Ujenzi.




