Na ATHNATH MKIRAMWENI
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ametangaza mikakati mikubwa ya kunufaika na uchumi wa bahari ukiwemo kununua meli, kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) na kuunganisha teknolojia ya kisasa.
Rais Dk. Samia aliainisha mikakati hiyo jijini Dar es Salaam, katika hafla ya uzinduzi wa meli ya kwanza ya uvuvi katika bahari kuu, uliofayika katika viwanja vya Chuo cha Mwalimu Nyerere, Kigamboni na kusema lengo ni kuimarisha sekta ya uvuvi kufanya vizuri katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
BANDARI ZA UVUVI
Kuhusu bandari za uvuvi, alisema serikali inaendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu muhimu zikiwemo bandari hizo za uvuvi na kubainisha kuwa, ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa umefikia hatua ya juu ya ukamilishaji.
Rais Dk. Samia alieleza kuwa, pamoja na mradi huo wa Kilwa, serikali ina mpango wa kujenga bandari nyingine ya uvuvi katika eneo la Bagamoyo, hatua itakayopanua uwezo wa nchi katika shughuli za uvuvi wa bahari kuu.
Aliongeza kuwa, ujenzi wa bandari hiyo utaenda pamoja na kuanzishwa kwa eneo huru la kiuchumi litakalohusisha shughuli za uvuvi na kuimarisha viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi.
Rais Dk. Samia alisema hatua hizo, zinalenga kuongeza uzalishaji, kufungua fursa za ajira kwa wananchi na kuimarisha usalama wa chakula kupitia upatikanaji wa mazao ya baharini.
UNUNUZI MELI NNE
Aidha, alibainisha kuwa serikali inaendelea na mpango wa kununua meli nyingine nne za uvuvi, meli ya mafunzo na utafiti, kwa lengo la kujenga uwezo wa taifa kushiriki kikamilifu katika uvuvi wa bahari kuu.
Alisisitiza kuwa, uwekezaji huo utaenda pamoja na kuimarisha mafunzo, utafiti wa kitaalamu na mifumo ya usimamizi wa sekta kuhakikisha rasilimali za bahari na maziwa zinasimamiwa kwa ufanisi kwa kuzingatia misingi endelevu.
“Hatua zinaendelea za ununuzi wa meli nyingine nne za uvuvi na meli ya mafunzo ya utafiti kama waziri alivyosema hapa, tutafanya hivi kujenga uwezo wa taifa kushiriki kikamilifu katika uvuvi wa bahari kuu,” alisema.
KUFUFUA TAFICO
Rais Dk. Samia alisema serikali imedhamiria kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), kuimarisha usimamizi wa rasilimali za bahari kuu na kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika uchumi wa taifa.
“Hatua hii inalenga kurejesha uwezo wa taifa kushiriki kikamilifu katika uvuvi wa bahari kuu, ambao kwa muda mrefu umefanywa na kampuni za nje, hali iliyopunguza manufaa kwa wananchi na mapato ya serikali,” alisema.
Alisema kufufuliwa kwa TAFICO kutaendana na uwekezaji wa vifaa na teknolojia za kisasa, kuongeza ufanisi na ushindani wa shirika hilo katika shughuli za uvuvi wa kimataifa.
Rais Dk. Samia alisema kupitia mkakati huo, nchi itadhibiti vyema rasilimali zake za bahari na kuhakikisha zinatumika kwa manufaa ya Watanzania, huku ajira zaidi zikitarajiwa kufunguliwa kwa vijana.
Mkuu wa nchi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za serikali katika kuhakikisha shirika hilo linaendeshwa kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji.
Pia, alisema serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu na mifumo ya usimamizi kuhakikisha TAFICO inakuwa imara na endelevu, huku mafanikio yake yakitegemea nidhamu na matumizi sahihi ya rasilimali.
Aliongeza kuwa, hatua hiyo ni ya kimkakati katika kulinda rasilimali za taifa na kukuza uchumi wa buluu, huku ukitarajiwa kuongeza tija na mchango wa sekta ya uvuvi katika maendeleo ya nchi.
Rais alieleza kuwa kwa muda mrefu uvuvi wa bahari kuu, umekuwa ukifanywa na meli na kampuni kutoka nje ya nchi, hali iliyopunguza mapato ya taifa na manufaa kwa wananchi.
MAELEKEZO MATANO
Pia, Rais Dk. Samia alitoa maelekezo matano kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, yanayotarajiwa kuimarisha sekta ya uvuvi na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.
Mosi, Rais Dk. Samia alisisitiza kuwa, watendaji wa wizara wanapaswa kushikamana na kwenda kwa kasi katika utekelezaji wa majukumu yao, kufanikisha malengo ya mageuzi ya sekta hiyo.
Alieleza kuwa, dhamira ya serikali ni kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinawanufaisha wananchi na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya nchi.
Pili, alielekeza umuhimu wa kutunza na kuendesha kwa ufanisi vyombo vinavyonunuliwa kwa shughuli za uvuvi, vidumu na kuleta manufaa ya muda mrefu.
Alionya kuwa, bila usimamizi mzuri wa rasilimali hizo, juhudi za serikali katika kuwekeza katika sekta hiyo zitakosa tija.
Tatu, Rais Dk. Samia alitambua changamoto zinazowakabili wavuvi wadogo na kuagiza wizara kuendelea kuzishughulikia kwa kuwapatia mitaji, teknolojia na masoko.
Alisema hatua hiyo itawawezesha wavuvi kuongeza uzalishaji na kuboresha kipato chao.
Nne, alisisitiza utoaji wa elimu ya ujasiriamali na utunzaji wa fedha kwa wavuvi wanufaike zaidi na shughuli zao, akieleza elimu hiyo itasaidia kuongeza thamani ya kazi mazao na kuboresha maisha yao.
Tano, Rais Dk. Samia alielekeza kuimarishwa kwa mikakati ya kudhibiti uvuvi haramu kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.
Alisisitiza kuwa, uvuvi endelevu ni muhimu kwa kulinda rasilimali za maji kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Rais Dk. Samia alieleza kuwa, hatua hiyo ni mwanzo wa mageuzi makubwa katika sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu kwa ujumla.
WAZIRI BASHIRU
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dk. Bashiru Ally, alisema uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika sekta ya uvuvi, umeanza kuzaa matunda hususan kupitia maendeleo ya miundombinu ya bandari ya uvuvi ya Kilwa na masoko ambayo yamefikia asilimia 97 ya ukamilishaji, huku hatua iliyobaki ikiwa ni upimaji wa mitambo kabla ya uzinduzi rasmi.
Dk. Bashiru alisema hatua ya kuanza kufikia dhamira ya nchi kunufaika na rasilimali za uvuvi wa bahari kuu ni kubwa, baada ya jitihada za muda mrefu hivyo uwekezaji huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa samaki kwa soko la nje na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Pia, serikali inaendelea na uwekezaji mkubwa kupitia mradi wa kuendeleza usimamizi wa uvuvi na ukuzaji viumbe maji wenye thamani ya dola milioni 117, utakaotekelezwa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia kwa miaka mitano,
Balozi Dk. Bashiru alisema mradi huo umelenga kujenga miundombinu, kuimarisha tafiti na mafunzo na kuwezesha upatikanaji wa wataalamu kuifanya Tanzania kushiriki kikamilifu katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu.






