NA MUSSA YUSUPH
DODOMA
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amemwelezea aliyekuwa Mbunge wa Peramiho mkoani Ruvuma, marehemu Jenista Mhagama, kuwa alikuwa kiongozi jasiri, mlezi wa wengi ndani ya Bunge, serikalini na alijitoa kwa dhati katika kuwatumikia wananchi.
Pia, alisimama imara kutetea haki, maendeleo na alikuwa nguzo ya matumaini na ustawi kwa wanawake na vijana.
Rais Dk. Samia aliyasema hayo jijini Dodoma alipoongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa marehemu Jenista katika Kanisa Katoliki, Maria – Theresa Ledochowska, Parokia ya Kiwanja cha Ndege.
Misa ya kuaga mwili wa Jenista ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais, Balozi Dk. EmmanuelNchimbi, Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, Spika wa Bunge, Mussa Azan Zungu na Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete.
Dk. Samia alisema Jenista alikuwa mfano wa uongozi uliotawaliwa na nidhamu, uadilifu na hofu ya Mungu.
“Sitosita kusema alikuwa kiongozi jasiri na mlezi wa wengi ndani ya Bunge na serikali, aliyejitoa kwa dhati kuwatumikia wananchi wa jimboni kwake na taifa kwa ujumla. Katika maisha yake ya utumishi alisimama imara kutetea haki, maendeleo na ustawi wa watu aliowaongoza.
“Alikuwa nguzo ya matumaini kwa wanawake na vijana na mfano wa uongozi uliotawaliwa na nidhamu, uadilifu na hofu ya Mungu,” alisema.
Aidha, Rais Dk. Samia aliwasisitiza wabunge na mawaziri umuhimu wa kuzingatia uadilifu na maslahi ya umma.
“Kwa waheshimiwa wabunge na mawaziri hususan wale wapya, niwasihi kufuata nyayo zake (Jenista) kwa namna ifuatavyo. Kwanza, mafanikio ya Bunge na Taifa yanatokana na mshikamano wa wabunge wote bila kujali tofauti za kisiasa.
“Pili, mijadala inabaki katika misingi ya kistaarabu kwa kuhakikisha inalinda misingi ya Bunge kama chombo cha uwakilishi wa wananchi na kutimiza wajibu wenu kwa uadilifu kama ilivyokuwa kwa Jenista Mhagama,”alisema.
Dk. Samia alisema ni vigumu kupata maneno ya maelezo katika msiba mzito kama huo wa kiongozi aliyegusa maisha ya watu wengi.
Alibainisha: “Nashukuru Mungu leo (jana) ndani ya kanisa hili nimepata kuyajua mengi ya maisha yake ya kiroho, nashukuru sana. Nilikuwa namfahamu maisha yake ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).”
Rais Dk. Samia alisema Jenista alikuwa mwalimu kwa taaluma ambaye alitumia kipawa hicho kulea na kusimamia mawaziri akiwa Mnadhimu wa Serikali Bungeni, Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM na Mwenyekiti wa Bunge.
“Wabunge na mawaziri walimheshimu na yeye alijiheshimisha. Katika nafasi zake alitoa mchango mkubwa kwa Chama, Bunge na Baraza la Mawaziri.
“Ndiye mtu pekee katika historia ya nchi yetu aliyewahi kuvaa kofia mbili za Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM na Mnadhimu wa Serikali Bungeni, kofia hizo zilimtosha na kumuenea sawa sawa,” alieleza.
Kwa mujibu wa Dk. Samia, Jenista alikuwa kiongozi asiyekuwa na mzaa lakini mcheshi, alikuwa mtii kwa mamlaka zake, chama chake na wananchi wake.
Vilevile, alisema kiongozi huyo alikuwa mnyenyekevu kwa Mungu wake, suala lililomfanya apendwe, kuheshimiwa na watu waliochini yake pamoja na viongozi wenzake.
“Alipata fursa kufanyakazi chini ya uongozi wangu kama Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu. Waziri wa Nchi, Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Waziri wa Afya.
Alieleza: “Kama alivyosema mwanangu Victor (mtoto wa marehemu) nilimpa jina la kiraka kwamba kila nilipomweka, Jenista aliziba vizuri. Amekuwa kiongozi anayesimama imara kutetea maslahi ya nchi bila kuchoka, bila kujali changamoto,” Dk. Samia alieleza.
Alisema safari ya uongozi kwa Jenista haikuwa rahisi lakini alitembea kwa ujasiri, hekima na heshima.
Dk. Samia alisisitiza kuwa kiongozi huyo atakumbukwa kwa tabasamu lake, hekima na moyo wake wa kujali maslahi ya Taifa.
