Na NASRA KITANA
SIKU moja baada ya kutunikiwa tuzo ya heshima na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), wadau wa michezo nchini wamempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuipaisha Tanzania kimataifa katika sekta hiyo.
Dk. Samia, Rais wa Kenya, William Ruto na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni walitunikiwa tuzo hizo jijini Rabat nchini Morocco katika hafla ya tuzo za CAF (CAF Awards 2025).
Watatu hao walitunukiwa tuzo hizo kutokana na nchi hizo za Afrika Mashariki kuandaa kwa mafanikio fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN 2024), zilizofanyika Agosti mwaka huu.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo juzi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa aliishukuru CAF huku akisema kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dk. Samia itaendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha soka linapiga hatua.
Alisema serikali inaendelea kuboresha na kujenga viwanja vya michezo nchini ikiwemo kuendeleza programu ya soka la vijana kwa wanawake na wanaume ili kushiriki katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
“Kwanza tunashukuru kwa tuzo hii mliyotupatia na sapoti kubwa ambayo mmeendelea kutupa kuhakikisha tunaendeleza soka nchini, tunaahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa CAF na FIFA kuhakikisha mchezo wa soka unapiga hatua zaidi,’’ alisema Msigwa.
WADAU WAFUNGUKA
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi na wadau mbalimbali wa michezo wamesema tuzo hiyo ni heshima kubwa kwa Tanzania na itaongeza chachu ya kukua kwa soka nchini.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia alisema: “Nilifurahia kuona tuzo hiyo inakwenda kwa Rais wetu Dk. Samia kwani anastahili kuipata, aliyoyafanya ni makubwa na nina imani ataendelea kufanya mengi zaidi kwa maendeleo ya soka hapa nchini,’’.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, amempongeza Rais Samia kwa tuzo hiyo huku akisema imeonyesha ni kwa kiasi mchango wake katika soka Afrika umeonekana.
Alisema serikali chini ya Dk. Samia imefanya kazi kubwa katika michezo ambapo imejenga miundombinu mbalimbali ikiwemo viwanja vya soka na kufanikiwa kuwa mwenyeji wa michuano ya CHAN na kupata nafasi ya kuandaa AFCON 2027.
Mchezaji wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Ally Mayay, alisema tuzo hiyo ni hatua kubwa katika soka la Tanzania kwani imeonyesha ni kwa kiasi gani nchi imepiga hatua katika soka.
‘’Ni furaha kwetu kwa Rais kutunikiwa tuzo hiyo na hapo ndipo inapooonyesha jinsi gani tumeendelea kisoka na kutambulika kimataifa hivyo tuendelee na kasi ya kufanya vizuri kuanzia ngazi za klabu na timu zetu za taifa,’’ alisema Mayay.
Naye nyota wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella, alisema amefurahia kuona Tanzania imepiga hatua kubwa katika soka.
‘’Hii ni ya thamani kubwa kwetu, mpira wetu sasa umepiga hatua kubwa na Rais Samia amechangia kwa kiasi kikubwa, tunaona timu zetu za Simba na Yanga zikifanya vziuri kimataifa lakini timu ya taifa pia kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa kiukweli tunatakiwa kujivunia katika hilo,’’ alisema.