“Mdogo wangu Jenista Mhagama, umetimiza wajibu wako kwa uaminifu mkubwa, umepigana vita vilivyokupasa. Uimara wa Taifa letu ni pamoja na mchango wako mkubwa. Mwenyezi Mungu akupe safari ya kheri, safari njema na ailaze roho yako mahali pema peponi.
“Sote kwa imani zetu, tunamuomba Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yako kwa amani, milele na milele. Tunamshukuru kwa maisha yako na yote uliyoyafanya kwa familia, jamii na Taifa kwa ujumla,” alisisitiza Rais Samia katika hotuba yake.
MAKAMU WA RAIS DK. NCHIMBI
Awali, Makamu wa Rais, Balozi Dk. Nchimbi, naye alisisitiza umuhimu wa viongozi kuwatumikia vyema wananchi kama ambavyo Jenista alivyofanya.
“Wakati tukitafakari kuhusu kifo cha Jenista, nikawaza sana, nikasema kama Mungu angeniambia niombe kitu kimoja tu. Ningeomba kwamba wabunge wote wa nchi hii, madiwani wote wapende na kutumikia watu wao kwa kiwango cha Jenista Mhagama.
“Tumeletwa duniani siyo tuishi tu, lakini pia kuwatumikia wenzetu. Ni utumishi kwa binadamu wenzetu ndiyo unaotupa heshima kwa Mungu na unaotufanya tukumbukwe kwa kazi tulizofanya,” alisisitiza.
Alisema kwa kipindi ambacho Jenista alitumikia kama Mbunge wa Peramiho, wananchi wa jimbo hilo hawana malalamiko juu yake, kwani alikuwa mtumishi wa kweli kwa watu wake.
“Alikuwa mnyenyekevu, anapenda sana watu wake, kitu alichotanguliza mbele katika maisha yake ya kazi ni kuwatumikiwa wananchi wa Peramiho. Hata alipopata nafasi ya uwaziri, hakuacha kuwatumikia wananchi wa Peramiho.
Alisisitiza: “Aliguswa sana na watu wanyonge wa kawaida ndiyo maana leo wanyonge wa Peramiho wanauchungu zaidi kwa sababu wanajua mpiganaji wao, mtetezi wao ameondoka, ametanguliwa mbele ya haki.”
SALAMU WA BUNGE
Akitoa salamu za Bunge, Spika wa Bunge, Mussa Zungu, alisema Jenista alikuwa kiongozi mahiri aliyeipenda nchi na kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
“Tangu nilipoingia Bungeni, alipenda kuniita mwanangu na mimi nikimuita Mama. Tuliishi vizuri sana, kikubwa kumuombea dua, sala na maombi, Mwenyezi Mungu ampokee amweke mahali pema.
Alieleza: “Nakushuru Mheshimiwa Rais kwa namna ulivyokuwa karibu na Bunge katika tukio hili na misiba ambayo tunayoipata, hasa kwa jana (juzi) ulivyotupatia ndege kupeleka mwili wa ndugu yetu na familia kwenda kumpumzisha Songea.”
“Niwaombe familia, msiba huu ni mzito sana, shikamaneni, pendaneni, msisikilize maneno ya kuwagawa. Hakuna jambo ambalo Mungu analipenda kama umoja wa familia, mmekuwa wenye bahati kuwa na mama mwenye wema, endelezeni wema wake,” alisisitiza.
MTOTO MAREHEMU
Naye mtoto wa marehemu Jenista, Victor Mhagama alisema, marehemu Jenista aliamini katika kuchapa kazi, aliwasisitiza vijana wake katika kuchapa kazi na uchaji wa Mungu.
Alisema marehemu Jenista aliipenda nchi yake na kuamini katika maendeleo, alipenda katika kujifunza na alipenda jambo analofanya liwe na matokeo.
“Mama alitusihi wote tuliyopita katika mikono yake uchaji wa Mungu, uchapakazi, elimu ukienda kwake vitabu tu vimejaa mama alipenda kusoma na wakati mwingine alisema Victor mimi ni Mbunge wa muda mrefu senator mchango wangu lazima uwe mzuri,” alisema.
Aidha Victor alimshukuru Rais Dk. Samia kwa namna alivyofuatilia kwa karibu katika muda mfupi wa kuugua kwa marehemu Jenista.
Pia alimshukuru Rais Dk. Samia, Rais wa Awamu ya Nne Dk. Jakaya Kikwete, Hayati Dk. John Magufuli, kwa kumuamini Jenista kwa kumpatia nafasi mbalimbali za uongozi katika serikali.
“Mama huyu alikuwa wa kipee sana kuna siku za sikukuu alikwenda kazini, nikamuuliza mama kwa nini unakwenda kazini, akaniuliza Victor nisipoijenga nchi ataijenga nani, tumsaidie Mheshimiwa Rais ana majukumu mengi.
Padri
Naye Padri Emanuel Mtambo, Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Maria Teresa Ledochawska, Kiwanja cha Ndege, alisema marehemu alikuwa na unyenyekevu wa aina yake, alikuwa mpenzi wa Yesu Kristo,
Alisema marehemu alikuwa anapeleka kanisani michango kwa ajili ya wahitaji na maskini.
WASIFU
Kwa mujibu wa Katibu wa Bunge Baraka Leonard Jenista alizaliwa Juni 23, mwaka 1967 kijiji cha Palangu – Peramiho mkoani Ruvuma.
Elimu
Katibu wa Bunge alisema Jenista alizaliwa Juni 23 mwaka 1957 na kusoma elimu ya msingi shule ya Mfalanyaki, Songea mkoani Ruvuma mwaka 1975 hadi mwaka 1981.
Pia alisema mwaka 1982 hadi 1985 Jenista alisoma elimu ya Sekondari katika Shule ya Wasichana ya Peramiho, huku mwaka 1986 hadi mwaka 1989 alisoma Chuo cha Ualimu Korogwe na kuhitimu Elimu ya Juu ya Sekondari na Stashahada ya Ualimu.
Mwaka 1999 alihitimu na kutunukiwa Stashahada ya Ujasiriamali Kituo cha Kimataifa cha Mafunzo kwa Wafanyakazi nchini Italia.
Aidha mwaka 2004 alihitimu Chuo cha Cambridge nchini Uingereza kwa kutunikiwa Shahada ya Juu ya Kimataifa ya Uongozi na Utawala.
Alisema hadi umauti unamkuta Jenista alikuwa akiendelea na masomo ya Shahada ya Uzamili katika Biashara katika Chuo cha Cambridge nchini Uingereza.
Aliongeza kuwa katika uhai wake, Jenista alihudhulia na kukamilisha mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi, yaliyohusu uratibu wa miradi, usimamizi wa rasilimali watu na utawala bora
Kazi na Ajira
Aliwahi kuwa mwalimu wa Shule ya Sekondari Songea Girls mwaka 1990 hadi 1997
Katibu wa Bunge alisema mwaka 2000 hadi 2005 alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Ruvuma, mwaka 2005 hadi 2025 alikuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho.
Mwaka 2005 hadi 2010aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii.
Aliongeza kuwa mwaka 2006 hadi 2010 alikuwa Mwenyekiti wa Bunge katika Bunge la tisa na la 10.
Mwaka 2015 hadi mwaka 2017 alikuwa Katibu wa Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
Pia alisema mwaka 2014 hadi 2015 alikuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwaka 2015 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu.
Vilevile Katibu alisema mwaka 2020 hadi 2022 alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi Vijana na Wenye Ulemavu. Mwaka 2022/2023 alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Pia alisema mwaka 2023 hadi mwaka 2024 Jenista alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, huku mwaka 2024 hadi 2025 alikuwa Waziri wa Afya.
HALI ILIVYOKUWA
Mamia ya wananchi wakiongozwa na viongozi mbalimbali walianza kumiminika kanisa hapo kuanzia saa nne asubuhi tayari kuanza misa hiyo ambapo hadi kufika saa sita mchana, kanisa hilo lilisheheni wingi wa waombolezaji.
Mara baada ya Rais Dk. Samia kuwasili kanisani hapo saa sita mchana, ilipofikia saa 6:46 mwili wa marehemu uliwasili kanisani ndani ya jeneza lililofunikwa bendera ya Bunge.
Viongozi wengine waliohudhuria ibada hiyo ni Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, viongozi wakuu wastaafu wakiongozwa na Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais Mstaafu, Dk. Philip Mpango na Waziri Mkuu Mstaafu Kassim Majaliwa.
Viongozi wengine ni Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Asharose Migiro, mawaziri, manaibu mawaziri, makatibu wakuu, wabunge na wakuu wa taasisi na idara mbalimbali za serikali.
Baada ya kukamilika kwa misa hiyo, mwili wa marehemu ulisafirishwa kwenda nyumbani kwake, Makambi wilayani Songea mkoani Ruvuma, ambako maziko yanatarajiwa kufanyika Desemba 16 mwaka huu, Kijiji cha Ruanda, wilayani Mbinga.




